Ihefu wamtibulia Minziro, Mbeya City yabanwa

Wednesday July 29 2020

 

By YOHANA CHALLE

MICHEZO ya hatua ya mtoano kucheza Ligi Mkuu msimu ujao imechezwa leo, huku timu za Ligi Kuu zikiwa na wakati Mgumu.

Mbao FC ikiwa ugenini Uwanja wa Highland Estates ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililofunga na Steven Mwaijala dakika ya 4 kwa njia ya penalti.

Katika Uwanja wa Nyankumbu wenyeji Geita nao walikwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City likifungwa na.Seleman Ibrahim dakika ya 38.

Kipindi cha pili Ihefu ilijihakikishia ushindi baada ya bao lililofungwa, Mridi Tangai dakika ya 84 na kuifanya timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 2-0.

Kwa ushindi huo Ihefu wametibua rekodi ya kocha wa Mbao, Felix Minziro ambaye hajapoteza mechi nane mfululizo zilizofanya timu hiyo kucheza hatua ya mtoano.

Geita nayo ikarudi mchezoni na kukomboa bao walilofungwa kipindi cha kwanza na Rehan Kibingu kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Advertisement

Ihefu imetinga hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili kundi A ikiwa na alama 51 na baadaye kuitoa Transit Camp hatua ya kwanza ya mtoano kwa penalti 4-2 baada ya sare ya maba 3-3 kwenye michezo miwili waliyokutana.

Geita Gold iliitoa Majimaji FC kwa idadi ya mabao 4-2 na kukutana na Mbeya City iliyomaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Mbao ikimaliza nafasi ya 16.

Nahodha wa Mbao, Wazir Junior anasema wapinzani wao walicheza vizuri na kuhakakisha wanapata ushindi nyumbani.

Kwa upande wake, Yusuph Kinyozi nahodha wa Ihefu anasema mchezo wa marudiano utakuwa mgumu kutokana na kucheza na timu nzuri.

Timu hizo zitarudiana Jumamosi wiki hii, kwa Mbao FC kuwa nyumbani na Mbeya City ikiwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya na mshindi wa jumla atapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Advertisement