HALI TETE: Mbeya City ikianguka, tatizo lilianzia hapa

Thursday July 2 2020

 

By MWANAHIBA RICHARD

MBEYA City ipo kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya kukusanya pointi 33 katika mechi 32 walizocheza, ambapo wamebakiza mechi saba pekee kumaliza ligi.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Mbeya City inashika nafasi ya 18 na chini yake kuna Mbao FC waliokusanya pointi 26 na vibonde Singida United wenye alama 15, timu zote zimecheza mechi 31.

Utaratibu wa msimu huu wa ligi, timu nne zinashuka moja kwa moja ambapo mbili zingine zitacheza mechi za mchujo na timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwani, msimu ujao wa ligi utakuwa na timu 16 badala ya 20.

Mbeya City ilitumia miaka saba kupanda Ligi Kuu Bara ambapo, msimu wa 2013/14 ndiyo ulikuwa msimu wa kwanza kucheza ligi hiyo kubwa nchini na kushika nafasi ya tatu huku Yanga ikitwaa ubingwa, Azam ikishika nafasi ya pili.

Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya iliwahi kushiriki michuano ya kimataifa ya Nile Base iliyofanyika nchini Sudan nafasi ambayo waliipata baada ya kushika namba tatu kwenye Ligi Kuu.

Hivi sasa timu hiyo iko kwenye shaka makubwa ya kubaki kwenye ligi msimu ujao kutokana na matokeo wanayoyapata ambapo, nyota walioipandisha timu hiyo wamezungumza na Mwanaspoti kuelezea mambo mbalimbali yanayoihusu timu hiyo, nini walifanya wakati wao pamoja na ushauri wao.

Advertisement

VIONGOZI WANAJUA TATIZO

Deus Kaseke alikuwa miongoni mwa wachezaji walioipandisha timu Ligi Kuu, alisajiliwa Yanga baada ya kufanya vizuri akiwa na Mbeya City, aliwahi pia kuichezea Singida United ilipopanda daraja amesema bado wana nafasi ya kubaki kwenye ligi.

“Viongozi wa Mbeya City wanajua tatizo la kuporomoka kwa timu, mfano Katibu Mkuu Emmanuel Kimbe anajua vizuri timu ilikotoka na inakoelekea, anajua ligi inataka nini pamoja na timu inahitaji nini kwa maana ya uendeshaji wake.

“Ni wakati wa Kimbe kujua jukumu la kufanya ili timu ibaki kwenye ligi naamini mechi zilizobaki wakifanya vizuri watakuwemo msimu ujao, wanatakiwa washinde nyumbani na kupambana ugenini, yote yanawezekana,” alisema Kaseke.

“Wakati ule ulikuwa ni wakati wetu, tulicheza kwa kuhitaji kufanya mambo makubwa binafsi kwa wachezaji ili tufanikiwe zaidi pamoja na mafanikio ya timu iwe miongoni mwa timu bora nchini, tuliweza hilo ingawa malengo yanatofautiana.

“Najisikia vibaya Mbeya City inapopata matokeo mabaya kwa sababu ni timu ambayo niliichezea, tuliipandisha na ikafanya vizuri ingawa sipo hapo tena, uwepo wao una maana kubwa jijini Mbeya.

“Sitarajii kuona inashuka ila kama itashuka basi vijana wengi watakuwa nyumbani, kwani ni timu ambayo imewafanya Wanambeya wajivunie na imetoa ajira kwa vijana wengi, waliokosa ajira Prisons waliajiriwa Mbeya City,” amesema Kaseke miongoni mwa wachezaji waliopandisha timu hiyo.

NONGA ADAI WACHEZAJI HAWAJITOI

Paul Nonga ni straika ambaye ni miongoni mwa wachezaji walioipa mafanikio Mbeya City amezungumzia sababu ya kuporomoka kwa timu hiyo kuwa; “Mwamko ulikuwepo, tuliwafanya mashabiki watusapoti kutokana na uwezo wetu uwanjani, tuliwasogeza karibu kutoka mbali.

“Timu ilikuwa na wachezaji wengi wenye njaa ya mafanikio, nidhamu ilikuwa kubwa, Kocha Juma Mwambusi na Maka Mwalwisi walitengeneza nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja.

“Wakati wetu ulikuwa huwezi kuona mchezaji yoyote ana rasta kichwani, nakumbuka kuna mchezaji alikuja na rasta ilimbidi anyoe, hivyo watengeneze nidhamu kabla hawajatengeneza timu. Mambo ya mitindo yalitakiwa yafuatwe baada ya mafanikio ya mpira, vyote hivi vinachangia timu kufanya vizuri.

“Tulitengeneza ushirikiano, tulipata sapoti kubwa kutoka Halmashauri ya Jiji, tulitazama mpira tu uwanjani, tulitengenezewa mazingira mazuri ya mishahara na posho, vyote hivyo tulivipata kwa kuvitengeneza wenyewe kwa kupata matokeo mazuri,” amesema Nonga.

Nonga ameelezea zaidi kuwa; “Ubora wa makocha ulichangia mafanikio makubwa ndani ya timu, makocha walichanganya kikosi kila sehemu, tulitengeneza kombinisheni nzuri na hamu ya mafanikio ilikuwa kubwa, tuliishi mazingira kama ndugu, umoja ulikuwa imara sana,” alisema.

“Kuondoka kwetu kulichangia kuporomoka kwa Mbeya City kwa kiasi kikubwa, kutengeneza timu ni rahisi ila ukiharibu ni ngumu kutengeneza na inachukuwa muda mrefu, tuliondoka zaidi ya wachezaji saba, ndiyo maana wanayumba maana wengi hawafiti.

