Mbio za magari... Hari Singh Rally Team wamepania kinoma ubingwa wa Tanzania

Wednesday March 25 2020

Hari Singh Rally Team wamepania kinoma ubingwa wa Tanzania,mbio za magari,Mandeep Dhani ,Rajpal Dhani ,

 

By Majuto Omary

Ni kawaida kwa familia moja kuwa na wanamichezo wanaojihusisha katika michezo tofauti. Hii inatokana na kuwa na mapenzi tofauti pamoja na ushawishi wa wazazi.

Pia kuna familia chache ambazo zinajihusisha na mchezo mmoja na kujizolea umaarufu. Mbali ya ushawishi wa wazazi, kuna wengine hutokea kupenda mchezo kutokana na ushawishi wa nyota mmoja ambaye wakati anacheza, yeye alikuwa shabiki wake.

Kuna wachezaji kama Scooter, Canyon, Jon, Brent na Drew ambao kutokana na mzazi wao Ricky Barry nchini Marekani kuwa nyota wa kikapu, watoto wamefuata nyayo zake. Kwa sasa Barry ni miongoni mwa wachezaji 50 wa zamani waliotamba katika mchezo huo nchini humo.

Katika mchezo wa tennis, kuna familia, mfano ya Richard Williams yenye wachezaji nyota wa mchezo huo, Serena na Venus ambao wameweka historia duniani. Mafanikio ya wachezaji hao yametokana na baba yao kuwa kocha wa mchezo huo. Williams amekuwa na msaada mkubwa kwa mabinti zake.

Kwa Tanzania pia kuna familia ambazo kutokana na ushawishi wa wazazi, zimeingia katika mchezo husika na kujizolea umaarufu. Ukiachana na mchezo wa kuogelea ambapo kuna waogeleaji watatu Celina, Peter na Alberto walioingia kutokana na mama yao Inviolata Itatiro kuwa kiongozi wa Chama cha Kuogea nchini (TSA), kwenye mbio za magari kuna familia ya Hari Singh Dhani ambayo watoto wanne hushindana katika mchezo huo.

Majina ya Gurjit Singh Dhani, Ajminder Singh Dhani, Rajpal Singh Dhani na Mandeep Singh Dhani ni maarufu katika mchezo wa magari.

Advertisement

Ndugu hao wameunda klabu inayoitwa Hari Singh Rally Team ambayo mbali ya kupata mafanikio imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo ya mchezo.

Katika mashindano ya kwanza ya kutafuta bingwa wa Taifa (NRC) wa mchezo wa magari, Ajminder alimaliza wa kwanza kwa kilomita 110 ndani ya dakika 40, sekunde 53 na nukta 7 katika mashindano yaliyofanyika mkoani Arusha.

Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha madereva 15, ndugu yake Mandeep Dhani alishinda nafasi ya tatu kwa kutumia dakika 41.31.3 huku Gurjit Singh akishika nafasi ya nne akitumia dakika 42.25.6 na Rajpal Dhani alimaliza nafasi ya tisa akitumia dakika 56.

HISTORIA KWENYE MBIO ZA MAGARI

Ajminder anasema walianza kupenda mbio za magari miaka mingi na baba yao mkubwa na mdogo, Surjeet Singh Dhani na Rajenderpal Singh Dhani ambao walishindana miaka ya 1970.

Surjeet alikuwa dereva na Rajenderpal Singh Dhani alikuwa ‘navigator’ na mbali ya kushindana nchini, pia walishindana nje ya nchi kama Kenya ambako mashindano ya East Africa Rally yalikuwa yanafanyika.

“Baba zetu hawakuwa na timu, walishiriki kama wao katika mashindano mbalimbali yaani binafsi tulipenda sana jinsi walivyokuwa wanashindana na sisi kuweka nia ya kufanya hivyo.

“Pamoja na magari ya kushindania mbio za magari yana gharama kubwa, haikuwa na vipingamizi kwa wazazi wetu kununua magari manne kwa lengo la kutimiza ndoto ya kila mmoja wetu, alianza Gurjit na Rajpal mwaka 2013 na baadaye mimi (Ajminder mwaka 2016) na Mandeep mwaka 2018,” anasema Ajminder.

Anasema kuwa unaweza kufikiria kuwa wao wanaishi pamoja, hapana, kwani kila mmoja pamoja na kufanya kazi katika kampuni ya ujenzi ya Hari Singh and Sons, kila mmoja anaishi eneo tofauti. “Mwingine yupo Dodoma, mimi nipo Dar es Salaam na mwingine yupo Moshi, pia kutokana na kazi yetu ya ujenzi, unaweza kujikuta upo eneo lingine kabisa, lakini wakati wa mashindano, tunakutana na kufanya mazoezi,” anasema akidokeza pia kuwa mwaka huu wamepania kufanya makubwa kwenye magari.

Anasema mafanikio katika mbio za magari yamewavutia wadhamini na sasa wanadhaminiwa na Benki ya Exim.

“Kushinda mashindano ya kwanza ya NRC ni ishara kuwa tumedhamiria kufanya vyema, lengo letu ni kushinda nafasi nne za kwanza na wengine kufuatia, tuna magari ya kisasa na vilevile tupo makini,” anaongeza.

Anasisitiza kuwa wamepania kushindana katika mashindano ya Afrika (ARC) ambayo yatafanyika nchini katika tarehe na mwezi utakaotangazwa baadaye.

“Tuna uzoefu wa mashindano mbalimbali ya kimataifa, tumeshiriki mashindano nchini Kenya kwa mfano Guru Nanak Kenya mwaka 2016, pamoja na kutomaliza kutokana na gari kuharibika, niliweza kufanya vizuri pia na kupata uzoefu,” anasema Ajminder huku akisisitiza mchezo huo unahitaji fedha ndio maana wachezaji wengi wanakwama.

Advertisement