Hatma ya Wanyama ndani Tottenham Spurs kizungumkuti

Muktasari:

Kushindwa kuondoka kwa Wanyama licha ya kuhakikishwa na kocha Jose Mourinho kwamba kupata namba katika kikosi chake itakuwa stori kubwa, kunaweza kufananishwa na kauli mpya kitaani ya demu kula fare baada ya kutumiwa na mpenzi wake wa kiume kwenda kumtembelea.

Nairobi, Kenya.Kuna sheng mpya kitaa ya kukula fare ambayo unaweza kuihusisha na nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama ambaye kwa mara nyingine tena, ameshindwa kuigura klabu ya Tottenham Hotspurs licha ya kuwa ni wazi kwamba pale hatapata namba tena.

Ilitegemewa sana kwamba Wanyama angejiunga na klabu mpya kwenye dirisha dogo la usajili la Januari ambalo lilifungwa rasmi Ijumaa saa sita usiku.

Lakini licha ya kuvumishwa na zaidi ya klabu sita zilizoripotiwa kuwinda sahihi yake, hakuna hata moja iliyowasilisha ofa.

Kushindwa kuondoka kwa Wanyama licha ya kuhakikishwa na kocha Jose Mourinho kwamba kupata namba katika kikosi chake itakuwa stori kubwa, kunaweza kufananishwa na kauli mpya kitaani ya demu kula fare baada ya kutumiwa na mpenzi wake wa kiume kwenda kumtembelea.

Hii ni kwa sababu Wanyama kwa mara nyingine kaganda kuondoka licha ya kuwa wengi walitarajia angegura  ili akasake muda wa mchezo kwingineko.

Kabla ya msimu huu kuanza, hali ilikuwa kama hiyo hiyo. Klabu kadhaa zilijitokeza kumsajili lakini hakuna dili iliyofanikiwa.

Sababu mbili ambazo zinaripotiwa kuwa chanzo cha kusabisha uhamisho wa Wanyama kuwa mgumu ni hela.

Ya kwanza ni klabu zilizomuulizia Wanyama, zimekuwa zikishindwa na dau kubwa la Pauni 8 milioni ambalo wanaitisha Spurs.

Ishu ya pili ni mshahara mkubwa wa Wanyama wa pauni 65,000 kila wiki ambao kiungo huyo anapokea kwenye mktaba wake wa sasa na Spurs na aliogoma kuupunguza.

Kutokana na hali hii, Wanyama amelazimika kuendelea kusalia Spurs na sasa huenda akaondoka kama mchezaji huru pale mkataba wake uliosalia na miezi 18 utakapotamatika.

Akifunguka hivi majuzi na jarida la Football.London kuhus hatma ya Wanyama, kocha Mourinho alikiri wazi wazi haoni ikiwa  ana mipango yeyote ya kuhitaji huduma yake.

“Machoni mwangu naona tukijenga timu kwa kuwategemea wachezaji wachanga kama (Harry) Winks na Tanguay Ndombele ambaye anahitaji kuimarisha kiwango chake zaidi. Kwa hiyo sio rahisi kwa Victor ila ikiwa anataka kukaa nasi, hamna tatizo,” Mourinho alinukuliwa.

Alipiga hatua zaidi na kudokeza  pamoja na hali hiyo Wanyama hajaomba kuondoka Spurs.

“Kwa sasa  bado hatujapokea ofa zozote na  pia Victor mwenyewe hajatuarifu ikiwa anataka kuondoka”

Miongoni mwa klabu zilizoripotiwa kumwinda ni pamoja na Norwich, Galatasary, Celtic, West Ham na Aston Villa.

Toka alipojiunga na Spurs, kaichezea jumla ya mechi 154 za ligi kuu na kupachika magoli 10 na kutoa asisti tatu.