Huyu Van Dijk mwacheni Klopp aweweseke

VIRGIL van Dijk. Wenyewe wanamwita VVD. Huyu ndiye, ni yeye akiwa moja ya sababu nyingi za Liverpool kumaliza ukame wao wa miaka 30 wa kubeba taji la ubingwa wa ligi. Huduma yake maridhawa.

Ni huduma yake bora iliyowafanya Liverpool kubeba Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana. Kila kitu kilianzia kwake kwa mafanikio ya Liverpool kwa miaka ya karibuni.

Saini yake ilikuwa ya pesa nyingi, lakini imeleta faida. Msimu huu, Jurgen Klopp alikuwa na matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wa ligi.

Kwa bahati mbaya, ndoto hizo zitahitaji kupambana sana kuweza kutimia. Van Dijk hatakuwapo uwanjani kwa miezi mingi baada ya kuumia goti na atahitaji upasuaji. Ni mchezo, lakini bila ya shaka Kop watakuwa na hasira na Jordan Pickford.

Rafu yake imemfanya Van Dijk kwenye hatari ya kukosa msimu wote wa 2020-21. Hili ni pigo, halina mjadala.

Van Dijk amekuwa mhimili wa Liverpool tangu alipotua Anfield, Januari 2018.

Kukosekana kwake ni pengo kubwa kwenye beki ya Klopp. Sasa atabaki na huduma za mabeki Joe Gomez na Joel Matip, ambao kimsingi hawajawahi kuanzishwa pamoja.

Shughuli ni pevu. Klopp lazima kichwa kimpasuke. Hakuna namna, Klopp atalazimika kutumia huduma za makinda, Sepp van den Berg, Rhys Williams na Nathaniel Phillips ambao ni mabeki kiasili, zaidi ya hapo, basi ni kiraka Fabinho. Shida ni kwamba hakuna beki kiongozi kwenye orodha hiyo.

Soka ni mchezo wa namba. Tangu alipotia mguu wake Anfield, Van Dijk amecheza mechi 130. Hakucheza mechi 13 tu. Hilo peke yake linaonyesha umuhimu wa mchezaji huyo kwenye beki ya Liverpool.

Namba hizo hizo, zinaonyesha kwamba kwenye mechi 130, Liverpool imeshinda mara 91 ikiwa na huduma ya Van Dijk uwanjani sawa na asilimia 70. Imetoka sare mara 20 na kupoteza mara 19 tu. Imefunga mabao 287 na kufungwa 124. Zile mechi 13, ambazo Van Dijk kajacheza, Liverpool imeshinda sita pekee, sawa na asilimia 46. Imetoka sare nne na kuchapwa mara tatu, huku ikiwa imefunga mabao 22 na kufungwa 20.

Hii ina maana kwamba ikiwa na huduma ya Van Dijk uwanjani, Liverpool ina chanya 163 ya mabao. Kwenye mechi ambazo hakucheza, wana chanya 2 tu ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwenye idadi hiyo ya mechi 130 ambazo Van Dijk alikuwa uwanjani, Liverpool haikuruhusu bao kwenye mechi 43. Hii ni huduma bora kabisa ambayo Liverpool wataikosa kwa miezi kadhaa na bila ya shaka hakuna mbadala wake huko Anfield.

Ukimwondoa Van Dijk, ukuta wa Liverpool unakuwa wa kawaida sana na hakuna ubishi kwamba miamba hiyo ya Anfield haitakuwa kwenye uimara wao kwa kukosa huduma ya Mdachi huyo kwenye safu yao ya ulinzi.

Pengine hii inaweza kuwa sababu moja kati ya nyingi itakayosababisha Liverpool kufeli kwenye michuano mingi kwa msimu huu.