‘’Baadhi yao waliokuja baada ya sisi kuondoka walianza kucheza kwa mazoea baada ya kuona timu imejulikana. Wasahau yaliyotokea wapambane kuhakikisha timu inabaki,” amesema Nonga

MWASAPILI HALALI

Hivi karibuni mashabiki wakiwa na matumaini ya ushindi wa nyumbani dhidi ya Aliance walijikuta wanaambulia kipigo cha bao 2-0. Hassan Mwasapili nahodha wa kipindi chote tangu timu hiyo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) anasema yupo katika wakati mgumu hasa kipindi hiki ambacho timu ipo kwenye mstari mwekundu.

“Hakuna kutafuta mchawi, hapa ni sisi wenyewe, tushirikiane tuwe pamoja. Nina imani kubwa kuwa tutafanikisha malengo yetu.

“Kipindi kile kila mchezaji alikuwa anatambua uwepo wake kwenye klabu, nafasi yake na namna ya kufanya kuipa mafanikio, msimu wa 2012/13 wote tulikuwa tunajitambua, asilimia kubwa tulikuwa hatujawahi kucheza ligi.

Mwasapili anaendelea kueleza kuwa; “Huwa naumia sana na matokeo haya, kipindi hiki nipo na wakati mgumu, matokeo yananifanya wakati mwingine nishindwe kutoka ndani, mechi ya Alliance iliniumiza sikulala siku mbili.”

Mbeya City imebakiza mechi sita, mechi mbili zitachezwa nyumbani dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania wakati mechi nne zitakuwa ugenini ambapo watacheza na Namungo, Ndanda, KMC na Azam.

“Kwa asilimia kubwa uongozi asilimia fulani wamechangia kufika hapa tulipofikia, mahitaji yanayohitajika yanayoonekana kutoyahitaji kwao, viongozi wanatakiwa kusimama kuwa kitu kimoja,” anaeleza Mwasapili, ambaye aliwahi kuichezea Azam kwa msimu mmoja na kurudi Mbeya City

MWAMBUSI AFUNGUKA

Kocha Juma Mwambusi ndiye kocha aliyeipandisha timu hiyo, kikosi chake kilikuwa na nyota wengi wazawa wa mkoa huo huku watatu pekee ndiyo aliwasajili akiwepo Nonga, Steven Mazanda ambaye pia ni mzawa ingawa alimsajili kutokana na uzoefu wake kuisaidia timu, wengine wote ni wale wapambanaji wa jiji hilo.

“Nilirudi Mbeya City ila sikuikuta Mbeya City ile ya zamani, hata ule utamaduni wetu haupo, viongozi waliopo sio watu wa mpira zaidi ya mmoja ambaye ni Katiba na tulikuwa naye toka huko mwanzo hivyo, anaelewa vizuri tulimopita.

“Wengi waliopo wanakupa presha pasipo kufuata ule utamaduni wetu tulioutengeneza wakati tunahangaika kuipandisha timu, kwanza kocha anapaswa kupewa muda wa kutosha kukaa na timu.

Wakati ule tulitumia sana wachezaji ambao wengi wao walitoka Mbeya, utamaduni ambao kwa sasa wameuharibu hatuhitaji kuchukuwa wachezaji wengi kutoka nje, wanatakiwa wazawa hata ukichanganya isiwe sana.

“Pia nilizingatia nidhamu, kujituma, uwajibikaji, na umoja ndani ya timu, hatukutengeneza makundi kuwa hawa wametoka mkoa fulani, kikubwa naiombea ipambane ili washinde mechi zilizobaki na wabaki kwenye ligi wajipange upya,” anasema Mwambusi.

KAULI YA KIMBE

Kimbe ni miongoni mwa viongozi pekee waliobaki kwenye timu hiyo ambao, walikuwepo tangu wanapambana kupanda Ligi Kuu Bara.

Kimbe anaifahamu Mbeya City pengine kuliko viongozi wote waliopo sasa.

“Bado mechi sita, imani yetu ni kushinda mechi zote ili timu ibaki kwenye ligi, hiyo ndiyo silaha yetu, hatuwezi kubaki kama hatutashinda mechi zilizobaki.

“Hatuna matokeo mazuri nyumbani, ila hatutaki kuangalia kwanini inakuwa hivyo, tumekubaliana wote kushinda, namna ya kushinda ni juu ya mwalimu, mechi zote kama fainali.

“Wachezaji waliokuwepo miaka sita ama zaidi hawawezi kuwa kama hawa walipo na hiyo ni kutokana na nyakati kubadilika.

“Mabadiliko makubwa ya wachezaji na makocha kwa muda mrefu, hiyo imetuathiri hasa ya makocha, tunabadilisha kila msimu, mabadiliko hayaepukiki kila sehemu kwani kunakuwa na sababu ya kufanya mabadiliko hayo. Maana wachezaji wengi waliondoka hivyo lazima waje wengine, maisha ya soka yapo hivyo”.

Kimbe amefananua zaidi kuhusu uchumi wa klabu kupitia mauzo ya jezi kuwa; “Tumepata changamoto kidogo, tofauti na msimu wa kwanza na wa pili, mfumo ambao tumeanza kwenda nao sasa wengi hawaujui, wengi walitaka mfumo wa zamani wa kila mtu kuuza ambapo tutaibiwa sana.

“Tumeisajili Brela Mbeya City iwe kampuni hivyo kila kitu kinapaswa kwenda kikampuni, ingawa msimu huu hatukuwa na mdhamini yoyote wa jezi baada ya yule wa kwanza Sport Master kumaliza mkataba wake, hivyo kupitia jezi hatujaingiza pesa ya kutosha hivi karibuni.”

Advertisement