hehee! Chongeni tena sasa

Muktasari:

  • Heritier Makambo ambaye alikuwa hajafunga bao kwa siku 52, alikuwa wa kwanza kuonyesha nia ya Yanga kutoka na pointi zote tatu kwa mara ya kwanza dhidi ya Mbao baada ya kuisawazishia timu yake bao murua dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza.

MWANZA . KABLA ya mechi ya jana Mbao FC ilikuwa ikichonga sana, hasa baada ya kuchungulia rekodi zao za nyuma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa dhidi ya Yanga, lakini kilichowakuta mbele ya mashabiki wao kiliwafanya waishiwe pozi, huku wenzao wakiwaambia chongeni tena!

Ujumbe huo licha ya kuambiwa Mbao, lakini ni kama vile ulikuwa ukipelekwa kwa Simba ambao baada ya ushindi mfululizo katika mechi zao za viporo walikuwa wakitamba sana mitaani wakiamini bado kidogo tu wainase Yanga kileleni, lakini kwa ushindi huo inabidi wajipange.

Unajua nini? Mwaka 2017 katika nusu fainali ya Kombe la FA Yanga ilivuliwa taji na kulala 1-0, siku chache baada ya kubeba taji la Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo waliifuata tena Mbao wakalala 1-0. Mbao ikawa shangwe kama lote. Halafu msimu uliopita tu, Yanga ikiwa na mwendo wa kugawa dozi, waliinyoshwa tena 2-0 na wauza mbao hao wa Mwanza.

Kisha si msimu huu walienda Simba wakiwa moto kinoma, lakini wakapigwa bao 1-0, basi Mbao wakajua hata safari hii mambo yatakuwa mukide na Yanga lazima ingenyooshwa tena Kirumba.

Hata hivyo walichokutana nacho kwa Vijana wa Mwinyi Zahera, iliwanyamanzisha Mbao baada ya kuwanyoosha mabao 2-1 na kuvunja mwiko wa kufunga bao ama kupata pointi yoyote mbele ya wakali hao wa jijini hapa.

Ikicheza bila baadhi ya nyota wake akiwamo kiungo fundi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yanga ilidhihirisha kuwa msimu huu inalitaka taji la Ligi Kuu Bara baada ya kuikimbiza Mbao na kuipasua mbele ya mashabiki wao, huku mji wa Mwanza ukirindima kwa shangwe za Wanajangwani.

Heritier Makambo ambaye alikuwa hajafunga bao kwa siku 52, alikuwa wa kwanza kuonyesha nia ya Yanga kutoka na pointi zote tatu kwa mara ya kwanza dhidi ya Mbao baada ya kuisawazishia timu yake bao murua dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza.

Hilo likiwa bao la 12 kwa Mkongomani huyo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga msimu huu tangu asajiliwe kutoka kwao DR Congo.

Kabla hapo Ndaki Robert aliitanguliza Mbao kwa bao la sekunde chache kabla ya mapumziko kutokana na uzembe uliofanywa na kipa Ramadhani Kabwili katika kufanya mpira wa krosi uliopigwa na Amos Charles.

Wakati wa mapumziko waamuzi wa mchezo huo walishindwa kuingia vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kushambuliwa na chupa za maji na mashabiki waliokuwa na hasira wanaodhaniwa wa Yanga kutokana na kutoridhiwa na maamuzi yao, hata hivyo askari Polisi waliingilia kati na kuwasindikiza.

Ndipo dakika ya 50 Makambo aliandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kufunga bao dhidi ya Mbao kwenye Uwanja wa Kirumba, alipounganisha kwa kichwa krosi ya Papy Kabamba Tshishimbi kabla ya Amissi Tambwe kuongeza la pili na la ushindi kwa penalti.

Penalti hiyo ilitokana na mtokea benchi Babilsa Chitembe kuunawa mpira wa Kelvin Yopndani na Tambwe kukwamisha wavuni dakika ya 68 na kumfanya Mrundi huyo kufikisha bao lake la saba msimu huu na kuifanya Yanga kufikisha alama 61 baada ya mechi 25 na kuwaacha Azam waliopo nafasi ya pili kwa alama 11, huku watani zao Simba wakiwaacha kwa alama 19 licha ya kuwa na michezo saba mkononi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kabla ya mchezo huo alikaa na vijana wake na kuwauliza kina nani wanaamini leo wanaenda kuvunja mwiko? “Niliwaambia wanaoamini tunaenda kushinda waingie garini na wote wakaingia, na kipindi cha pili baada ya kufungwa niliwaambia wasichoke wapige krosi mfululizo na tutaondoka na ushindi.”

Zahera alisema bahati nzuri vijana wake walitekeleza na kufanikiwa kurudisha bao na kuongeza la ushindi. Naye Robert Ndaki aliyefunga bao la kufutia machozi la Mbao, alisema wamepoteza kwa kushindwa kutumia nafasi walizopata na wanakubali matokeo kwa vile asiyekubali kushindwa sio mshindani.