He! Ozil ndo hivyo watu hawamtaki

Thursday July 11 2019

 

LONDON, ENGLAND. Habari ndiyo hiyo. Arsenal wanalo hilo. Ni hivi, miamba ya soka ya Uturuki, Fenerbahce imefuta mpango wa kumsajili kiungo fundi wa Kijerumani, Mesut Ozil.

Arsenal wanataka kuachana na mchezaji huyo ili kupunguza bili ya mishahara yao klabuni kutokana na kumlipa mchezaji huyo Pauni 350,000 kwa wiki, lakini sasa mambo yanakuwa magumu hata kumtoa tu mchezaji huyo kwa dili la mkopo.

Awali ilifichuka kwamba wababe hao wamepanga kumchukua mchezaji huyo, lakini taarifa za Mirror Sport ni kwamba mpango huo haupo tena na kwamba wameshamnasa kiungo mwingine wa Kijerumani, Max Kruse kwa mkataba wa miaka mitatu na kuachana na Ozil, kwa sababu wanacheza nafasi moja uwanjani.

Ozil amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kwenye timu hiyo ya Uturuki baada ya hivi karibuni kuoa binti wa kutoka nchi hiyo, mrembo Amine Gulse, huku mwenyewe akiwa na asili ya Kituruki.

Taarifa ya Fenerbahce imeweka wazi kwamba hakuna mpango wowote wa kuinasa huduma ya mchezaji huyo na kwamba wanaheshimu ubora wa mchezaji huyo na vile alivyokuwa akiwawakilisha ng'ambo ya mipaka ya nchi yao, lakini mpango huo hauwezi kutokea kwa kipindi cha karibu.

Ozil mwenyewe hayupo tayari kuondoka Arsenal anataka kubaki kwenye timu hiyo hadi mwisho wa mkataba wake ambapo umebaki miaka miwili, lakini shida linakuja kwa kocha Unai Emery, ambaye mpango wake ni kumwondoa kwenye kikosi chake ili kupunguza bili ya mishahara.

Advertisement

Advertisement