MAJANGA: Haya ndio yaliyomkuta bondia Class Marekani

VIJANA wengi wanatamani kuishi Marekani, bila shaka simulizi za maisha ya kule na namna wanavyoona kwenye mitandao ya kijamii na kwenye runinga yanawapa mzuka wa kuishi huko hasa wale ambao, hawajawahi kufika huko.

Ndivyo ilikuwa kwa bondia Ibrahim Class, ambaye mwishoni mwa mwaka 2018, bingwa huyu wa dunia wa Global Boxing Council (GBC) alipata ofa ya kwenda kuishi Marekani ambako alikaa kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kurejea nchini.

Class anasema aliletewa mkataba mnono ambao, ulimshawishi kutoka Dar es Salaam kwenda kuanza maisha mapya.

“Tuliondoka nchini na Chaurembo Palasa, mwenyeji wetu kule alikuwa mtu mmoja raia wa huko aliitwa Napolio. Safari yetu ilikuwa nzuri na tulifuata taratibu zote za kuingia nchini humo.

“Napolio alitupokea vizuri tukawa tukiishi kwake mjini Washington DC, tulikaa kama mwezi mmoja, maisha yakaanza kubadilika,” anasimulia Class.

Ingawa hapa nchini ziliibuka taarifa kuwa, Class amekwenda Marekani kuwa bondia wa mazoezi (sparing patner) wa bei rahisi, wengine wakavumisha kuwa anafanya vibarua kwenye maduka makubwa.

Anasema mkataba wake ulikuwa wa kwenda kufanya mazoezi kule na kutafutiwa mapambano ambayo angepigana akitokea nchini humo na Napolio ndiyo angekuwa meneja wake.

“Kile ambacho kiliwekwa kwenye mkataba kikawa tofauti, tukiwa pale nyumbani kwa Napolio nikawa nawasiliana na rafiki yangu mmoja anaitwa God yupo Texas, tukamueleza changamoto tunazopitia akakubali twende kwake.”

Anasema yeye na Chaurembo walihamia kwa God ambako walikaa kama wiki mbili, mwenyeji wao akawatafutia gym ya kufanyia mazoezi, walifanikiwa akaanza mazoezi kule.

Anasema baadaye God aliwaunganisha kwa ndugu yao anaitwa Eddy kwa ajili ya kufanya mazoezi na kucheza mapambano, ambako walikaa mwezi mmoja kabla ya kupata pambano nchini Afrika Kusini.

“Tulikwenda Afrika Kusini na Palasa, baada ya lile pambano, Palasa alisema anarudi Tanzania, mimi nikarudi Marekani.

KUJITEGEMEA

Class anasema baada ya kurejea Marekani alizungumza na Eddy akamwambia anahitaji kujitegemea kwa kuwa mwenyeji wake alikuwa na familia na tayari alikuwa amewapa hifadhi ya muda mrefu.

“Nilipanga nyumba ambayo kwa mwezi nilikuwa nikilipa dola 1,300 (Sh2.9mil), ambayo ilijumuisha bili ya umeme na maji, nikaanza kujitegemea.”

Anasema akiwa nchini humo, mbali na ngumi lakini pia alitafuta kibarua akawa anafanya ambacho kilikuwa kikimuingizia fedha.

“Maisha Marekani yalikuwa ni gharama, ni kweli nilikuwa nikipata fedha, lakini gharama za maisha ziko juu sana nchini humo, nilikaa mwaka mmoja.

Anasema akiwa Marekani alipata pambano mjini Califonia ambako ni mitaa ya Floyd Mayweather, hivyo alikwenda kupiga kambi mjini humo.

YEYE NA PACQUIAO

Akiwa Califonia, alijifua kwenye gym ya kocha wa Manny Pacquiao, ambaye alimsaidia katika mazoezi kabla ya kupanda ulingoni kuzichapa kwenye pambano hilo ambalo alipoteza kwa Technical Knock Out (TKO).

