Gwambina, Biashara machinjioni

SASA ni rasmi, Bodi ya Ligi imevifungulia viwanja vya Karume mjini Musoma na Gwambina Complex, Mwanza, ambao ni uwanja wa nyumbani wa Gwambina. Hatua ya kufunguliwa kwa viwanja hivyo inatokana na marekebisho yaliyofanyika ili kukidhi kutumia kwa Ligi Kuu.

Meneja wa Biashara inayotumia Uwanja wa Karume, Frank Wabare alisema; “Hapa ndipo wachezaji wetu wanacheza kwa amani na kujiamini. Ndio nyumbani na tunarejea kwa nguvu, subirini muone vipigo,” alisema.

Kwa upande wa Gwambina, Mwanaspoti pia lilizungumza na Kocha Novatus Flugence ambaye alisema; “Wachezaji wetu karibu wote wameuzoea huu uwanja kwa sababu tangu Daraja la Kwanza mpaka michezo ya mwanzo wa ligi tulicheza hapa hivyo, tulivyofungiwa kuna vitu tulipoteza lakini nashukuru bodi kwa kuruhusu tuendelee kutumia na naamini tutakuwa bora zaidi.”

Baraza amekuwa na rekodi ya kibabe tangu apewe kazi ya kukinoa kikosi hicho msimu uliopita, amepoteza mchezo mmoja kwenye uwanja huo dhidi ya Polisi Tanzania walioshinda bao 1-0.

Msimu huu katika michezo minne waliyocheza nyumbani ikiwamo ule wa CCM Kirumba wameshinda zote, ikiwa ni dhidi ya Gwambina, Mwadui, Mtibwa Sugar na Ihefu ambao waliwala juzi bao 1-0.

“Hapa ni machinjioni, tunahitaji kuendeleza ushindi kuanzia nyumbani na ugenini pia, msimu huu sitaki kupoteza mechi yoyote na timu pinzani zielewe wazi zinapofika hapa hakuna mteremko,” alisema Baraza.

Kocha huyo raia wa Kenya aliongeza kuwa msimu huu anahitaji kuona timu yake ikitakata kila mechi na kwamba, kutokana na mwenendo walionao hivi sasa lazima wafikie malengo yao.