Haya Mbappe ni Madrid tu

Wednesday September 16 2020

 

PARIS,UFARANSA. HABARI ndo hiyo. Kylian Mbappe anaripotiwa kuiambia klabu yake ya Paris Saint-Germain kwamba anachotaka ni kwenda kujiunga na Real Madrid kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwakani.

Mbappe huenda akaachana na PSG mwakani huku mkataba wake kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ufaransa ukifika tamati 2022. PSG inasubiri kupokea ofa za kutoka klabu mbalimbali za Ulaya kama watashindwa kumsainisha dili jipya na tayari kuna timu kibao zimeonyesha dhamira ya kumnasa. Fowadi huyo aliwahi kusifia mafanikio ya Liverpool, lakini Manchester City na Manchester United nazo zimekuwa zikitajwa kwenye vita ya kufukuzia huduma ya mshambuliaji huyo. Ripoti zinadai kwamba Man City wameshaandaa kabisa mipango ya kumsajili Mbappe na wanafikiria kuachana na mpango wa kunasa huduma ya Lionel Messi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mwandishi wa habari maarufu huku Ulaya, Josep Pedrerol, Mbappe ameshawaambia PSG kwamba anataka kwenda Madrid. Mbappe anaamini kwamba kwa kwenda kujiunga na Real Madrid atapata nafasi ya kukamilisha ndoto zake za kubeba Ballon d’Or.

Jambo hilo litamfanya awe kwenye orodha ya mastaa wa nguvu wa Ufaransa waliowahi kukipiga kwenye kikosi cha Los Blancos, akiwamo kocha wa sasa Zinedine Zidane.

Huko Ufaransa, PSG bado wapo kwenye matumaini makubwa kwamba mchezaji huyo hataondoka katika kikosi chao.

Advertisement