Huko Mashinani hawakubaki salama

Muktasari:

Talanta nyingi zimekuwa zikiibuliwa Mashinani ambako wanamichezo wengi wamnekuwa wakishiriki kwenye ligi mbalimbali.

 JANGA la virusi vya corona vyenye kuleta ugonjwa wa Covid-19, litasalia kuwa kumbukumbu isiyofutika kwa kizazi cha sasa na baadaye kutokana na athari zake zilizotikisa ulimwengu wote hasa michezo.

Kando na kusababisha maafa  makubwa kwa mamilioni ya watu, ugonjwa huo uliathiri shughuli mbalimbali ikiwemo michezo baada ya mataifa mengi kulazimika kupiga marufuku mikusanyiko ya umma kama hatua ya kuzuia msambao wa virusi hivyo.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo michezo iliathirika pakubwa sio tu katika ngazi ya kitaifa bali pia katika maeneo ya mashinani ambako michezo iliyokuwa ikiendelea ilisitishwa ghafla kutokana na agizo la serikali.

Katika eneo la Likoni michuano ya Kitaka Foundation Peace Cup iliyokuwa imefikia hatua za mduara wa timu 16 ilipigwa breki ghafla Machi 15 wakati wa mechi baina ya Zaragoza FC dhidi ya Peru.

Mashabiki waliokuwa wamefurika katika uga wa Black Pool ili kujionea mpambano huo, hawakuwa na budi ila kurudi makwao baada ya maafisa wa polisi kuwafurusha kutoka uwanja huo.

Maafisa hao walikuwa wakitekeleza amri iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta ya kupiga marufuku mikusanyiko ya umma kama hatua ya kuzuia msambao wa virusi vya corona baada ya kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha maambukizi.

Hadi kufikia sasa michuano hiyo bado imeendelea kusitishwa ikisubiri serikali kuondoa lockdown ya michezo kukiwa na jumla ya mechi tatu za kukamilisha raundi ya timu 16.

Kando na mechi baina ya Peru na Zaragoza, lockdown ilisitisha mechi ya Napoli FC na Sharks FC pamoja na Kenya Navy dhidi ya Gazab, ambapo Kocha wa Peru FC Saidi Bweta, anasema vijana wake walikuwa wamejiandaa vilivyo kushinda mechi hiyo.

Shughuli za Shirikisho la Soka, FKF tawi dogo la Kaunti ya Mombasa ziliathirika pakubwa na Lockdown ya michezo na kupelekea ofisi za tawi hilo kufungwa baada ya viongozi wake kushindwa kulipia kodi.

Mwenyekiti wa tawi hilo Juma Goshi Alliy anasema tawi hilo hutegemea zaidi pesa zinazolipwa na klabu kama ada ya kushiriki na kwamba, baada ya kusitishwa kwa michezo hawakuwa na njia mbadala ya kulipia kodi ya ofisi.

Katika kipindi fulani, Goshi  aliiomba serikali kuwakumbuka na pesa ilizokuwa imeahidi kuwapatia wachezaji kama ruzuku ya kupambana na janga la covid-19, ili waweze kulipia ofisi hizo japo kwa miezi mitatu.

Kando na kushindwa kulipia ofisi, mechi za Ligi zinazoendeshwa na tawi hilo hazikuweza kuendelea tena hadi kufikia.Kati ya Ligi zilizokuwa na ushindani mkali ni pamoja na Mombasa Premier, Mombasa Veterans, Ligi ya Daraja la Kwanza na Daraja la Pili ambazo zilikuwa na idadi ya timu 18 kila moja.

Katika Kaunti ya Kwale, janga la covid-19 lilipelekea kusitishwa kwa kalenda ya kila mwaka ya mashindano ya Kaunti ambayo huanzia ngazi ya wadi hadi Kaunti ambayo hutumika kufanyia uteuzi kikosi cha timu ya Kaunti hiyo.

Katika mahojiano ya hapo awali, Waziri wa Michezo wa Kaunti hiyo Ramadhan Bungale aliliambia Mwanaspoti kwamba, kutokana na kuwepo kwa janga hilo serikali ya Kaunti hiyo haingeweza kuendelea na ratiba yake ya kila mwaka ya mashindano hayo.

Alisema serikali ya Kaunti hiyo ilikuwa imeelekeza juhudi zake katika kukabiliana na janga hilo ili kuhakikisha visa vya maambukizi vinadhibitiwa vilivyo.

Alisema shughuli za michezo katika Kaunti hiyo zitaweza kuendelea tena baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa mwelekeo lakini wakati huo huo akiwahimiza wachezaji kujihusisha na mazoezi ya binafsi huku wakifuata maagizo ya wataalamu wa afya.

“Tumefunga michezo lakini nawahimiza wachezaji kufanya mazoezi ya kibinafsi huku wakizingatia masharti ya afya ili kuepuka maambukizi ya corona,’’ akasema.

Janga hilo pia lilipelekea kugeuzwa kwa uwanja wa michezo wa Ukunda Show Ground ambao kwa kawaida utumiwa na Klabu ya SS Assad kama uga wao wa nyumbani katika mechi zake za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza na kuwa soko la kuuzia bidhaa kwa wafanyabiashara.

Serikali la Kaunti hiyo ililazimika kuwapeleka wafanyabiashara katika uga huo kama hatua ya kuzuia mgusano baina ya wanabiashara hao na wanunuzi bidhaa kama njia ya kuzuia maambukizi. Hata hivyo, taratibu serikali imeanza harakati za kuruhusu maisha kuendelea kama zamani japo kwa tahadhari kubwa hivyo, ruhusu rasmi ikitolewa wanamichezo wataanza kukiwasha upyaaa.