HATARI! HUU NDIO UCHAWI WA CARLINHOS

SI unaona zile kona bao za Carlinhos kwenye mechi za Yanga? Kama unafikiri jamaa huwa anazibahatisha ujue mapema utachekwa. Kiungo huyo kutoka Angola kumbe uchawi wake ambao umekuwa ukipagawisha mashabiki wa Jangwani na kuwapa presha mabeki wa timu pinzani huwa anaufanyia kazi kwa kutenga muda kila siku mazoezini ili kuzidi kuwa mtamu.

Ni hivi. Yanga imevuna pointi 10 kwa kutumia pasi mbili za viungo Carlinhos na winga Tuisila Kisinda, lakini unaambiwa kumbe ubora wao huwa wanaufanyia kazi kwenye mazoezi binafsi.

Carlinhos mpaka sasa ametengeneza mabao mawili akitumia mipira ya kona mbili katika mechi mbili na zote zikifungwa na beki Lamine Moro, lakini Tuisila ametengeneza bao moja akitumia krosi ikifungwa na kiungo Mukoko Tonombe.

Viungo hao wamekuwa wakijifua mazoezini kwa mipira ya namna hiyo ambapo kila mazoezi yanapoisha wenzao wakirudi kupumzika, wawili hao wanabaki na kujipa mazoezi ya aina mbalimbali ya mipira wakitumia muda usiopungua dakika 20 kunoa makali.

Carlinhos amekuwa akibaki na mipira yake 10 katika mazoezi, kisha hujaribu kupiga pasi za mbali na hata karibu akilenga lango na kufunga huku kukiwa hakuna kipa langoni.

Juzi, Mwanaspoti lilimshuhudia kiungo huyo raia wa Angola akifanya mazoezi hayo katika uwanja wa ndani wa kambi ya AVIC iliyopo Kigamboni - nje kidogo ya mji, mara baada ya wenzao kuondoka walipomaliza mazoezi ya pamoja yaliyosimamiwa na Said Maulid ‘SMG’.

Kiungo huyo alikuwa akipiga mipira hiyo ambapo alionekana kutumia dakika zisizopungua 15-20 kupiga mipira hiyo, huku Kisinda akimuangalia na kumuelekeza alipoona anakosea.

Katika mipira 10, Carlinhos alilenga lango na kufunga mipira sita, huku minne ikipaa juu kidogo ya lango. Tangu atue Yanga, Carlinhos amekuwa akiwakuna mashabiki kwa umahiri wa kupiga kona zenye macho ambazo zimekuwa zikitia misukosuko lango la wapinzani wao, na kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Mkapa aliingia kutokea benchi na kupiga kona matata iliyowekwa wavuni na Lamine Moro katika dakika za jioni.

Kisha alirejea tena Uwanja wa Jamhuri alipoanzishwa kikosi cha kwanza na kona yake ya dakika ya 61 kumaliziwa kwa shuti na Lamine ikiipa Yanga ushindi wa kwanza baada ya siku 1824 tangu walipoifunga Mtibwa kwenye uwanja huo mwaka 2015.

TUISILA NAYE SASA

Wakati Carlinhos akifanya yake, Kisinda alijaribu mipira kama hiyo, lakini zaidi alijielekeza kujaribu kukimbia kwa kasi na mpira kisha kupiga krosi katikati ya eneo la goli. Baada ya mazoezi hayo wawili hao walionekana kujadiliana mambo mbalimbali, kisha kuondoka kurejea kambini na kuonyesha kwamba kumbe wanachofanya katika mechi huwa wanavifanyia mazoezi.

Mpaka sasa mazoezi hayo yameipa faida Yanga ambapo imefanikiwa kuvuna pointi 10, kati ya hizo sita zikitengenezwa kwa mipira ya kona ya Carlinhos huku tatu zikipikwa na Kisinda kwa krosi.