Huyu dogo anapita mulemule mwa Samatta-2

Muktasari:

Jana aliishia ilivgyobaki kidogo tu atue Yanga akitokea Serengenti Boys, lakini kilitokea kitu kilichoifanya Singida United wambebe jumla. Ilikuwaje? Endelea naye...

JANA Jumapili tulianza makala ya nyota wa timu ya taifa ya vijana ya Ngorongoro Heroes, Ally Ng’anzi akieleza safari yake kisoka, akiwa na kiu ya kufika alipo Mbwana Samatta.

Samatta, nahodha wa Tanzania anawika Ubelgiji akiichezea KRC Genk akiwa ndiye kinara wa mabao kwa sasa huku timu yake ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Jupiler.

Jana aliishia ilivgyobaki kidogo tu atue Yanga akitokea Serengenti Boys, lakini kilitokea kitu kilichoifanya Singida United wambebe jumla. Ilikuwaje? Endelea naye...

“AFCON ilivyomalizika Yanga ilikuwa timu ya kwanza iliyoonyesha nia ya kunihitaji, sikubabaika wala nini maana lengo langu lilikuwa ni kucheza Ligi Kuu, hivyo sikuangalia ukubwa wa klabu nilijisemea timu itakayokuwa ya kwanza kunipa mkataba nitajiunga nayo.

“Walionyesha nia lakini walichelewa kunipa mkataba, hivyo Singida United wakanifuata na kunipa mkataba, sikuwa na chakupoteza zaidi ya kufanya maamuzi, nikajiunga nayo.”

SINGIDA ILIMDAKAJE?

“Aliyenitafuta alikuwa ni Sanga kupitia simu yake ya mkononi na kueleza wanatamani niwe mchezaji wao, mara moja wakanifuata nilikaongea naye ana kwa ana kisha nikasaini mkataba wa miaka mitatu.

“Nashukuru Mungu, niliishi vizuri na nikajikuta nimekuwa rafiki wa Mudathir Yahya aliyekuwa kama injini ya Hans Pluijm, alinipa moyo kuwa ipo siku nitacheza na kweli ilitokea nafasi nikatumika katika Ligi kama beki wa kulia dhidi dhidi ya Majimaji ya Songea,” anasema.

WAKALA APAGAWA

Baada ya kumalizika kwa Afcon ya vijana, Morfaw aliendelea kumfuatilia Ng’anzi kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes hapo ndipo alipomvulia kofia kiungo huyo kwa kiwango alichokionyesha kwenye mchezo dhidi ya DR Congo.

Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa CCm Kirumba, Mwanza mnamo Machi 31 mwaka jana na wakala huyo alikuwapo uwanjani kunishuhudia.

“Nilicheza vizuri baada ya mechi alitoa ahadi ya kunipeleka Ulaya, nilifurahi sana na niliona Mungu amefungia milango,” anasema.

MWIGULU AHUSIKA

“Uongozi wa Singida, ulivyopata hizo taarifa za kupata wakala aliye tayari kunitafutia timu walifurahi na kusema watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.”

“Siku zilisogea na nikaambiwa nijiandae kuelekea Jamhuri ya Czech ambako ilipatikana timu, Morfaw alinisisitizia kuwa uwezo wangu nitakaoendelea kuonyesha utanifanya anipeleke timu kubwa zaidi,” anasema.

Ng’azi anasema miongoni mwa viongozi wa juu kabisa ambao wameonyesha sapoti ya kukamilika kwa dili lake ni pamoja na mwanasiasa maarufu, Mwigulu Nchemba.

Mbali na Mwigulu kuhusika kwenye dili la Ng’anzi kutua Jamhuri ya Czech pia nyota wa zamani wa Stars na Yanga, Nizar Khalfan kumbe naye amecheza nafasi kubwa ya kukamilika kwa uhamisho wa bwana mdogo huyo wa kujiunga na Vyskov ya daraja la pili nchini humo.

“Niligundua kuwa Nizar naye ni miongoni mwa watu muhimu kwangu, alikuwa akifanya mawasiliano na yule wakala na kila kitu kilivyokamilika aliniambia alicheza naye Vancouver Whitecaps ya Canada iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu Marekani (MLS),” anasema.

