Ghafla Liverpool imegeuka kuwa binti maringo?

GORDON Brown, Waziri Mkuu wa zamani wa England aliwahi kuulizwa ni kitu gani kizuri Waingereza wanazalisha kwa sasa na dunia nyingine inaweza kujivunia. Alijibu kwa maringo yaliyopitiliza. Alijibu kwa kifupi. “Ligi Kuu ya England”.

Unaweza kumkatalia? Hapana. Kuanzia Malaysia, Newala kule Mtwara, New Delhi India, Miami Marekani, Buenos Aires pale Argentina na hata Melbourne pale Australia. Wote tunasubiri Ligi Kuu ya England.

Mwamuzi wa pambano la Fulham na Arsenal, Chris Kavanagh atakapopuliza filimbi kuanzisha pambano la kwanza la Ligi Kuu ya England pale Craven Cottage tutakuwa tunakaribishwa katika ligi maarufu zaidi duniani. Tunasubiri kuona nini msimu huu? Liverpool atatetea taji? Man City atapora taji? Manchester United ataingia Top Four au kuwania ubingwa? Arsenal ataingia Top Four? Chelsea yupo katika anga za ubingwa? Wote tunatazama kule juu.

Wakati tukitazama juu tunamkuta mtu ambaye watu watakuwa na hasira naye zaidi. Liverpool. Ndiye namba moja mpaka sasa. Kuwa namba moja ni rahisi, kuendelea kuwa namba moja ni kitu kigumu zaidi katika maisha ya soka.

Liverpool kuna mawingu kidogo. Anatazamiwa kutetea taji lakini wako wapi wachezaji wapya? Nahisi kuna kiburi kinaendelea pale Anfield. Kama sio kocha basi matajiri wanaringia kikosi chao. Kiburi hiki kinatoka wapi?

Tulidhani wangeingia sokoni kwa nguvu kuimarisha kikosi chao. Wamemchukua beki Mgiriki, Kostas Tsimikas katika upande wa kushoto ambaye tunajua anakwenda kuwekwa benchi na Andy Robertson. Sioni akichukua namba pale. Robertson amefiti vema katika mfumo wa Jurgen Klopp.

Kabla ya hapo Januari alitua mchezaji anayeitwa Takumi Minamino ambaye mpaka sasa ameshindwa kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza. Alikuwa mchezaji mzuri, lakini nadhani Klopp alitaka kutuonyesha uwezo wake wa kufanya maajabu ya kumgeuza mchezaji wa kawaida kuwa wa ajabu kama alivyofanya kwa Mane. Liverpool ilipaswa kuingiza kikosini wachezaji ambao wana ubora wa kupora nafasi za waliopo hasa katika eneo la kiungo na ushambuliaji. Inaonekana kama vile Klopp anawalinda Mo Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino. Tulidhani angemchukua Timo Werner akamuacha aende Chelsea.

Tulidhani eneo hilo Klopp angepambana kumnasa mchezaji wa daraja la juu ambaye angeidai nafasi yake kutoka kwa Mane au Salah au Firmino. Hata hivyo mwamuzi wa pambano la Liverpool na Leeds akikaribia kuanzisha kipute pale Anfield bado hawa watatu hawajapewa mpinzani. Kwa sasa anahusishwa Thiago Alcantara. Inawezekana akamchukua. Huyu ndiye mchezaji tuliyemtarajia. Huyu ni aina ya mchezaji ambaye anaingia katika timu huku akiidai nafasi yake na si kusubiri kucheza mechi za Carabao au FA kama ninavyotazamia kwa Kostas Tsimikas.

Inawezekana Klopp anakwenda katika msimu mwingine wa nne wa timu iliyokamilika akiwa na matumaini yale yale. Kuna ule msimu aliukimbiza ubingwa wa Ulaya, lakini akapigwa fainali na Real Madrid pale Ukraine.

Kuna msimu mwingine ulikuja mbele yao ambapo waliukimbiza ubingwa wa Ulaya na kufanikiwa kuupata pale Madrid baada ya kuichapa Tottenham. Ndani ya msimu huo huo waliachwa pointi moja na Manchester City katika mbio za ubingwa.

Msimu uliofuata wametwaa ubingwa wa England. Namaanisha msimu uliopita. Yote haya yanafanyika huku Liverpool ikiwa na utatu mtakatifu pale mbele. Mane, Salah na Firmino. Wataendeleza mwendo mdundo mpaka lini? Ni swali la kujiuliza kwa umakini.

Wataendelea kupewa changamoto na Divork Origi mpaka lini? Labda angeingia Timo Werner angewapa changamoto zaidi. Timu lazima ichangamshwe mara kwa mara. Sir Alex Ferguson alikuwa ana uwezo wa kufanya hivyo.

Katika soka kuna kitu kinaitwa ‘Second Season syndrome’. Huu ni uchovu wa msimu wa pili baada ya kufanya vema katika msimu uliopita. Baada ya ubingwa wa England ambao waliusaka kwa miaka 30 hatuwezi kujua wachezaji wataamka msimu huu wakiwa na uchovu upi. Ni katika nyakati kama hizi, Sir Alex alikuwa anajua namna ya kukichangamsha kikosi chake.

Oktoba 5 dirisha la uhamisho litafungwa. Sio mbali sana katika masuala ya uhamisho kwa sababu kunakuwa na mchakato mrefu linapokuja suala la uhamisho wa mchezaji. Siamini kama Liverpool itakuwa na maajabu sana.

Majuzi nilimuona Jurgen Klopp akiwa na sura nyekundu alipoulizwa kusuasua kwa Liverpool katika uhamisho wa wachezaji. Akatoa jibu la kukejeli Chelsea na Manchester City kwamba zina pesa nyingi kutoka kwa matajiri wa mafuta. Ukweli ni kwamba tangu 2016 Liverpool ilipotinga fainali za Europa na kuanza kupata mafanikio mengi katika kipindi hiki ni wazi pia wameingiza pesa nyingi. Mafanikio hayaji bure. Yanaambatana na pesa. Liverpool imevuna pesa nyingi kwa kutwaa ubingwa wa Ulaya na pia kufika fainali waliyochapwa msimu mmoja kabla.

Klopp asitake kuniambia Liverpool ni masikini. Ubahili wa sasa inawezekana unatokana na matajiri wa Kimarekani kuanza kuwa na mkono wa birika au yeye mwenyewe kuamua kuanza kufuata nyendo za Arsene Wenger. Sina ndoto nzuri kuhusu Liverpool ya msimu huu. Nina ndoto mbaya. Napata usingizi wa mang’amung’amu kidogo.