Hafidhi Saleh kutoka dereva mpaka meneja wa klabu ya Yanga

Wednesday September 11 2019

 

By Charity James

WAHENGA hawakukosea waliposema kipenda roho hula nyama mbichi, msemo huo unaishi kwa mratibu wa Yanga, Hafidhi Saleh ambaye alijitenga na kila kitu kisa timu hiyo.

Tangu 2007 alipoanza kazi rasmi ya udereva Yanga, hakutaka kujihusisha na mambo mengine, familia yake haikuunga mkono moja kwa moja kazi hiyo, lakini kwa sababu alipenda aliamua kukomaa nayo.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Hafidhi na amefunguka mambo mbalimbali ikiwemo kufilisika, kisa Yanga, lakini tukio hilo halijamfanya ajute badala yake anaendelea kuitumikia kwa moyo mmoja.

DEREVA MPAKA MENEJA

Hafidhi alianza kazi yake rasmi ya udereva Yanga 2007 chini ya kocha Profesa Dusan Kondic ambaye alianza kuinoa klabu hiyo mwaka huo akipokea mikoba ya Jack Chamangwana.

“Kondic alidumu klabuni hadi 2010 na kuachia mikoba iliyochukuliwa na Kostadin Papic niliendelea naye kama dereva nikiwa chini ya Meneja Emmanuel Mpangala ambaye alimaliza majukumu yake sambamba na Papic,’” anasema.

Advertisement

“Mwaka 2011 nilianza rasmi majukumu ya umeneja baada ya Mpangala kumaliza muda wake, nilikuwa chini ya kocha Sam Timbe ambaye alifundisha mwaka mmoja na kutimuliwa na nafasi yake ilichukuliwa na Kostadin Papic ambaye alirudi tena Yanga kwa mara ya pili kwa mkataba wa miaka miwili.”

Hafidhi anasema, “Papic alinishauri nikasomee nafasi ya umeneja baada ya kubaini naweza kufanya kazi vizuri na kila kocha anayepita klabuni hapa nikiwa kama kocha na meneja kwa wakati mmoja, kocha huyo alitimuliwa tena na nafasi yake ilichukuliwa na Tom Saintifiet mwaka 2012.

“Saintifiet aliifundisha Yanga mwaka mmoja, nafasi yake ikachukuliwa na Ernest Brand mwaka 2012/13, akaondoka na nafasi yake ikachukuliwa na Hans Van Pluijm (2013/14), naye akaondoka.

“Akaajiriwa Marcio Maximo, alifundisha msimu mmoja na ndipo aliporudi tena Pluijm mwaka 2015/16, baada ya kutimuliwa walimuajiri George Lwandamina (2016/18). Hakumaliza msimu alimuachia Mwinyi Zahera.”

Hafidhi anasema katika tawala zote hadi kocha Lwandamina alitumika kama kocha na meneja wa timu, lakini chini ya utawala wa Zahera alibaki katika majukumu ya udereva na kubadilishiwa nafasi akiwa kama mratibu wa klabu.

AMEONGOZA YANGA MIAKA 18

Miaka 18 ni umri wa mtu mzima kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini ndio miaka ambayo ameifanya kazi Hafidh akiwa Yanga.

Anasema kuwa anajivunia kujuana na watu akiwa klabuni hapo ikiwa ni sambamba na kutengeneza familia.

“Nimekaa Yanga mwaka wa 18 sasa, sina ninachoweza kujivunia zaidi ya kusomesha wanangu na kuendesha familia ikiwa katika misingi imara. Najivunia kuwa mwanachama na uimara wangu umenipa uongozi wa matawi,” anasema.

“Mimi mbali na umeneja, uratibu ambao naufanya ni katibu mkuu wa tawi la Yanga Kariakoo, hii yote imetokana na utendaji mzuri chini ya viongozi na makocha niliofanya nao kazi na kingine naomba kuwajulisha Watanzania kuwa kupata kazi Yanga si rahisi, hivyo mimi kuweza kudumu miaka yote hiyo ni neema.

“Ni mtu wa watu wazee, vijana, watoto hii ni kutokana na kumheshimu kila mmoja, Yanga ni timu kubwa inaongozwa na watu wa kila aina mwenye hasira, furaha, nidhamu mimi nimeweza kufanya nao kazi bila ya kumuangusha kwa lolote najivunia hilo pia.”

