Inter yaimiminia mvua ya mabao AC Milan

Muktasari:

  • Inter Milan imeongeza kasi ya ushindani katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Italia, baada ya kuilaza AC Milan katika mchezo wa derby ya San Siro.

Rome, Italia. Antonio Conte amepania kutwaa ubingwa wa Italia msimu huu baada ya kuendeleza rekodi ya kushinda katika mechi zake.

Ushindi wa jana wa mabao 4-2 dhidi ya watani wao wa jadi AC Milan umeifanya timu hiyo kucheza mechi 16 bila kupoteza.

Inter Milan imekwea hadi nafasi ya kwanza na kuiporomosha  Juventus ambayo imekuwa kileleni muda mrefu.

Kocha huyo alisema anataka kutimiza ndoto ya kuipa ubingwa Inter Milan licha ya kukabiliana na upinzani mkali dhidi ya Juventus na Lazio.

“Tuna ndoto. Tumekuwa tukiimarika kutoka mchezo mmoja hadi mwingine. Hawa vijana wamekuwa wakifanya kazi nzuri,” alisema Conte.

Inter Milan Jumatano keshokutwa itakuwa nyumbani Napoli kabla ya kupepetana na wapinzani wao wanaowania ubingwa huo Lazio.

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Romelu Likuku ameendelea kung’ara baada ya kufunga bao. Inter Milan na Juventus zina pointi 54 zikifuatiwa na Lazio (53) na Atalanta (43).