Harmonize afutiwa nyimbo YouTube mara ya 3, Uongozi wake wafunguka

Monday July 27 2020

 

By Nasra Abdallah

Msanii anayefanya vizuri kwa sasa katika muziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul maarufu Harmonize kwa mara ya tatu sasa ameendelea kufutiwa nyimbo kwenye mtandao wa YouTube kutokana kile kinachoelezwa na kuiga biti.

Hii ni baada ya jana Jumapili Julai 26, 2020 msanii Rosaree kuripoti kwenye mtandao wa YouTube kuhusu kuibiwa biti la wimbo Kanyor Aleng aliouachia wiki mbili zilizopita ambapo Harmonize ameutumia kuimba wimbo wa Amen.

Wimbo wa Amen Harmonize ameuachia juzi kwa ajili ya kuombeleza kifo cha aliyekuwa Rais Awamu ya Tatu,Benjamin Mkapa.

Hii sio mara ya kwanza kwa msanii huyo nyimbo zake kushushwa katika mtandao huo, kwani Novemba mwaka 2019 aliibua gumzo baada ya wimbo wa ‘Uno’ alioutoa kwa mara ya kwanza tangu aachane na WCB kufutwa.

Hii ni baada ya mtayarishaji wa sauti ya wimbo huo, Magix Enga,kutoka nchini Kenya kumpa wiki moja bosi huyo wa lebo ya Konde Gang kuoondoa wimbo huo kabla hajachukua hatua zaidi kutokana na kuchukua biti bila idhini yake.

Hata hivyo baadaye waliyamaliza na wimbo huo kurejeshwa.

Advertisement

Kama haitoshi Machi mwaka huu, albamu yake ya AfroEeat ilifutwa kwenye baadhi ya mitandao baada ya kuelezwa kutokuwa na hakimiliki kwa baadhi ya vionjoo vya nyimbo.

Kati ya waliomlalamikia msanii huyo anayefanya vizuri kwa sasa na wimbo wa Fall in Love ni wale wasanii wa Morogoro wanaojiita Nego kupitia wimbo wao wa kibanio,Harmonize anaelezwa kuiiba na kuiweka kwenye nyimbo yake ya ‘I miss you’ unayopatikana katika albamu hiyo.

Mwanaspoti imeutafuta uongozi wake ili kuweza kulizungumzia hili,ambapo meneja wake anayefahamika kwa jina la Mjerumani,amesema suala la wimbo wa Amen hawezi kulizungumzia kwa sasa kwa kuwa bado wanalifuatilia.

Wakati kuhusu kufutiwa nyimbo mara kwa mara kwa msanii wao, Meneja huyo amesema  ni mambo ya kawaida hutokea katika kiwanda cha muziki ukizingatia kwamba vionjo vingi vya nyimbo za kiafrika hufanana.

“Harmonize sio msanii wa kwanza kufutiwa nyimbo nchini na hata duniani, ni mambo ya kawaida katika muziki ukizingatia kwamba hakuna vionjo vya muziki wa Afrika ambavyo mtu anakuwa navyo peke yake kwani ni aina ya muziki ambao hufanana kwa koasi kikubwa.

“Nawaomba mashabiki wake watulie wakati suala hili linaendelea kufanyiwa kazi na tuna imani nyimbo hiyo itarudi,”amesema Mjerumani.

Advertisement