Ishu ya Kakolanya bado moto!

Tuesday December 4 2018

 

By Mwanahiba Richard

MENEJA wa Beno Kakolanya, Seleman Haroub amesema hakuna barua iliyoandikwa kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wala Yanga kuhusu madai ya mchezaji wake ila wanafikiria kuwasilisha barua hiyo Yanga muda wowote.

Kakolanya anayeichezea Yanga anaidai klabu hiyo pesa ya usajili pamoja na mishahara, madai ambayo yamemfanya ashindwe kujiunga na kikosi chake ambacho jana Jumatatu kilikuwa uwanjani dhidi ya Prisons pale Sokoine, Mbeya.

Habari ambazo zilienezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kipa huyo anaweza kuondoka Yanga na kujiunga na watani zao, Simba Haroub amesema hazipo na hakuna barua yoyote iliyoandikwa.

“Watu hutengeneza maneno, nafahamu taratibu za kudai masilahi ya mchezaji, hatuwezi kukurupuka na kwenda TFF kupeleka madai yetu, kinachotakiwa kufanywa tena kwa weledi mkubwa ni kufanya mazungumzo na Yanga ambapo tumeyafanya kwa mdomo.

“Baadaye ndipo tutafikiria kuandika barua ya kupeana muda wa kulipa madeni hayo na barua hiyo kopi yake itakwenda TFF, tukiona mambo bado magumu ndipo tutaandika barua moja kwa moja TFF ya kuomba msaada, huo ndio utaratibu na si vinginevyo.

“Sisi sote ni familia moja ya mpira, tunafahamu hali halisi ya uchumi ndani ya Yanga ingawa hatumaanishi kuwa wasitulipe, hakuna mpango wowote wa Beno kujiunga Simba na siwezi kufanya hivyo, sitakuwa muungwana kwani hatujachukua hatua yoyote ya kudai kiofisi kwa maana ya kuwaandikia barua,” alisema Haroub ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba upande wa klabu.

TFF nayo ilikanusha juu ya taarifa hizo zilizozagaa mitandano kuwa hakuna kikao chochote kilichokaa cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kujadili suala hilo.

Katika taarifa hizo zilizosambaa zilieleza kamati hiyo imethibitisha Kakolanya ni mchezaji huru baada ya Yanga kushindwa kumlipa madeni yake ambayo ni pesa ya usajili na mishahara.

Hata hivyo, akihojiwa jana Jumatatu, muda mfupi kabla ya mechi na Tanzania Prisons, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera, alisema hawezi kumtafuta mchezaji ambaye haonekani mazoezi na jukumu la kutoa taarifa kutokuwepo ni la mchezaji sio kocha.

Amesema hastahili na hana sababu ya kumtafuta mchezaji na Kakolanya alipaswa kupiga simu kwake ama viongozi wa Yanga kuwajulisha sababu za kutoonekana kwake, lakini yote hayo hayakufanyika, hivyo ataendelea kuwa kimya tu.

“Jukumu la kocha sio kumtafuta mchezaji ambaye haonekani mazoezini, hiyo ni kazi ya mchezaji husika kueleza kwanini hatakuwepo kwa kocha ama viongozi,” alisema kocha huyo kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Congo.

“Sipaswi na sina kawaida ya kumtafuta mchezaji. Kama haonekani, basi itabaki hivyo, nami nitaendelea kufanya kazi na wachezaji ambao wapo kwenye kikosi kwani, wana uwezo mkubwa,” aliongeza Zahera.

Advertisement