Hazard, muda wowote kutangazwa Bernabeu

Friday June 7 2019

 

MADRID, HISPANIA . NI suala la kutazama saa yako na kuwa karibu na televisheni yako. Mambo yanakaribia kufika mwisho. Muda wowote kuanzia sasa Real Madrid itamtangaza Eden Hazard kama mchezaji wake na si mchezaji wa Chelsea tena.

Sakata la muda mrefu la Hazard kwenda Madrid linakaribia mwisho baada ya klabu zote mbili, Real Madrid na Chelsea kukubaliana ada ya uhamisho ya staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ambaye amekwishaonyesha nia yake ya kuondoka katika dirisha hili.

Kwa mujibu vya vyombo mbambali vya England jana Alhamisi, Hazard atauzwa kwa dau la Pauni 88.5 milioni huku pia kukiwa na ongezeko la pesa katika dau hilo kwa kadiri ambavyo atapata mafanikio akiwa na timu yake mpya Real Madrid.

Chelsea inalazimika kumuuza Hazard kutokana na kubakiza mkataba wa mwaka mmoja Stamford Bridge na endapo itamuwekea ngumu staa huyo, basi ataondoka bure mwishoni mwa msimu ujao baada ya kushindwa kusaini mkataba mpya zaidi ya mwaka 2020.

Hazard, 28, anatazamiwa kuondoka Stamford Bridge akiwa shujaa baada ya kufunga mabao mawili katika pambano la fainali za Ulaya dhidi ya Arsenal Jumamosi iiyopita na mara baada ya pambano hilo aliwaaga mashabiki akisisitiza kuondoka klabuni hapo.

“Nimeshachukua maamuzi yangu tayari, nilisema hilo wiki mbili zilizopita. Kwa sasa inategemea na klabu, klabu zote mbili. Na mimi nasubiri kama mashabiki, tutajua ndani ya siku chache zijazo,” alisema nyota huyo aliyenunuliwa kutoka Lille ya Ufaransa mwaka 2012.

Advertisement

“Nadhani ni kwaheri, lakini katika soka hauwezi kujua. Ndoto yangu ilikuwa ni kucheza katika Ligi Kuu ya England na nimefanya hivyo kwa miaka sana. Labda sasa ni wakati wa kusaka changamoto mpya,” aliongeza staa huyo.

Real Madrid imepania kumchukua Hazard ambaye anaonekana kuwa mbadala wa muda mrefu wa staa wake wa zamani, Cristiano Ronaldo ambaye aliuzwa kwenda Juventus kwa dau la Pauni 88 milioni katika dirisha kubwa la mwaka jana.

Tangu Ronaldo aondoke, Madrid imepwaya na msimu huu iliondoka bila ya kuambulia taji lolote huku ikivuliwa ubingwa wa Ulaya na Ajax baada ya kuchukua taji hilo kwa miaka mitatu mfululizo chini ya Ronaldo.

Tayari Madrid imefungua pochi lake kwa kuwanunua mastaa wawili wakianzia kwa beki wa kimataifa wa Brazil, Eder Militao waliyemnunua kwa dau la Pauni 44 milioni kutoka Porto ya Ureno mwanzoni mwa mwaka huu lakini staa huyo anatazamiwa kuanza kuvaa jezi msimu ujao.

Mwingine aliyenunuliwa ni mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Serbia, Luka Jovic aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 62 milioni kutoka Eintracht Frankfurt ambalo linamfanya kuwa mshambuliaji ghali katika historia ya Real Madrid.

Achilia mbali Hazard, Madrid inakaribia kumchukua beki wa kushoto wa Lyon na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Ferland Mendy na habari zimeenea staa huyo anakwenda kupimwa afya Madrid muda wowote kuanzia sasa baada ya klabu hizo kukubaliana dau la Euro 50 milioni.

Achilia mbali staa huyo, Madrid inaonekana kuwanyemelea mastaa wengine kama kiungo mahiri wa Manchester United, Paul Pogba huku pia ikihusishwa na staa wa PSG, Kylian Mbappe pamoja na kiungo mahiri wa Tottenham Hotspurs, Christian Eriksen ambaye amekiri anaweza kuondoka klabuni hapo katika dirisha hili.

Advertisement