ALIVYOTUA KIBABE ULAYA

Ng’anzi anasema baada ya kila kitu kikamilika alitua Jamhuri ya Czech na kukutana na mapokezi mazuri ambayo hakuyategemea,. huku akishangaa uzuri wa taifa hilo, anadai alipelekwa moja kwa moja hadi eneo alilokaa kwa muda.

“Macho yanu yalikuwa yakishangaa miji mbalimbali ambayo tulikuwa tukikatisha, wenyeji wetu walikuwa wakitueleza majina ya kila mji ambao tuliupita hadi, Vyškov mjini.”

Ng’anzi anasema alipotua huko hakuanzia timu kubwa.

“Nilianza kucheza kikosi B huko nilikuwa nikitizamwa na kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza, nilicheza gemu kama tatu hivi, yule kocha aliukubali uwezo wangu ni wakaamua kunipeleka kikosi cha kwanza,” anasema.

KOCHA AMKUBALI GHAFLA

Kiungo huyo anasema mchezo wake wa kwanza kuwa benchi ulikuwa dhidi ya Rymarov, Oktoba 20 mwaka jana ambapo hadi unamalizika ugenini hakupata nafasi ya kucheza.

“Tulifungwa mabao 2-1, mchezo wa pili pia sikupata nafasi ya kucheza safari hiyo tulishinda kwa mabao 2-1, mchezo wa tatu nao sikupata nafasi, lakini nashukuru Mungu Novemba, 10 tukiwa nyumbani nilicheza kwa dakika 17 tu.

“Dakika zile zilitosha kocha kunikubali kwa sababu nilichokuwa nakifanya ni kuhakikisha natoa sapoti kwa mabeki wa kati pia nilikuwa nikiachia mipira kwa haraka, penye ulazima wa kukaa nao nilifanya hivyo na kupiga mashuti mawili,” anasema

“Jamaa kwa kazi niliyoifanya siku ile walianza kuniita Ngolo Kante, nadhani ni kwa sababu ya kuwa rangi yangu ni nyeusi na ni mchezaji ambaye nacheza nafasi anayoicheza Mfaransa huyo na ninatamani kufikia mafanikio yake,” anasema.

Ng’anzi anasema waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na anadai kuwa alijisikia furaha na baada ya mchezo huo, yakafuata mapumziko marefu ambayo yanamalizika mwishoni mwa mwezi huu yaliyomfanya arejee nchini ili kusheherekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

GIZA LAMSHANGAZA

“Kilichonishangaza Jamhuri ya Czech ni giza kuingia jioni, sikuamini yani kule saa moja ni muda wa kulala kwa sababu mida ya saa 10 tu giza unakuta limeingia,” anasema Ng’anzi anayekumbusha mkasa uliowahi kumpata Supamaketi.

Anasema kama ingekuwa Supamaketi ya Bongo, wala isingekuwa ishu, ila ughaibuni ilibaki kidogo tu aumbuke hasa kama asingekuwa na fedha za kuokoa jahazi.

Anasema kwa Bongo kilichompata ingekuwa simpo tu, angerudisha baadhi ya vitu ili kuendana na kiwango cha fedha alichobeba kufanyia manunuzi yake binafsi.

“Kilichotokea siwezi kusahau aisee, maana nilienda mwenyewe siku hiyo kufanya manunuzi, wakati huo bado sijazijua vizuri hela zao kutumia, nilibeba kiasi ambacho nilihisi kinatosha.

“Siku huyo mtu ambaye amekuwa kama msaidizi wangu alikataa na kusema leo nimechoka nenda mwenye sasa nilifika na kuchukua nachotaka ile naenda kulipia, hela kumbe haitoshi na kwa wenzetu huruhusiwi kurudisha vitu ulivyovichukua.”

“Niliomba nikachukue kiasi kilichopelea nyumbani nilikimbia fasta na kurudi haraka na kisha nikamalizana nao tangu siku hiyo nimekuwa mzito kwenda mwenyewe kwenye manunuzi,” anasema Ng’anzi.

RATIBA YAKE KWA SIKU

“Kibaya ni kwamba kila mtu baada ya mazoezi yuko na mambo yake, hivyo sina kampani kama nyumbani ambapo nilikuwa napata muda wa kutembea na marafiki zangu.

“Nachofanya baada ya mazoezi ni kurudi napokaa kupumzika na baadae naelekea gym kwa ajili ya kujiweka fiti, mazoezi tumekuwa tukifanya mara nyingi nyakati za asubuhi,” anasema.

