Huko Kirumba ni rekodi, visasi tu

Sunday January 19 2020

 Mbao VS Simba-Alliance- kocha Sven Vanderbroek -Uwanja  CCM Kirumba-Kocha wa Alliance-, Fredy Felix ‘Minziro-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-’

Mashabiki wa Simba wakishangilia baada ya timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao, katika mchezo uliopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza. Simba wanashuka tena dimbani leo Jumapili kuwakabili Alliance FC. PICHA | SADDAM SADICK 

By Saddam Sadick,Mwanza

BAADA ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Mbao, Simba inashuka tena uwanjani leo kuwakabili Alliance, huku kazi kubwa ikiwa kwa kocha wake, Sven Vanderbroek kuendeleza rekodi ya ushindi kwa wapinzani hao.

Mchezo baina ya timu hizo unatarajia kupigwa dimba la CCM Kirumba jijini hapa na rekodi zinaibeba Simba kwani tangu Alliance ipande daraja msimu uliopita haijawahi kupata hata sare tofauti na vipigo tu.

Mechi ya mwisho kukutana timu hizo kwenye uwanja huo jijini hapa, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku mchezo wa awali uliopigwa dimba la Taifa Dar es Salaam Alliance ililala mabao 5-1.

Mpambano wa leo unatazamwa kuwa mgumu kwani Alliance watakuwa wakipambana kuvunja uteja na kulipa kisasi, huku Wekundu wakihitaji kuendeleza rekodi hasa kwa kocha wao Vanderbroek.

Hadi sasa Simba inaongoza ligi kwa pointi 38 baada ya mechi 15, huku Alliance wakiwa na alama 20 katika nafasi ya 12 baada ya kushuka uwanjani mara 16.

Kocha wa Alliance, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu apewe majukumu kuiongoza timu hiyo, anahitaji ushindi ili kuanza vyema kibarua chake. Alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji ushindi, hivyo wanashuka uwanjani kwa lengo la kupambana kuvunja mwiko kwa vigogo hao wa Ligi Kuu.

Advertisement

“Ni kweli Alliance haijawahi kushinda mbele ya Simba, lakini kila kitu na muda wake, kikubwa tuombe uzima mengine tutazungumza baada ya dakika 90,” alisema Minziro.

Kwa upande wake, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kurejea kwa kinara wao wa mabao, Meddie Kagere kunaongeza nguvu kikosini katika vita ya kusaka ushindi.

“Hadi sasa timu iko vizuri na matarajio yetu ni kushinda mechi hiyo na tayari Kagere amerejea baada ya kumaliza adhabu yake ya kadi tatu za njano, hata Dilunga yuko fiti,” alisema Meneja huyo.

Advertisement