Huwezi kuamini hawa wanausikia ubingwa wa ligi kuu redioni

Thursday May 16 2019

 

LONDON,ENGLAND.NDOTO ya juu kabisa ya kila mwanasoka duniani ni kubeba ubingwa hasa ule wa ligi kutoka kwenye nchi anayochezea.

Liverpool inapambana na hali yao kwa miaka 29 sasa kusaka taji lao la kwanza la Ligi Kuu England. Jambo hilo limewashuhudia nyota wake kibao wakiondoka kwenda kusaka ubingwa kitu ambacho kimetokea pia huko Arsenal ilipopoteza nyota wake wengi kisa tu mataji hakuna.

Lakini, kuna orodha ya wanasoka mahiri kabisa waliocheza soka kwenye ubora wao na kwenda timu kubwa, lakini hadi sasa bado hawajabatika kubeba ubingwa wa taji la Ligi Kuu.

1. Marek Hamsik

Umri: Miaka 31

Mechi za ligi: 482

Kiungo fundi wa mpira aliwashuhudia wenzake kama Ezequiel Lavezzi, Edinson Cavani na Gonzalo Higuain wakiondoka Napoli kwenda kubeba mataji huko kwingineko. Lakini, staa huyo amebaki Napoli na sasa umri umekwenda bila ya kubeba ubingwa wa ligi licha ya kucheza mechi 482. Hivi karibuni alijiunga na Dalian Yifang ya China pengine itampa ubingwa.

2. Antoine Griezmann

Umri: Miaka 28

Mechi za ligi: 356

Staa mkubwa kabisa huko kwenye La Liga, Antoine Griezmann ni moja ya wachezaji ambao hadi sasa wanasotea kubeba ubingwa wa ligi licha ya kucheza mechi 356.

Staa huyo wa Atletico Madrid umri wake unakwenda na wakati Atletico inashinda La Liga yeye hakuwapo kwenye timu hiyo. Pengine msimu ujao atatimiza hilo akihamia Barcelona.

3. Marco Reus

Umri: Miaka 29

Mechi za ligi: 305

Baada ya kushindwa kupata nafasi Reus aliondoka Borussia Dortmund na kurudi tena hapo mwaka 2012 akitokea Monchengladbach. Kipindi ambacho anarudi hapo, Dortmund walitoka kuchukua mara mbili mfululizo Bundesliga na baada ya hapo, Bayern Munich wakaanza kutawala. Reus amecheza mechi 305 za ligi bila kubeba taji huku umri ukienda kasi.

4. Pierre-Emerick Aubameyang

Umri: Miaka 29

Mechi za ligi: 346

Straika, Pierre-Emerick Aubameyang alitumikia misimu yake minne kwenye soka la kulipwa akiichezea AC Milan kabla ya kwenda Saint-Etienne kisha Borussia Dortmund na sasa Arsenal. Lakini, kote huko, straika huyo matata kabisa ambaye si muda mrefu atafikisha miaka 30 hajabeba ubingwa wa ligi, licha ya kucheza mechi 346 kwenye michuano hiyo.

5. Laurent Koscielny

Umri: Miaka 33

Mechi za ligi: 394

Moja ya mabeki mahiri kwenye soka ni Laurent Koscielny, ambaye amekuwa akitamba na Arsenal kwa sasa. Beki huyo Mfaransa aliwahi kuichezea pia Guingamp, Tours na Lorient huku akiwa amecheza mechi 394 za ligi.

Umahiri wake wote wa uwanjani, Koscielny anausikia tu ubingwa wa ligi kwenye bomba huku umri wake ukizidi kumtupa mkono.

6. Daniele de Rossi

Umri: Miaka 35

Mechi za ligi: 457

Kiungo wa shoka, Daniele De Rossi, amekuwa mtumishi wa muda mrefu kwenye kikosi cha AS Roma, akicheza mechi 457 za ligi kwa misimu yake 18 katika timu hiyo, lakini hata siku moja hajawahi kuonja utamu wa ubingwa wa ligi.

De Rossi atastaafu mwisho wa msimu huu na ameishia kuwa wa pili kwenye Serie A mara nane huku akishinda Kombe la Dunia.

7. Fernando Torres

Umri: Miaka 35

Mechi za ligi: 568

Fernando Torres kuondoka kwenye orodha ya wachezaji mahiri walioshindwa kubeba ubingwa wa ligi. Torres, anayekipiga Sagan Tosu amebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya na penalti, lakini atazeeka bila ya kubeba ubingwa wa ligi.

8. Dimitri Payet

Umri: Miaka 32

Mechi za ligi: 459

Dimitri Payet ni bonge la mchezaji. Huduma yake ndani ya uwanja hakuna asiyeifahamu, akipita kwenye timu nyingi na kubwa kama vile Lille, Marseille, West Ham, Nantes, Saint-Etienne na AS Excelsior. Lakini, kwa uhodari wake wote, Payet ataelekea kuzeeka bila ya kushinda ubingwa wa ligi licha ya kucheza mechi 459 katika michuano hiyo kwenye timu zote.

9. Hugo Lloris

Umri: Miaka 32

Mechi za ligi: 465

Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, kipa Hugo Lloris ni moja ya wachezaji wenye hadhi kubwa sana katika mchezo wa soka. Kwa uhodari wake wote wa uwanjani, Lloris ameshindwa kubeba ubingwa wa ligi licha ya kucheza kwenye timu za maana kama Nice, Lyon na Tottenham. Ameshacheza mechi 465 za ligi, lakini bado hajaonja utamu wa ubingwa.

10. Juan Mata

Umri: Miaka 31

Mechi za ligi: 411

Staa wa Kihispaniola, Juan Mata alianzia kwenye akademia ya Real Madrid, akashindwa kupata nafasi akatimkia Valencia alikocheza kwa mafanikio na kunaswa na Chelsea kabla ya sasa kukipiga Manchester United.Mata ni staa mkubwa sana kwenye soka akicheza mechi 411 za Ligi Kuu, lakini suala la kuonja utamu wa ubingwa wa taji hilo hajawahi kuuonja.

Advertisement