KILUGHA CHAMCHANGANYA

Mbali na Kiingereza ambacho kimekuwa kikitumika kwa mataifa mengi ya Ulaya, Ng’anzi anasema hakuna kitu kinachomuumiza kichwa kama kilugha ambacho kimekuwa kikitumika nchini humo ambacho ni Kislovak.

“Aisee! Ni chenga tu, nikisikia ambao naongozana nao wanaanza kukizungumza nachofanya natoa simu yangu ya mkononi na kuweka phone masikioni kisha nasikiliza muziki mzuri wa nyumbani Tanzania,” anasema.

TRENI ZAMPAGAWISHA

“Wameendelea wenzetu treni zao utadhani ndege, Jamhuri ya Czech usafiri wao mkubwa ni treni kutoka mji mmoja kwenda mwingine, ni masaa machache unaweza kutumia kwenye safari ya umbali mrefu,” anasema.

Kuhusu vyakula Ng’anzi anasema licha ya kukumbuka vyakula vya nyumbani Tanzania ambavyo ndivyo vilivyomlea hadi anatimiza miaka 18, bado vyakula vya Jamhuri ya Czech havimsumbui kabisa.

“Zile safari za hapa na pale nikiwa na timu ya taifa ilinisaidia sana maana kuna aina ya vyakula ni vya kimataifa ambavyo ukienda kwenye mataifa yalitoendelea unakutana navyo.”

Ng’anzi alizitaja aina ya vyakula kwa lugha ya kigeni ambavyo ni maarufu nchini humo, Side dishes, Soups, Meat dishes, Snacks, Sweets, Breads na pastries.

AWAKATAA WAREMBO KIAINA

Ng’anzi anasema amekuwa akikutana na mademu wakali wa kizungu, lakini hana mapango nao kutokana na kutambua kuwa ili atimize ndoto zake anatakiwa ajitunze.

“Nikijiingiza huko nadhani utakuwa mwisho wa safari yangu ya soka, nafasi ninayocheza ya kiungo wa chini ni ngumu muda wote wa mchezo inanihitaji nisafe ili kuhakikisha tunakuwa imara,” anasema.

AITAKA MONACO

Ndoto za Ng’anzi ni kucheza soka la kulipwa Ufaransa na moja ya klabu ambayo anaihusudu ni AS Monaco ambayo anaichezea kiungo wa Kihispania, Cesc Fabrigas.

“Wakala wangu alicheza soka Ufaransa, aliniambia ana ukaribu na timu nyingi za nchini humo, amekuwa akiniambia kuwa hakuna kinachoshindikana kikubwa ni kuweka juhudi.”

ANACHOVIMBIA WAKALA WAKE

Miongoni mwa vitu ambayo wakala wa Ng’anzi, Morfwa anavyovimbia kichwa mbali na kuwasaidia vijana kibao wa Afrika Magharibi, lakini ni pamoja na kumsimamia kiungo Moussa Sissoko wa Tottenham Hotspur ya England.

AWASTUA VIJANA WENZAKE

Katika mahojiano yetu na Ng’anzi alimalizia kwa kuwataka vijana wenzake kutokata tama, waamini kuwa ipo siku ambayo jina anaijua mungu watatimiza ndoto zao za kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Adui namba moja wa mafanikio ni kukata tama, ikiwa wewe mwenye ndiye unayejikatisha tama basi tambua mchawi namba moja wa wewe kushinda kupiga hatua ni wewe mwenyewe.

“Muogope kama ukoma mtu anayekukatisha tama, kikubwa ni kuamini kuwa ipo siku, utatoboa,” anasema Ng’anzi kisha na kutudokezea kuwa yuko mbioni kuelekea Marekani.

Akicheka kiungo huyo wa zamani wa Singida United na kusema yajayo yanafurahisha na kumalizia timu hiyo nimeshamalizana nayo ila kuna vitu vidogo vimesalia ila inashiriki Ligi Kuu Marekani ambayo ni maarufu kama MLS.

Wito wake kwa wachezaji wenzake ni kujituma, kuwa na nidhamu sambamba na kupenda kujifunza kwa wengine waliofanikiwa, kama ambavyo amekuwa kijifunza kupitia kina Samatta na wakali wengine wanaotamba nje ya nchi kwa sasa.