He! Hebu msikie Klopp anachosema huko Liverpool

Muktasari:

Mjerumani huyo amekuwa akiheshimu mikataba yake katika klabu anayokwenda kufanya kazi, hivyo jambo hilo lina maana kwamba atabaki Anfield hadi mkataba wake utakapofika tamati kama ilivyotokea alipokuwa Mainz na Borussia Dortmund.

LIVERPOOL, ENGLAND. UTANI mwingine bana. Kocha Jurgen Klopp amedai huenda akaamua kuchukua uamuzi wa kustaafu ukocha wakati mkataba wake wa kuinoa Liverpool utakapofika mwisho 2022.

Kocha huyo wa Liverpool alikuwa Ujerumani mapema wiki hii kupokea tuzo bora ya ukocha iliyotolewa na moja ya gazeti maarufu kabisa huko kwao.

Klopp akiwa siriazi alisema hafahamu kitu gani atakifanya baada ya kipindi hiki cha miaka mitatu kupita na huenda akafikiria kustaafu kabisa.

Kocha huyo alisema anaweza kuchukua uamuzi wa kustaafu mapema zaidi kuliko makocha wengine na kudai kitu hicho kinagota sana kwenye mawazo yake.

Mjerumani huyo amekuwa akiheshimu mikataba yake katika klabu anayokwenda kufanya kazi, hivyo jambo hilo lina maana kwamba atabaki Anfield hadi mkataba wake utakapofika tamati kama ilivyotokea alipokuwa Mainz na Borussia Dortmund.

Klopp alipoulizwa nini kitafuata baada ya kuipa Liverpool ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, alisema: “Natumaini nitaendelea kufanya mambo mazuri, lakini katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ijayo, sifahamu nini kitatokea.

“Pengine nitastaafu! Si kwamba ni lazima litokee hilo, la lakini isiwe kesi litakapotokea, kwamba isiwe ni kitu cha ajabu.”

Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Klopp alihusishwa na mpango wa kwenda huko Juventus, huku Bayern Munich ikitajwa mara kadhaa kwamba huenda akafukuzia huduma yake akawe kocha kwenye kikosi chao.

Klopp anapambana kwa nguvu zote kuipa Liverpool ubingwa wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England.