Gerald Mdamu Soka lilimlaza juu ya mti

Muktasari:

Mwanaspoti lilipiga stori na mshambuliaji huyo na kufunguka kuhusu maisha yake binafsi na yale ya soka.

HAPA Bongo, ifunge tu Simba au Yanga, tayari una jina kubwa. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Gerald Mathias Mdamu aliyeichezea Mwadui FC kwa misimu minne.

Ni hadi ilipofika Oktoba 30 mwaka jana, Siku aliyoitungua Simba na kuitibulia rekodi yake ya kutokufungwa michezo 15 mfululizo kwa kuipa ushindi timu yake ya Mwadui FC kwa bao lake la kichwa lililomshinda kipa Aishi Manula dakika ya 33 na kuondoka na pointi tatu.

Mwanaspoti lilipiga stori na mshambuliaji huyo na kufunguka kuhusu maisha yake binafsi na yale ya soka.

Soka lamlaza juu ya mti

Changamoto ni moja ya msukumo wa kuyafikia mafanikio ikiwamo kutokukata tamaa. Ni kama ilivyokuwa kwa Mdamu ambaye pamoja na kufikia mafanikio haya, anaeleza, aliwahi hadi kulala juu ya mti kisa soka na hii ni kutokana na kuogopa kichapo kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa hapendi kabisa ajihusishe na soka.

“Namshukuru Mungu hadi hapa nilipofikia kwani nimepitia mengi ikiwamo kupigwa sana na baba kuanzia uwanjani nikicheza mpira. Nilikuwa nikifanikiwa kumtoroka nakimbia na naogopa hata kurudi nyumbani kuhofia kichapo zaidi na hapo naamua tu kwenda kulala juu ya mti,” anasema.

“Baba alikuwa mkali sana. Alikuwa hapendi utani kabisa. Kuna muda alikuwa anamzuia hadi mama asinipe chakula kosa likiwa ni mimi kujihusisha na soka, hivyo, nashinda njaa, lakini akiondoka, mama kwa huruma yake, alikuwa ananipa chakula,” anasema.

Ndoa yakatisha masomo

Baba na mama wanapokwaruzana kwenye familia, watoto ndio wanaoteseka. Wanakosa haki zao za msingi ikiwamo elimu. Mdamu anaeleza jinsi ndoa ya baba yake ilipoingia dosari na kushindwa kuendelea na shule ingawa alipenda kufika mbali.

“Baba na mama walitengana kutokana na matatizo yao ya kimahusiano na baba alikuwa anaisahau kabisa familia yake na kutuacha tukiteseka kupata fedha ya kula kitu ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea na shule nianze kujihusisha na soka ili nipate fedha ya kujikimu mimi pamoja na mama yangu ambaye kwa sasa ni sarehemu,” anasema.

Amkataa baba

“Tangu baba na mama watengane mimi nilikuwa upande wa mama (Mwenyezi Mungu ampumzishe sehemu salama), baba alikuwa hana mapenzi na familia yake na tangu alipomwacha mama hadi sasa sina mawasiliano naye wala sijui yuko wapi,” anasema.

“Alikuwa kikwazo kwenye upambanaji wangu wa kutaka kucheza soka hilo halikuniumiza sana kutokana na alikuwa ananijenga ili niwe msomi lakini hilo la shule pia alishindwa kulikamilisha aliivuruga familia kwa kumsumbua mama yangu akishindwa kumuachia hata fedha ya matumizi hilo ndio liliniumiza sana,” anasema.

Ndondo  Cup  yamtoa

“Baada ya baba na mama kutengana niliamua kuachana na shule na kujikita kwenye soka. Nimecheza timu nyingi siwezi kukumbuka ngapi. Nimecheza sana mashindano ya kombe la Mbuzi na lengo likiwa ni kupata kipato ili kuisaidia familia yetu,” anasema.

