Hongera Simba, mlistahili taji la 2018-19

Muktasari:

  • Ni matokeo ya kuwa na kikosi bora zaidi kinachoundwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa, na takwimu zote zinathibitisha.

SIMBA ndiyo mabingwa wapya 2018-19 wakitetea kimafanikio taji lao walilolitwaa msimu uliopita.

Kwa mara ya pili mfululizo, Simba wanalibeba taji hilo wakiwa mkoani Singida, wakiwa wamebakisha mechi mbili ili kumaliza msimu huu.

Ni taji la 20 la Ligi Kuu ya Bara kwa Wekundu wa Msimbazi wakizidi kupunguza pengo lililokuwapo dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa taji hilo Yanga waliolibeba mara 27.

Mbio za nyika, mabonde na milima katika kuwania taji hilo zimefikia tamati baada ya Wekundu wa Msimbazi kuthibitisha kwamba wao ndiyo wafalme wa soka la Bongo kwa msimu wa pili mfululizo.

Ufalme wa Simba msimu huu umepatikana baada ya miamba hao kupoteza mechi tatu tu za ligi – mbili dhidi ya Kagera Sugar na moja dhidi ya Mbao FC ya Mwanza. Ni ufalme wanaoustahili kwani Simba ilikuwa ikitawala takriban kila mechi iliyocheza, hata ilizopoteza.

Ilikuwa ni nadra sana kuona Simba ikipelekwa puta uwanjani, lakini ilikuwa ni yenyewe iliyokuwa ikiwafanya wapinzani wausake mpira kwa tochi.

Kuwafanya wapinzani kuusaka mpira kwa tochi msimu mzima hakukuja hivi hivi.

Ni matokeo ya kuwa na kikosi bora zaidi kinachoundwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa, na takwimu zote zinathibitisha.

Pacha watatu wa safu yao ya ushambuliaji ndiyo wanaotisha zaidi nchini wakifunga jumla ya mabao 54, yaani mawili tu pungufu ya yale ambayo wamefunga wachezaji wa timu nzima ya Yanga, ambayo ndiyo ilikuwa ikishindana nao katika mbio za ubingwa. Straika wao Meddie Kagere ndiye kinara wa mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora akiwa na magoli 23.

Pacha wake katika ushambuliaji, John Bocco amefunga mabao 16 na Emmanuel Okwi ametupia mabao 15 katika Ligi Kuu msimu huu.

Safu ya kiungo iliyojaa ‘mafundi’ Clatous Chama, Haruna Niyonzima, James Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na wengine ndiyo iliyotawala ikiwatia njaa wapinzani msimu mzima.

Wakali hao chini ya makamanda wa ulinzi, Serge Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walikuwa na kila sababu ya kumaliza msimu wakiwa timu iliyofungwa magoli machache zaidi (14). Azam FC iliyo katika nafasi ya tatu ndiyo inayofuatia kwa kuruhusu mabao machache (21) na Yanga (26) hadi sasa.

Kipa wao Simba, Aishi Manula, ndiye ‘Tanzania One’ kwa sasa na anatarajiwa kutwaa tuzo ya Glovu za Dhahabu ya Kipa Bora wa Msimu.

Takwimu zinaongea. Simba ilikuwa kila kitu katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu.

Ndiyo maana haikuwa ajabu ilipopata mafanikio Afrika pale ilipochanja mbuga hadi robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa dhidi ya TP Mazembe ya DRC.

Kazi kubwa iliyofanywa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ni ya kupongezwa, huku pia uongozi chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed ‘Mo’ Dewji, ukistahili pongezi hizi pia kwa kukaa chini na kusuka kitu kikubwa, ambacho kimeifanyia makubwa nchi pia kwa kuitangaza na kuipandisha kwenye viwango vya ubora kutokana na mafanikio yao Afrika msimu huu.

Ni kwa juhudi zao ndiyo maana katika msimu wa 2020-21, Tanzania itawakilishwa na jumla ya timu nne katika michuano ya klabu Afrika -- Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Pongezi pia ziende kwa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, mtoto wa gwiji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara.

Anaweza kuwa anawanyima usingizi Yanga kwa maneno yake mengi dhidi yao, lakini Manara anafanya kazi kubwa ya uhamasishaji ambayo imechochea kwa namna moja ama nyingine mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi msimu huu. Mafanikio ya Simba msimu huu, yanathibitisha umuhimu wa kuwekeza katika soka na michezo kwa ujumla.

Baada ya Ligi Kuu ya Bara kukosa mdhamini msimu huu, maisha yalikuwa magumu kwa asilimia kubwa ya timu shiriki.

Jambo hilo lilipunguza ushindani. Ushahidi ni timu ya Coastal Union iliyolazimika kusafiri kwa basi umbali wa zaidi ya kilometa 332 siku ya mechi yao dhidi ya Simba na kuwasili saa chache kabla ya pambano kuanza kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, wakijaribu kukwepa gharama za malazi jijini hapa.

Kilichotokea kila mtu alikitarajia. Walikumbana na kipigo cha mbwakoko cha magoli 8-1 kutoka kwa Simba, kipigo ambacho kimeweka rekodi ya kichapo kikubwa zaidi msimu huu.

Kukosa pesa ya kulipia hoteli kwa Coastal Union siyo kosa la Simba. Na wala haiwahusu. Ndiyo maana wakawaadhibu bila huruma huku Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wakiondoka na mpira kila moja baada ya kila mmoja kutupia ‘hat-trick’ katika mechi hiyo.

Kwa uwekezaji huu, Simba wana nafasi kubwa ya kubaki Wafalme wa Soka la Bongo kwa misimu mingine mingi mbele, isipokuwa kama timu nyingine zitafuata nyayo.

Hongera Simba kwa uwezekezaji huu. Hongera Wekundu wa Msimbazi kwa kubeba ndoo ya 20 Ligi Kuu.