Hatma ya kocha mpya Simba mikononi mwa Tenga ,Madadi

Tuesday December 3 2019

Hatma - kocha mpya Simba- mikononi mwa Tenga-Madadi- kurithi -mikoba ya Mbelgiji -Patrick -Aussmes-makocha-

 

By Thobias Sebastian

JANA Jumatatu vigogo wa Simba walianza kuchambua maombi ya makocha wanaotaka kurithi mikoba ya Mbelgiji Patrick Aussmes, ambaye amefutwa kazi hivi karibuni. Habari za kuamini ni kwamba, makocha kibaoa wametuma maombi kuitaka kazi hiyo, lakini shughuli pevu ni kwenye usaili ambapo, watakutana na watu waliobobea kwenye masuala ya soka wakiwemo makocha waliofundisha klabu mbalimbali kwa mafanikio makubwa.

Mbali na makocha, pia kwenye jopo hilo yumo aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ambaye utawala wake umekuwa ukipigiwa mfano mpaka sasa kutokana na kuweka misingi bora ya kukuza na kuendesha soka la Tanzania.

Wengine ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi na Sunday Kayuni ambao wote wana uzoefu mkubwa na soka.

Iko hivi, awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, alitoa nafasi kwa kila mjumbe kupendekeza kocha ambaye atakuja kuinoa timu hiyo baada ya kuachana na Aussems.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba, miongoni mwa makocha waliopendekezwa ni Goran Kopunovic, ambaye aliifundisha Simba msimu wa 2014–15. Hata hivyo, jina lake likakutana na upinzani hasa kwenye eneo la malipo hivyo, kukatwa mapema tu.

Imeelezwa kuwa Kopunovic ilipendekezwa ili kuinoa Simba hadi mwishoni mwa msimu, lakini pingamizi likawa ni kuwa kutokuwa kwenye timu kubwa yenye hadhi kama ya Simba.

Advertisement

Mwingine aliyependekezwa ni na wajumbe kuridhia ni Pierre Lechantre, lakini ishu ikaja kwenye mshahara ambapo, ili kupata huduma yake ni lazima mfuko utoboke kwelikweli. Habari za kuamini zinaeleza kwamba, kwa mwezi peke yake malipo ya Lechantre yanaweza kufikia Sh80milioni.

Kutokana na hilo, Mo akakabidhi mchakato wa kumpata kocha mpya kwa Ofisa Mtendaji Senzo Mazingisa, ambaye kwa kushirikiana na timu yake wanatarajiwa kuwasilisha majina ya makocha wasiozidi watatu kwa Kamati ya Madadi.

Baada ya kupitishwa kwa majina ya makocha hao watatu, wataletwa nchini na kukabidhi kwa kamati hiyo tayari kwa usaili na atakayepenya hapo ndiye atapewa dili la kuinoa Simba akiungana na Suleiman Matola.

Aussems, ambaye ametimuliwa mchakato wake wa kupata ajira Simba ulipitia utaratibu kama huo, kwa kamati maalumu ikiongozwa na Madadi kumfanyia usaili kisha kuwasilisha taarifa ya kitaalamu kwa uongozi wa Simba.

Hata hivyo, safari hii ameongezeka ni Tenga, ambaye hakuwemo wakati wa Aussems. Pia, safari hii atakosekana Dk. Mshindo Msolla, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Yanga. Kwa ufupi Mwanaspoti linakupasha kuhusiana na vigogo wa kamati hiyo.

OSCAR MIRAMBO

Kwa sasa ndiye Mkurugenzi wa ufundi wa TFF, akiwa amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Ami Ninje. Pia, amewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys ambayo ilishiriki mashindano ya mataifa Afrika kwa Vijana yaliyofanyika hapa nchini mapema mwaka huu.

Mirambo pia alikuwa mwalimu wa michezo katika Sekondari ya Makongo, ambayo ilikuwa na sifa ya kuzalisha wachezaji wengi vijana ambao, baadaye walikuja kuwa mastaa wakubwa kwenye klabu za Ligi Kuu Bara.

MADADI

Madadi kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, lakini amewahi kushika nafasi ya kocha mkuu na msaidizi katika klabu ya Simba kwa miaka tofauti. Pia, ndiye kocha pekee katika historia ya Simba aliyewahi kuifikisha kwenye fainali ya Afrika mwaka 1993.

Kabla ya Ninje kuchukua nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi, Madadi ndiye alikuwa akiishika mwaka 2017. Anatajwa kama mmoja wa viongozi waliokuza na kuhamasisha soka la vijana, waamuzi, timu za taifa na maeneo mengine ya msingi katika soka.

TENGA

Tenga kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), lakini amewahi kushika nafasi mbalimbali kama kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), nahodha wa muda mrefu Taifa Stars rekodi ambayo mpaka sasa haijavunjwa. Tenga, ambaye amepata kuzichezea klabu za Yanga na Pan African, ambapo baadaye alikuja kuwa kocha.

Nafasi nyingine ambazo ameshika Tenga ni msuluhishi wa mgogoro wa soka la Kenya, Mwenyekiti wa Baraza la Soka la nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).Pia, amekuwa Rais wa TFF akiongoza kwa mafanikio makubwa na kuacha alama.

Wakati Taifa Stars inashiriki Fainali za Mataifa Afrika mwaka 1980, Tenga ndiye alikuwa nahodha wake na baada ya hapo hatukupata nafasi hiyo hadi mapema mwaka huu.

KAYUNI

Kayuni mpaka sasa ni mkufunzi wa makocha anayetambulika na Caf, Mkurugenzi wa Ufundi Caf, Alikuwa kocha wa Yanga katika miaka ya 1997, baada ya hapo mwaka 2011 alikuwa, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF.

Alikuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Kocha wa AFC Leopards ya Kenya ambapo aliwapa ubingwa wa Ligi Kuu kabla ya kwenda tena kuinoa Bandari.

Madadi alipokea kijiti cha kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, 2017, ambacho kilitoka kwa Kayuni ambaye alimaliza kutumikia muda wake aliokuwa madarakani. Pia, amepata kuichezea Yanga.

MADADI AFUNGUKA

Madadi alisema mwaka jana alikuwepo katika kamati ya iliyomfanyia usaili Aussems, ambaye walimpitisha kutokana na sifa zake kulingana na mahitaji ya Simba.

“Mambo ambayo tuliangalia ni leseni ya kufundisha ya Caf, alikuwa na sifa za kufundisha soka la Afrika kwa maana ya kuanzia ligi za ndani na mashindano makubwa.

“Mbinu zake za kufundisha zinahitajika katika soka la sasa kwa maana ya kuweza kushindana na timu kubwa kama TP Mazembe, Al Ahly na nyinginezo, anaweza kuwa sahihi katika kuifikisha Simba kwenye malengo yake.

“Aina gani ya mbinu ambazo anatumia kulingana na mechi zilivyo na kwa nini anapenda kutumia mbinu hizo, anawasilisha vipi mbinu zake kwa wachezaji hadi kumuelewa ili kwenda kuzifanyia kazi katika mechi, anaweza kuishi na aina ya wachezaji na wachezaji wa kwetu na ligi yetu ilivyo,” alisema Madadi.

“Msimu huu vinaweza kuongezeka kama Simba watakuwa na malengo mengine tofauti lakini, mambo makubwa tutaanza kuviangalia hivyo kwanza. Baada ya kazi hiyo tutawasilisha mapendekezo yetu kwa uongozi waliotupa kazi,” alisema Madadi.

Advertisement