SIRI YA KUONGOZA MUDA MREFU

Hafidh anasema uaminifu na heshima ndizo siri kubwa zilizomfanya adumu muda mrefu katika klabu ya Yanga huku akibainisha kuwa hata mapenzi aliyonayo kwa timu hiyo yamechangia kuweza kuelewana na viongozi hadi makocha anaofanya nao kazi.

“Mimi namheshimu kila mtu mtoto, mkubwa, kijana na hata mtu nisiyemfahamu, hicho kinaweza kikawa kigezo cha mimi kukubalika na viongozi wote niliofanya nao kazi na ninaoendelea kufanya nao kazi kikubwa ndio hicho,” anasema.

“Uaminifu wangu ni namna ambavyo nimeweza kufanya kazi na makocha wa kigeni ambao mara nyingi hawana utaratibu wa kuhifadhi vitu vyao vizuri, mimi nilikuwa na jukumu la kuweka katika usalama na kuwakumbusha, kitu ambacho kilikuwa kinanipa heshima kubwa hadi sasa nipo hivyo sina tamaa.”

MSHAURI WA MAKOCHA

Hafidhi anafanya kazi zaidi ya moja ndani ya Yanga ni dereva, mratibu wa timu na amekuwa akiwashauri makocha ambao amefanya nao kazi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo.

“Nina namba nyingi sana siku hizi na nyingine huwa nazipokea bila kufahamu ni nani kanipigia, wengi wao wamekuwa wakinitumia mimi kunipa maoni yao ili niweze kufikisha kwa kocha kutokana na ukaribu wangu na makocha wanaomba niwafikishie ujumbe wao, ambao kwa asilimia kubwa ni wa kuwashauri makocha,” anasema na kuongeza:

“Napokea simu kutoka mikoa mbalimbali kama nilivyokuambia kuwa mimi naheshimu kila mmoja, sina sababu ya kukata simu ya mtu, huwa napokea na kumsikiliza shida yake nini na baada ya hapo ndio nakata. Katika simu nyingi ninazopokea ni kumshauri kocha kuhusiana na majukumu yao, nimekuwa nikifikisha ujumbe na kumuacha kocha kuwa na uamuzi wa kutumia au kuacha.”

Anasema kwenye simu yake anazo namba zaidi ya 2,000 kitu ambacho kimemfanya aongeze simu nyingine ili aweze kumudu kuwasiliana na kila mtu ambaye anatamani kuzungumza naye.

ANACHOKIPATA KWENYE UMENEJA

Kuna siri nzito anatembea nayo Hafidhi ndani ya miaka 18 ya kufanya kazi Yanga, akifichua kuwa wapo mashabiki ambao hawaelewi timu ifanye vizuri ama vibaya, wao kazi yao ni kukosoa.

“Maisha ya Yanga ni magumu sana hasa ukiwa ndani ya uongozi kwani tunakutana na changamoto nyingi sana kutoka kwa mashabiki kwa kuwa kuna wanaoamini katika pasi nyingi hata timu ikikosa matokeo wanataka kubaki na kitu cha kuongea maskani kwao kwamba ilicheza vizuri,” anasema Hafidhi.

“Pia kuna wachezaji ambao wanataka matokeo tu timu hata ikicheza vibaya wao wanahitaji matokeo wasipopata wanaongea sana na hadi kutukana matusi ya nguoni hata kutukania wazazi uvumilivu ndio unaweza kukukalisha Yanga ukiwa na moyo mwepesi huwezi kuvumilia,” anasema.

ANACHOJIVUNIA

“Sina mafanikio makubwa tangu nimetua Yanga, kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba najivunia kufahamiana na watu na nimekutana na viongozi wakubwa ambao sikufikiria kama ningeweza kukutana nao, mpira umenikutanisha na marais.”

Anasema, “pia mbali na kufahamiana na watu nimeweza kunufaika na vyakula hasa tukisafiri kwenda mikoani huwa tunasimamishwa na mashabiki wanaoipenda Yanga na kutukusanyia nafaka kama mchele, mahindi, maharagwe na vyakula vingine vingi.

“Nimezunguka nchi nyingi kupitia Yanga, nimeenda mikoa mingi ambayo naamini nisingekuwa katika klabu hiyo sidhani kama ningeweza kwenda, hicho pia naweza kusema najivunia, kwa mafanikio hamna nipo kutokana na mapenzi japo kazi hii imenisomeshea wanangu,” anasema.

“Kidogo nachokipata kinalea familia ikiwa ni sambamba na kuwasomesha wanangu, nina watoto wanne wawili wa kike na wawili wa kiume wote wamesoma wa mwisho yupo kidato cha kwanza.”

