Hoteli ya Stars Misri ni kiboko

Tuesday June 11 2019

 

By Charles Abel


STARS inaendelea na kambi ya maandalizi yake huko Cairo, Misri kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zitachezwa nchini humo kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 ikijichimbia kwenye Hoteli ya kifahari ya Renaissance Cairo Mirage City.

Hoteli hiyo ambayo ipo katika Kitongoji cha Heliopolis jijini Cairo, ina huduma zote stahiki kwa wachezaji ikiwemo vyumba vya hadhi ya juu, kumbi za chakula, mabwawa ya kisasa ya kuogelea, eneo la kuchezea gofu, kumbi za mazoezi pamoja na sauna.

Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini Shirikisho la Soka nchini (TFF) linatumia kiasi kikubwa cha fedha kugharimia kambi kwenye hoteli hiyo ambayo watakaa hadi Juni 20 na watapangiwa hoteli nyingine ya kukaa ambayo hawatolipia gharama zake.

Kiasi cha zaidi ya Sh128 milioni kitatumika kugharimia huduma ya malazi tu kwenye hoteli hiyo ambayo wastani wa chumba kimoja ni Dola 180 (Sh413,600)

Stars imeenda na msafara wa takribani watu 40 hivyo idadi ndogo ya vyumba ambayo itavitumia ni 25 jambo linaloifanya kwa siku itumie Dola 4675 (Sh10.7 Milioni)

Kwa jumla katika siku 12, gharama ya malazi itakuwa ni Dola 56,100 (Sh129 milioni) ambacho hakihusishi fedha inayotumika kugharimia huduma ya chakula na kukodi uwanja wa mazoezi inaoutumia kwenye maandalizi hayo.

Advertisement

“Hali ya kambi ni nzuri na timu ipo kwenye hoteli nzuri ambayo ina miundombinu yote ambayo inawafanya wachezaji wawe na maandalizi mazuri kwa hiyo kwa jumla kambi iko vizuri,” alisema meneja wa Stars, Danny Msangi.

Advertisement