Gofu majeshi kutimua vumbi

Mashindano ya mkuu wa Majeshi ya mchezo wa Gofu yanatarajia kutimua vumbi katika viwanja vya Lugalo Septemba 19 na 20.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2020, Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwogo amesema wamejipanga kuhakikisha mashindano hayo yanaenda vizuri.

Luwogo amesema zoezi la usajili wa wachezaji katika mashindano hayo linaendelea ambapo mpaka sasa wachezaji 110 wamejiandikisha kushiriki.

Amesema mashindano hayo yatawashirikisha wachezaji kutoka klabu zote za gofu hapa nchini hivyo anaimani ushindani utakuwa mkubwa na mzuri kwa washiriki wote.

"Mashindano ya Mkuu wa Majeshi hufanyika kila mwaka na tutaenda Septemba 18 kwa wasimamizi huku 19/20 wachezaji wa ridhaa, tunaishukuru NMB kwa kudhamini," amesema Luwogo

Luwogo amesema mchezo huo unashirikisha rika zote ambapo watoto watapata nafasi ya kushiriki.

Kwa upande wake Omary Mtinga kutoka NMB amesema wao wamekuwa wakijitosa kudhamini mashindano hayo ambapo mwaka huu wametoa Sh 40 milioni kwa ajili ya kusapoti mashindano hayo.

"NMB tumekuwa karibu sana na majeshi ndio maana kila mwaka tunadhamini mashindano haya, mwaka huu kama mnavyoona tumeboresha udhamini wetu na tutaendelea kudhamini," amesema Mtinga

Kwa upande wa Meja Frank Kaluwa ambaye ni Meneja wa Klabu ya Gofu amesema wamejipanga kuhakikisha mashindano hayo yanaenda vizuri zaidi.

Amesema kila kitu kipo sawa na kilichobaki kuanza kwa mashindano hayo ambapo wanatarajia kuwa na washiriki wengi zaidi.