WAZAWA NA WAGENI

Anasema soka la Tanzania linabadilika na linakua siku hadi siku kitu ambacho kinawafungua wachezaji wa ndani kulichukulia soka kama biashara na baadhi yao wameanza kutoka nje kwenda kucheza soka la kulipwa.

“Tumshukuru sana nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samata amefungua milango kwa nyota wengi kutamani kutoka kwenda kucheza soka la kulipwa na kuitangaza nchi yetu ikiwa ni sambamba na kuwa na wachezaji wengi wanaocheza timu ya taifa wakitokea nje ya nchi,” anasema.

“Zamani wazawa walikuwa hawajitambui, sasa wanajitambua na wanaonyesha ushindani kwa nyota wa kigeni, kikubwa kinachowabeba wageni wanakuwa na vitu vya tofauti na wazawa na wanakuwa na kitu cha ziada ambacho ni funzo kwa wazawa.

“Wachezaji wa kigeni wengi wanaokuja wanakuwa na vitu vya tofauti na naamini kama kuna wachezaji wanaweza kujifunza kupitia nyota hao wanaweza wakawa na njia rahisi ya wao kutoka na kwenda nchi nyingine kujaribu soka la kulipwa kama wanavyoona wenzao wanakuja Tanzania.”

FAMILIA ILIMFUNGIA VIOO

Katika maisha ya kawaida familia ndio imekuwa ikichangia mafanikio ya mtu na kupunguza, hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya familia ya Hafidh kutomuunga mkono katika kazi yake hiyo anayoifanya Yanga.

“Ndugu zangu hasa baba na mama walikuwa hawapendi kabisa mimi nijishughulishe na mpira wakiamini kuwa napoteza muda ni bora nikafanya kazi nyingine yeyote na si soka, lakini kutokana na mapenzi niliyonayo kwa Yanga sikusikiliza hilo,” anasema.

“Tangu nilivyokuwa na umri mdogo nilikuwa naipenda sana Yanga, nilivyopata nafasi ya kufanya kazi nilifurahi, hivyo sikutoa nafasi ya kuwasikiliza wazazi wangu nikiamini ninachokifanya nakipenda na niliamini nipo sahihi kwenye hilo.

“Niliingia Yanga kwa ajira, hivyo niliamini maneno ya wazazi hayawezi yakawa chachu ya kukata tamaa wakati nilikuwa na uhakika wa kuingiza fedha kama mwajiriwa, namshukuru Mungu nimeweza kufanya vitu vingi kwa familia yangu.”

USHIRIKINA NA SOKA

“Watanzania walio wengi wanaamini kuwa ushirikina unafanyika tena kwa kiasi kikubwa, mimi ninachokiamini si ushirikina ni mila za Kiafrika ndizo zinazofanyika kwa kushirikisha dini mbili ya Kikristo na Kiislamu, hayo ndio naweza kuzungumzia kwa sababu nimeyashuhudia na sio ushirikina,” anasema. “Timu inakuwa na wachezaji wenye dini mbili tofauti, hivyo tumekuwa tukifanya mila zote kwa kualika wachungaji kwa upande wa kwanza na mashehe upande wa pili ili kutoa somo kwa wachezaji kulingana na dini zao, na kuhusiana na suala la ushirikina sina imani na hilo na sijawahi kushuhudia ukifanyika.

“Ushirikina ungekuwa na nafasi kubwa michezoni, basi timu yetu ya taifa ingefika mbali ikiwa ni sambamba na timu zote zilizowahi kupata nafasi ya kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa wangeweza kutumia mbinu hiyo ili waweze kufanya vizuri, naamini hauna nafasi.”

UKOCHA NI ‘STRESI’

Anasema amedumu muda mrefu katika nafasi ya umeneja na sasa ni mratibuna akiwa karibu na makocha anafahamu changamoto wanazokutana nazo wakiwa katika benchi lao la ufundi, hivyo hafikirii na wala hajawahi kutamani kuwa kocha wa soka.

“Nimekaa karibu na makocha na nalifahamu soka kutokana na kusoma kozi mbalimbali zinazohusu mchezo huo sijawahi kufikiria au kutamani siku moja kufundisha mpira kwa sababu ukocha si kazi ya ajira ya muda mrefu, wapo kwa ajili ya kuchukuliwa na kutimuliwa hiyo kazi mimi siiwezi kabisa,” anasema Hafidhi.