“Nilijifua kwenye gym ya kocha Fred Rochie ambaye ni kocha wa Pacquiao hadi siku ya pambano, ingawa kocha wangu binafsi, ambaye nilitoka nao Texas nilikuwa nikimlipa,” anasema.
Anasema kutokana na juhudi ya mazoezi aliyokuwa akiionyesha kule Texas, kocha alimpa ofa ya kutumia gym bure na alikuwa akimlipa akijiandaa kucheza  pambano
“Mara ya mwisho kocha wangu nimemlipa dola 6,000 (Sh 13 milioni) kwenye pambano langu, Marekani maisha ni ghali kidogo, tofauti na huku kwetu, lakini pia michongo ya kupata pesa ipo,” anasema.
Class, ambaye pambano lake la ubingwa wa dunia lililopewa sapoti na serikali kabla ya kwenda Marekani, aliingiza Sh 18 milioni anasema kwa maisha ya Marekani ukiwa na kipaji, ngumi zinalipa.
“Kibongo bongo siwezi kumlipa kocha 13 milioni kwa pambano, lakini Marekani nililipa pesa hiyo tena kocha akinisaidia tu, kwani ilikuwa ni kwenye pambano na gharama za gym nilipewa ofa,” anasimulia.
Bondia huyo, ambaye anajiandaa kucheza ubingwa wa dunia nchini baada ya janga la corona kupita, anasema gharama za maisha nchini Marekani pia ziko juu.
Class, ambaye alianza ngumi mwaka 2010 anasema katika maisha yake ya ngumi hawezi kulisahau pambano lake la Mei Mosi, 2013 alipocheza na Amos Mwamakula.
“Mpinzani wangu alinitambia mno, si yeye tu, hadi mashabiki wake na hata wangu walijua nitapigwa, nilielezwa sifa zake kila siku tangu siku niliposaini kuzichapa naye hadi siku ya pambano,” anasimulia.
Class anasema sifa kubwa ya Mwamakula bondia kutoka Mbeya aliambiwa ni kuwa ana nguvu nyingi, hivyo ni bondia mwenye ngumi nzito na kamwe hatomuweza, ingawa alishinda pambano hilo ambalo lilimpa ujasiri hadi sasa.
Class, 29, anasema alianza kujifunza ngumi akiwa na miaka 10, wakati huo alipenda kuufuatilia mchezo huo.
“Siku moja nilimuomba Chaku Master (Said), anisaidie nijifunze, alinipeleka kwa Kinyogoli (Habibu) akaanza kunifundisha,” anasimulia.
Anasema kwa kuwa alipenda kujifunza, alifuata maelekezo yote ya kocha na Kinyogoli amekuwa msaada mkubwa katika safari yake hiyo.

UBINGWA WA DUNIA
Julai Mosi, 2017, Class alitwaa ubingwa wa dunia nchini Ujerumani, baada ya kumchapa Jose Ferero kwa pointi na kuutetea ubingwa huo miezi minne baadaye jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru alipomchapa Koos Sibiya wa Afrika Kusini.
Anasema alicheza pambano hilo akiwa kwenye kiwango bora, kabla ya kwenda Ujerumani alifanya mazoezi na mabondia tofauti tofauti nchini akiwamo Abdallah Pazi na Cosmas Cheka.
“Nilipokuwa nikitetea ubingwa wangu, bahati mbaya niliumia mguu, hakuna aliyekuwa akifahamu hili, nilicheza kwa tabu, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu alinisimamia hadi nikashinda nyumbani,” anasimulia
Bondia huyo ambaye ni wa pili nchini kwenye uzani wa super feather na wa 75 kati ya mabondia 1586 duniani anasema ngumi zimemsaidia mambo mengi kwenye maisha yake ikiwamo kujenga mjengo wake Kimara, jijini Dar es Salaam.
Tangu 2010 alipoingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa, Class amecheza mapambano 29, ameshinda 23 (11 kwa KO), amepigwa mara 6 (3 kwa KO).