Geita Gold ikishindwa kupanda kuna mkono wa mtu

MAMBO yameanza kuiva huko Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayotarajia kutimua vumbi wikiendi hii katika msako wa timu mbili zitakazopanda moja kwa moja Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa taarifa yako wachimba madini kutoka Geita, Geita Gold wametamba tayari wanachukua nafasi moja hivyo wapinzani wake watangoja hatua ya mtoano. Geita Gold ni moja ya timu tishio FDL na inapokutana na wapinzani wao hupaswa kujipanga vilivyo.

Msimu huu mambo yamekuwa tofauti kuanzia benchi la ufundi ili kuhakikisha kikosi hicho kinakuwa tishio zaidi. Baada ya Gipco FC kupigwa bei sasa inawafanya wachimba madini hao kubaki wenyewe na kukusanya mashabiki wa mkoa wote kuwasapoti kwenye mbio za kuwania safari ya kuelekea Ligi Kuu.

WAMEJIPANGA

Ofisa Habari wa timu hiyo, Gabril Gabo anasema usajili walioufanya na mabadiliko ya benchi la ufundi vinawapa jeuri kupambana na kujipa matumaini ya kupanda Ligi Kuu. “Misimu miwili tumeishia hatua ya mtoano na tumeonyesha kiwango kikubwa kwa muda wote huo, hivyo tunaamini msimu huu kila kitu kitakwenda sawa,” anasema.

“Timu ilianza mazoezi mapema chini ya Kocha Fred Minziro, na asilimia kubwa ya wachezaji wapo fiti, kikubwa ni mapambano pekee yanayongojewa kwa sasa.”

Anawaomba wadau na wapenzi wa soka kuipa sapoti timu yao ikiwa pamoja na kuifuatilia kwenye michezo ya nyumbani na ugenini.

Gabo anasema kazi kubwa ya Minziro ni namna ya kutafuta kikosi cha kwanza kutokana na usajili bora na ndio maana hata katika michezo mitatu ya kwanza ya kirafiki kocha alikuwa akibadilisha wachezaji.

“Tumecheza na Kagera Sugar hapa nyumbani na kutoka nao sare ya mabao 2-2, kisha tukacheza na Gwambina pale Misungwi, Mwanza na tukapoteza 2-1 kisha tukaichapa 2-1 Mwadui FC nyumbani kwao,” anasema.

MINZIRO APEWA KAZI

Agosti 29 uongozi wa Geita Gold ulimtambulisha Minziro kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Msimu uliopita Minziro alizifundisha timu kadhaa ikiwemo Alliance, Mbao, Mawenzi, Pamba na sasa kajiunga na Geita Gold.

Unapotaja makocha wenye rekodi zao huko FDL, basi huwezi kulisahau jina na Minziro aliyezipandisha Ligi Kuu timu za Singida United msimu wa 2016–2017, kisha 2018/19 akaipandisha KMC.

Mara zote Minziro hueleza katika soka hasa la FDL kazi inakuwa nyepesi kama timu ina pesa, lakini pia sapoti na ushirikiano wa uongozi wa timu kwa benchi la ufundi.

“Hakuna kitu kinachoshindikana kwenye soka kama una watu wanaojua soka na wanaojituma, kufungwa ni moja ya sehemu ya michezo, hivyo kikubwa ni kupambana zaidi,” anasema kocha huyo.

Anasema FDL ni moja ya ligi ngumu, lakini anaamini atafanikiwa kutimiza lengo la timu kwa kadri iwezekanavyo na anaona mwanga baada ya mazoezi waliyoyafanya kwa siku kadhaa.

TUJIKUMBUSHE

Kama utakumbuka msimu wa 2016/17, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilizishusha timu nne za FDL kutokana na upangaji wa matokeo michezo ya mwisho.

Geita Gold Mining ni mojawapo ikiwemo JKT Oljoro ya Arusha, JKT Kanembwa ya Kigoma na Polisi - Tabora baada ya michezo ya mwisho Geita ilishinda mabao 7-0 mbele ya Kanembwa na Oljoro ikifungwa 7-0 na Polisi. Hata hivyo, Geita ikatumia ujanja wa kuinunua Mshikamano na kubadilisha jina ikaitwa Geita Gold iliyoifanya kuendelea kudunda ndani ya FDL.

SHUGHULI WANAIJUA

Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya pili na alama 37 na katika hatua ya awali ya mtoano ilikutana na Majimaji na kuichapa 2-1 ugenini kisha ikashinda kwa idadi hiyo nyumbani.

Hatua iliyofuata ilikutana na Mbeya City na kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani kisha kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kuifanya Geita kuendelea kusota FDL.