“Unafanya kazi ukiwa huna uhakika wa ajira ya kudumu, huelewi kama unaendelea au unatolewa, sio kazi hiyo siiwezi na ukizingatia umri nilionao na magonjwa ya presha naweza nikafa, nawaachia wenye mioyo migumu mimi siwezi hata kidogo.”

5-0 ZA SIMBA ZILIMLAZA HOSPITALI

Mabao yaliyofungwa na Emmanuel Okwi ambaye aliingia kambani mara mbili, Juma Kaseja kwa mkwaju wa penati, Felix Sunzu na Patrick Mafisango yalitosha kumlaza kitandani Hafidh mwaka 2012.

“Katika maisha yangu ya soka kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Simba hakitafutika kwenye kumbukumbu, ni kipigo ambacho kiliniweka kitandani siku tano bila ya kutoka nje, nilipata maumivu makali na nakumbuka nilikuwa katika benchi siku hiyo,” anasema.

“Mbali na kipigo hicho pia nilipatwa na mshtuko mwingine katika mchezo wetu dhidi ya Simba, tena tulianza kushinda bao 3-0 kipindi cha kwanza wakarudi kusawazisha zote kipindi cha pili na mpira kumalizika kwa idadi ya mabao 3-3, nilijisikia vibaya sana kwani niliamini siku hiyo tunaweza kulipa kisasi kwa kuwafunga bao nyingi zaidi,” anasema na kuongeza:

“Mpira wa soka hauna matokeo mazuri kwa mwanadamu aliye na mapenzi ya kweli na timu hasa inapokosa matokeo mazuri wengi wanakutwa na matukio ya kuumiza na kusikitisha kwani kuna wanaozimia na wengine wanakufa kisa matokeo.”

MECHI ALIYOFURAHIA

Kwenye soka kuna matokeo matatu kushinda, kufungwa na kutoka sare. Katika matokeo hayo kuna aina zake za upokeaji kwenye ushindi ni furaha, sare ni furaha lakini isiyo zaidi na kufungwa ndio maumivu makubwa ambayo yamekuwa yakiwaumiza wapenda soka walio wengi. Hafidh anabainisha kuwa katika maisha yake ya soka amepitia matokeo yote, lakini pia katika kufungwa alishawahi kupata furaha baada ya timu yake kupata matokeo mabaya lakini ilionyesha mchezo mzuri ambao kila shabiki hakukasirishwa na matokeo.

“Nakumbuka mchezo huo ulikuwa ni ugenini tulifungwa lakini matokeo hata hayakutuumiza tuliona kama haikuwa bahati yetu kwani tulicheza mpira mwingi ugenini dhidi ya Waarabu Al Ahly, tulifungwa dakika ya 89 baada ya kupata sare ya bao 1-1 nakumbuka Donald Ngoma ndiye aliyesawazisha na baadaye ndio tukafungwa bao la ushindi,” anasema.

ALIJIWEKA REHANI KISA YANGA

“Naipenda sana Yanga tangu nikiwa na umri mdogo nimekuwa karibu na timu hiyo kwa kuifuatilia, sijawahi kuona ajabu kuidhamini timu hiyo ili tu iweze kufikia malengo wanayokusudia kuyafanya, mapenzi yangu kwa timu hiyo siyo madogo kama wengine wanavyonichukulia,” anasema.

“Nimeshawahi kujiweka rehani kwa ajili ya timu hii huwezi kuamini, nakumbuka nilisafiri na timu kwenda Arusha kwa ajili ya ya mchezo wa ligi dhidi ya Arusha FC, timu ilifikia hoteli ikitegemea mapato ya mlangoni kulipia hoteli waliyofikia na hatukufanikiwa kupata fedha ya kiwango tulichokuwa tunatakiwa kulipa.

“Niliamua kuwaomba viongozi wa hoteli wairuhusu timu irudi jijini Dar es Salaam ili iweze kuendelea na ligi halafu mimi nibaki hapo hadi timu itakapopata fedha ya kulipia kitu ambacho kilikubalika na timu ikasafiri, ilipofika baada ya siku mbili walifanikiwa kupata kiasi cha fedha kilichobaki na kutuma ili mimi niweze kuachiwa,” anasema.

Hafidhi anasema kuna mashabiki wanapambana na kutoa maneno makali kwamba wao wanaumizwa na matokeo mabaya ya Yanga na kutoa maneno machafu kwa wachezaji na makocha kitu ambacho hakina msaada kwa timu na hata kwa wachezaji wanaowatukana mwanachama.

ITAENDELEA ALHAMISI

Advertisement