Haya, Timo Werner aanza tizi Chelsea

LONDON, ENGLAND. MAMBO ni moto. Straika mpya wa Chelsea, Timo Werner amewapa mzuka mashabiki wa timu hiyo baada ya kupigwa picha akionekana kwenye mazoezi yake ya kwanza na miamba hiyo ya Stamford Bridge.

Staa huyo Mjerumani alitua London hivi karibuni na Jumapili iliyopita alikuwapo uwanjani wakati timu yake mpya ya The Blues ilipoichapa Wolves 2-0 na kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Werner hakutaka kupoteza muda, ameanza kazi mara moja baada ya kwenda kujifua na wenzake huko Cobham, huku wachezaji wenzake wakijiandaa na fainali ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal, Jumamosi.

Werner haruhusiwi kucheza mechi hiyo itakayopigwa Wembley, lakini atatumia muda huo kuzoeana na wenzake kabla ya kuingia kwenye mapumziko ya kujiandaa na msimu mpya.

Mashabiki wa Chelsea walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii wakizungumzoa jambo hilo baada ya kumwona straika wao waliyemsajili kwa Pauni 54 milioni akiwa ndani ya uzi wa bluu wa Chelsea.

Mmoja aliandika: “Ona, jamaa amependeza kwenye bluu, sivyo jamani!

Mwingine aliandika: “Jamaa ameshakuwa gwiji tayari”.

Shabiki mwingine aliandika: “Yupo hapa na yupo fiti”.

Kuna shabiki mwingine wa Chelsea alisema: “Safi, atashinda Kiatu cha Dhahabu msimu ujao”.

Mashabiki wa Chelsea wana kila sababu ya kufurahia baada ya kuwapo na ripoti Kai Havertz yupo njiani kwenda kuungana na Mjerumani mwenzake huko Stamford Bridge.

Kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Havertz alizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kubonyesha kitufe cha like kwenye picha ya Werner aliyoposti kwenye Instagram baada ya kutua London.

Wawili hao kwa pamoja wamehusika kwenye mabao 40 na asisti 14 kwenye Bundesliga msimu huu.