“Timu iliyonitoa na kunifanya nikajulikana na kusajiliwa na timu ya Ligi Kuu ni Tabata United ilikuwa inashiriki Ndondo Cup. Uwezo wangu ndio uliwavutia mabosi wa Mwadui FC ambao waliamua kunipa mkataba na ndio timu ninayoitumikia hadi sasa.”

“Siwezi kuzungumzia sana ligi kwani nimecheza timu moja tu hadi sasa,” alisema na kuongeza, “Maisha ya Mwadui ni ya kawaida kama zilivyo timu nyingine zote,” anasema.

HAJAWAHI KULA UMEME

“Soka ni burudani nafurahi kucheza na najituma ili niweze kufanikiwa kupitia kazi hiyo, hivyo mara nyingi nimekuwa nikicheza kwa nidhamu lengo ni kuona nafikia malengo. Najivunia sijawahi kuonyeshwa kadi nyekundu na sitamani janga hilo linikute,” anasema Mdamu ambaye anakumbuka alivyotua tu Mwadui, mshahara wake wa kwanza alinunulia Smart phone aina ya Tecno Phantom 6 Plus anayoitumia hadi sasa na akiapa hatokaa aiuze kwani itabaki kumbukumbu yake.

Tchetche, ronaldo wamkuna

Tangu aanze kucheza Ligi Kuu mwaka 2016 akiwa na Mwadui FC, Gerald amekuwa akivutiwa na soka la mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche.

“Tchetche ni mpambanaji na huwa hakati tamaa. Hadi sasa huwa namfuatilia kupitia vipande vya video akiwa uwanjani. Natamani siku moja ningepata nafasi ya kucheza naye timu moja,” anasema Mdamu na kuongeza kwa soka la Ulaya anavutiwa zaidi na nyota wa Juventus Mreno, Christan Ronaldo.

“Ni mchezaji wangu bora miaka yote. Ni mpambanaji japo umri umeenda. Napenda sana kumfuatilia,” anasema.

CHIRWA TISHIO ZAIDI

Mdamu anajua soka, hivyo anajua ni nani aliye bora na hapa anakupangia kikosi cha wachezaji wa Ligi Kuu bara inayoendelea kwa sasa na anaamini tishio zaidi ni Mzambia Obrey Chirwa wa Azam FC.

Kipa Musa Simba, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Bakari Nondo, Yocob Mohammed, Abdulilazizi Makame, Awesu Awesu, Abdulazizi Makame, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Chirwa, Gerald Mathius na Ally Ramadhan.

“Kikosi hicho kina wachezaji bora kila idara timu pinzani wanatakiwa kujipanga sana kwani kinaweza kikawa kinatwaa mataji kila msimu ni wachezaji wenye uchu wa mafanikio na wapambanaji,” anasema mshambuliaji huyo ambaye anasema kwake akiwa uwanjani hachagui nafasi, mpange mshambuliaji au kiwango, utamkubali tu na anaimudu zaidi ushambuliaji kwani Kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ndiye aliyenibadilisha namba alipokuwa anaifundisha Mwadui FC.

Geita yamtoa kijasho

Unakumbuka zile mechi za play off na Mwaduiu ilikuwa ikicheza na Geita? Unaambia ndio mehi ambayo Mdamu hawezi kuisahau kutokana na walitakiwa wajinasue kushuka daraja.

“Ilikuwa Juni 10, 2019 dhidi ya Geita. Mchezo huo wa play off ziwezi kuusahau. Tulipambana kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu. Ni hadi dakika za mwisho ndio tulibahatika kupata bao la pili baada ya kupata sare ya bao 1-1,” anasema na kuongeza, “Baada ya hapo ilibidi kujilinda tukiombe mpira uishe na baada ya refa kupuliza kipenga cha mwisho, tulilipuka kwa shangwe na kila mchezaji hakuamini kutokana na kazi kubwa tuliyoifanya.”