Gor Mahia hakuna kugura

Thursday June 13 2019

 

By Thomas Matiko

MWENYEKITI wa Gor Mahia anayeondoka Ambrose Rachier katamka wazi wazi katu hatakubali wachezaji wa klabu hiyo kumfuata naibu kocha wao wa zamani Zico aliyeikacha timu na kujiunga na KCB.

Rachier kasisitiza atahakikisha hakuna mchezaji anayemfuata Zico huko kwa wanabenki KCB. Kumekuwepo na tetesi kuna uwezekano wa wachezaji watano muhimu wa Gor wakamfuata Zico huko aliko kwa sasa.

Hata hivyo, Rachier kachekea uvumi huo akisema hamna mtu anayeondoka kwenda KCB akishikilia hakuna mchezaji aliyemwendea ofisini na barua ya kutaka kugura pia.

“Kile nilichopokea ni barua ya kujiuzulu yake Zico wala hamna mchezaji yeyote aliyenijia akiwa na nia ya kusepa” Rachier akasema.

Hata hivyo, Rachier kasema kuwa wataaachia baadhi ya wachezaji waondoke ili watengeneza nafasi ya kuweza kuwasajili mastraika wawili wapya, beki mmoja na kiungo.

Ishu kubwa kwa Gor kuelekea msimu ujao ni hawa straika baada ya washambuliaji wao Meddie Kagere na Jacques Tuyisenge kundoka. Kagere alisepa katikati ya msimu na kujiunga na Simba huku Tuyisenge akiondoka mwishoni mwa msimu kujiunga na  Petro Atletico ya Angola.

Advertisement

Kumekuwepo na ripoti tayari wameshamsajili straika wa Sony Sugar, Derrick Otanga aliyemaliza msimu kwa kupachika magoli 13 hata hivyo uongozi huo umekanusha.

“Hatujamsajili Otanga wala mchezaji yeyote yule. Dirisha la usajili bado halijafunguliwa ila ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba tayari tumeanza mazungumzo na wachezaji kadhaa sema siwezi kuwataja sababu wengi wao wangali na mikataba na klabu zao,” kasema Naibu Katibu Mkuu Ronald Ngala.

Advertisement