Guu la Chama lavuruga mambo huko

Muktasari:

KIPA wa Biashara United, Daniel Mgore ametamka kuwa hakuwahi kufungwa bao nne kwenye mchezo mmoja hivyo kipigo cha 4-0 walichokipata kutoka kwa Simba kimemharibia rekodi yake.

KIPA wa Biashara United, Daniel Mgore ametamka kuwa hakuwahi kufungwa bao nne kwenye mchezo mmoja hivyo kipigo cha 4-0 walichokipata kutoka kwa Simba kimemharibia rekodi yake.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Biashara ilichezea kichapo hicho kutoka kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa uwanja wa Taifa ikiwa ndio kichapo cha kwanza cha timu hiyo tangu imeanzishwa miaka minne iliyopita.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na Clatous Chama dakika ya tisa na 26 huku la tatu likifungwa na Medie Kagere dakika ya 52 na la nne likafungwa na Chris Mugalu dakika ya 84.

Kabla ya mechi ya Simba,Biashara ilikuwa imeshinda dhidi ya Gwambina na Mwadui.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgore alisema; “Ni jambo ambalo kwangu kila nikifikiria linaniumiza sana ishu sio kupoteza mchezo ila tatizo ni kufungwa mabao mengi kwenye mchezo mmoja ni mechi ambayo nitaikumbuka sana.

“Unajua tangu nimeanza kucheza soka la ushindani Daraja la Kwanza na Ligi Kuu nilikuwa sijawahi kufungwa mabao manne kwenye mchezo mmoja kitu ambacho sitoweza kukisahau kwenye ule mchezo,” alisema Mgore.

Alisema mechi ilikuwa ngumu sana kwao kwani Simba walikuja kwa kasi kubwa jambo ambalo liliwafanya wapoteane kabisa uwanjani na kuruhusu mabao hayo.

“Mechi ilikuwa ngumu sana kwetu tulipambana sana na kuweza kutoruhusu mabao mengi zaidi maana Simba walikuwa bora zaidi kikubwa sasa tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting,” alisema kipa huyo.