Huko Ihefu mzuka umepanda

STRAIKA wa Ihefu FC, Enock Jiah amesema ushindi walioupata juzi dhidi ya Ruvu Shooting, umewafuta machozi kufuatia kupoteza mechi ya ufunguzi dhidi ya Simba na kwamba, kwa sasa morari imerudi kikosini.

Timu hiyo mpya katika Ligi Kuu, ilianza vibaya msimu kwa kupoteza mabao 2-1 dhidi ya Simba, ambapo juzi ikiwa tena nyumbani iliwalaza Ruvu Shooting bao 1-0.

Ihefu inayonolewa na Kocha Makka Mwalwisi ilipanda daraja kupitia hatua ya mchujo kwa kuiondoa Mbao FC kwa faida ya mabao mawili ya ugenini baada ya kufungwa 4-2 katika mechi ya mwisho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Jiah ambaye ndiye aliipatia bao la ushindi timu yake, alisema ushindi huo umerejesha upya nguvu na morari kikosini kuweza kuendelea kusaka alama tatu.

Alisema kwa sasa hesabu zao ni kukusanya pointi sita katika uwanja wao wa nyumbani kabla ya kuondoka mikoa ya Kanda ya Ziwa licha ya kwamba malengo hayajatimia vizuri.

“Tulikuwa na mkakati wa kushinda mechi zote za nyumbani lakini Simba walitutibulia, kwa hiyo tunajiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ili tushinde tufikishe alama sita tuelekee Kanda ya Ziwa,” alisema Kinda huyo.

Nyota huyo wa zamani wa Mwadui FC, aliongeza kuwa kutokana na muunganiko ulioanza kutengenezwa kikosini anaamini Ihefu itafanya vizuri licha ya kuwa huu ni msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu.

“Lakini pia nafurahia kuona naanza kutupia mabao, natamani mwisho wa msimu kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya mfungaji bora, najiamini wala sina presha.”