Huyu Partey, ubingwa unakuja Arsenal

Saturday October 17 2020

 

LONDON, ENGLAND. ALIYEKUWA mkuu wa kitengo cha kusaka vipaji wa klabu ya Arsenal, Francis Cagigao anaamini kuwasili kwa kiungo Thomas Partey kwenye klabu hiyo ya Emirates kutawafanya kuwa tofauti na kuanza kuwa siriazi kwenye kushindania mataji.

Kocha Mikel Arteta alimfukuzia kiungo huyo mkabaji kwa kipindi chote cha dirisha la majira ya kiangazi na kufanikiwa kunasa saini yake kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo wakati alipokubali kulipa Pauni 45 milioni kuvunja mkataba wake huko Atletico Madrid. Staa huyo wa Ghana anatua Emirates akiwa kwenye hadhi kubwa kutokana na kile alichokuwa akikifanya Wanda Metropolitano.

Na Cagigao, ambaye alifichua kipaji cha staa wa zamani wa miamba hiyo, Cesc Fabregas kabla ya kuachana na kazi hiyo ya kutafuta vipaji vipya vya Arsenal, aliyofanya kwa miaka 24, sasa anaamini Arsenal wamepata mtu wa kuwapatia mataji.

“Ni mchezaji tuliyemfukuzia kwa muda mrefu na niliwasilisha jina lake miaka michache iliyopita,” alisema Cagigao.

“Mara ya kwanza nilimwona miaka sita iliyopita akiichezea Almeria kwa mkopo kutoka Atletico Madrid na alikuwa kiungo wa boksi kwa boksi, akishambulia pia.

“Nadhani tutamwona akisumbua sana kwa sababu alikuwa mtu muhimu kwenye kiungo ya Atletico. Atakuwa kitu muhimu kabisa kwenye kikosi cha Arsenal kitakachowafanya waanze kushindania mataji.”

Advertisement

Arteta, 38, hakuweka wazi kama atamchezesha Partey dhidi ya Manchester City leo Jumamosi.

 

Advertisement