HISIA ZANGU : Fei Toto, Diatta alama ya tunachovuna Cairo

Muktasari:

  • Kila wikiendi Diatta anacheza kishindani katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Leo atacheza na Genk ya kina Mbwana Samatta, wikiendi ijayo atacheza michuano ya Europa, na baada ya hapo atarudi nyumbani kucheza na Anderlecht.

ULIMUONA Fei Toto juzi Jumapili? Niliishia kucheka kwa uchungu. Unaachaje? Mmoja kati ya viungo bora kabisa katika Ligi Kuu yetu. Juzi alijikuta katika kundi la mamba wenye hasira akapwaya. Usingeweza kudhani ni Fei yule unayemfahamu.

Sitaki kumzungumzia Fei kama Fei. Taifa Stars haijafungwa kwa sababu yake. Imefungwa kwa sababu ya pengo kubwa lililopo baina ya Senegal na Tanzania. Kuna pengo kubwa la uwezo wa kiakili na kimwili kati ya wachezaji wa Tanzania na wale wa Senegal.

Fei alikuwa alama ya soka letu dhidi ya soka la Senegal. Fei, ni fundi kama alivyo lakini alipwaya kwa sababu moja tu kubwa. Hachezi soka la ushindani kila wikiendi. Wikiendi hii anacheza dhidi ya KMC, wikiendi ijayo anacheza na Namungo katika michuano ya FA.

Anacheza taratibu kwa sababu amezoeshwa hivyo. Hapati wapinzani ambao wanaweza kumbadili. Wikiendi nyingi anakutana na mechi nyepesi. Alishindwa kubadilika kwa sababu kasi ya mchezo ilikuwa kitu kigeni kwake.

Kipaji chake kama angekuwa anachezea Nantes ya Ufaransa kwa sasa ina maana angekuwa ana nguvu na utayari mwingi wa kucheza. Angekuwa ana akili iliyokomaa. Hii ndio tofauti ya Krepin Diatta aliyefunga bao la pili na Fei Toto aliyetolewa dakika ya 40 kipindi cha kwanza.

Kila wikiendi Diatta anacheza kishindani katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Leo atacheza na Genk ya kina Mbwana Samatta, wikiendi ijayo atacheza michuano ya Europa, na baada ya hapo atarudi nyumbani kucheza na Anderlecht.

Kama ilivyo kwa Fei, Diatta namchukulia kama mfano tu lakini wachezaji wote wa Senegal wanacheza Ulaya. Wote wanashindana kila siku. Wanashindana kuanzia kupata nafasi katika timu, hadi katika kuhakikisha nafasi zao hazipotei.

Ni wachezaji wanaolala nyumbani siku moja kabla ya mechi lakini ni wachezaji wenye ukomavu mkubwa wa akili na kimwili. Hii ndio tofauti ya Fei Toto na Diatta. Kwa kipaji inawezekana Fei Toto ana kipaji kikubwa kuliko Diatta. Lakini nani ana akili na mwili uliokomaa kucheza soka? Diatta.

Haya yanatokea wakati Fei Toto ana miaka 21 wakati Diatta ana miaka 20. Ina maana ndani ya miaka 20 tayari Diatta anacheza Ligi Kuu ya Ulaya, wakati Fei Toto hajaanza safari na anazidi kulegezwa kwa kucheza dhidi ya JKT Ruvu kila wikiendi.

Nilikuwa namtazama Fei wakati akitolewa hadi wakati kamera zikiwa zinamfuata katika benchi. Hakuonekana kukasirikia maamuzi ya Kocha Emmanuel Amunike. Alijua alipwaya na alistahili kwenda nje. Kasi ya mchezo ilimshinda na hakutegemea. Alidhani mechi ngumu dhidi ya Azam ni sawa na mechi ngumu dhidi ya Senegal.

Mtazame Farid Mussa. Ingawa anacheza Ligi Daraja la Kwanza Hispania lakini ungeweza kuona utofauti wake. Ana kasi, nguvu na akili. Muda mwingi alikuwa anajiamini na kujaribu kutunishiana misuli na mastaa wa Senegal kwa sababu amezoea kukaa gym Ulaya na kufanya mazoezi mengi binafsi. Yuko fiti.

Stars ina wachezaji tisa tu ambao wanacheza nje. Na wengi kati yao hawachezi katika ligi ngumu. Kabla hata hawa tisa hawajasogea kwenda mbali bado tunakabiliwa na changamoto ya wachezaji wengi wa ndani ambao hawana utayari wa kimwili na kiakili kukabiliana na Senegal.

Senegal ingeweza kutengeneza vikosi vingine viwili na bado Stars isingeweza kufua dafu. Wana kikosi kikubwa cha kuchagua wachezaji wao na wote wanacheza nje katika klabu ambazo ni maarufu zaidi ya Tenerife au Genk. Sisi tuna Mbwana Samatta ambaye tunataka afanye maajabu yasiyowezekana.

Yote haya yanatokea wakati Ibrahim Ajibu anapogomea kwenda TP Mazembe na kutaka kucheza Simba. Mashabiki wengi wa timu anayoenda wanamsapoti. Na ni mashabiki haohao wakienda kutazama mechi za timu ya taifa wanatazamia maajabu. Inachekesha sana.

Huu ndio muda ambao wachezaji wa Serengeti Boys kina Kevin John inabidi waondoke mapema kwa ajili ya kuzoea maisha ya kina Diatta. Hata hivyo, kila siku tunasikia danadana. Atatusaidia vipi siku za usoni kama haondoki sasa hivi?

Safari yetu ni ndefu. Imeonekana juzi. Kuna mengi tunaweza kuongea na kujidanganya lakini kwa sasa hatuna wachezaji wenye utimamu wa mwili na akili. Tutaishia kumchosha tu Samatta ambaye safari yake aliianza mapema.

Bahati mbaya tiba ya yote haya haitatokana na ligi isiyo ya ushindani kama yetu. Wachezaji wetu watoke. Hawawezi kupata utimamu wa mwili na akili kama wa Diatta katika umri wa miaka 20. Tatizo tumechelewa na tunaendelea kuchelewa huku wachezaji wetu wakipewa sifa nyingi katika magazeti.

Ukweli umejitenga juzi. Fei Toto ameonekana kama mtoto wa shule mbele ya Diatta na Idrissa Gana Gueye wakati si ajabu ana kipaji kikubwa kuliko wao. Ni wakati wa kujifunza na kuchukua hatua.