HAKUNA MJADALA, PAUNI 400 MILIONI PESA INAYOTOSHA KUMNASA MBAPPE

Tuesday September 15 2020

 

PARIS, UFARANSA. WAACHE wauane. Asikwambie mtu, hii saini itawavuruga wengi, watatoana roho.

Unajua ni saini ya nani? Ni hii hapa, saini ya staa wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe.

Mbappe anatarajia kuanzisha vita ya Pauni 400 milioni kwa vigogo wa Manchester, Liverpool na Real Madrid.

Manchester City na Manchester United ndizo zinazopewa nafasi kubwa ya kunasa huduma yake kutokana na uwezo wao wa kusajili kwa pesa nyingi na kulipa mastaa wao mishahara mikubwa.

Fowadi huyo staa amebainika ataachana na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu. Kutokana na mkataba wake kubakiza miaka miwili msimu huu utakapofika mwisho, PSG inatarajia kupata Pauni 300 milioni kama ataamua kushikiria msimamo wake wa kutaka kuondoka.

Mbappe kwa sasa analipwa mshahara wa Pauni 15 milioni kwa mwaka na matarajio ni kwamba mshahara wake utaongezeka kwa Pauni 5 milioni zaidi atakapohamia kwenye timu nyingine. Na timu yoyote itakayofanikiwa kunasa saini yake, basi haitampa mkataba usiopungua miaka mitano, hivyo kwa Pauni 20 milioni kwa mwaka katika dili la miaka mitano, kwenye mishahara peke yake atakuwa ameingiza Pauni 100 milioni.

Advertisement

Man United, Man City na Real Madrid hawawezi kushtushwa na mshahara huo wa Pauni 100 milioni, lakini shida itakuja kwa Liverpool ambao hawana utamaduni wa kutumia pesa nyingi kusajili mchezaji mmoja, kama walitumia Pauni 310 milioni kunasa mastaa kibao kati ya mwaka 2017 na 2018. Lakini, mwa mwaka mmoja uliopita, wamiliki wa Liverpool usajili waliofanya hauzidi Pauni 20 milioni wakati alipiga dili kadhaa za kibiashara zilizowaongezea faida kama ya Pauni 32 milioni.

Hivyo kwa wababe hao wa Anfield kumsajili Mbappe watahitaji kuuza mastaa wake watatu kwenye fowadi, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane. Staa Msenegali, Mane anaweza kufungulia mlango wa kutokea kama ataendelea kushikilia msimamo wake wa kugomea kuongeza mkataba mpya kutoka huu wa sasa unaokwisha 2023. Real Madrid inamhitaji staa huyo, huku ikiamini inaweza kumnasa kwa ada ya Pauni 150 milioni.

Kuhusu Man City, wao walifanya jaribio la kumsajili Lionel Messi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kabla ya mambo kukwama. Kwa dili hilo walitaka kumlipa Messi Pauni 600,000 kwa wiki - hivyo suala la kumlipa mshahara mkubwa Mbappe atakapokuja kwenye kikosi chao haliwezi kuwa tatizo kabisa. Man United wao watamhitaji Mbappe kwa gharama yoyote ile kwa sababu wanaamini atazidi kuwaongezea umaarufu kwenye soka la dunia na hivyo kukamatia dili za pesa ndefu.

Uhusiano wa Mbappe na Jurgen Klopp ulikuja baada ya kocha huyo Mjerumani kumshawishi mshambuliaji huyo kwa saa kibao akajiunge na timu yake huko Anfield kabla ya kuamua kutua PSG.

Klopp alisema: “Nampenda sana, huo ndio ukweli. Ni mchezaji wa aina yake, ni kijana mzuri.”

Mbappe mwenyewe alishawahi kusema kwamba Liverpoo ni “mashine” wakati walipobeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kusubiri kwa miaka 30.

Advertisement