GF Trucks yaibeba tena Mbao FC

Muktasari:

Huu ni mwaka wa tatu kwa GF Trucks kuidhamini Mbao FC baada ya leo kusaini mkataba wa mwaka mmoja

HUU ni mwaka wa tatu kwa Mbao FC, kudhaminiwa na Kampuni ya GF Trucks and Equipment LTD baada ya leo Ijumaa kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja.
Hii ni mara ya tatu kwa Kampuni ya GF Trucks and Equipemnt LTD kuidhamini Mbao FC ambapo iliidhamini miaka miwili iliyopita.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Imran Karmoli, alisema walipata ushawishi wa kuidhamini Mbao kwa madai ya kutaka kusapoti mpira wa miguu nchini ili kuhakikisha unakuwa na ushindani.
Mbali na wao kuidhamini Mbao FC, pia alitoa mwito kwa kampuni zingine kuidhamini timu hiyo kwamba watapata mafanikio au faida ya kuwekeza kwao.
"Lengo letu ni kuona soka linasonga mbele kwani linawapa ajira vijana wengi, hilo linatupa nguvu kushawishi makampuni mengine kuwekeza Mbao FC ama timu nyingine.
" Tumefaidika na Mbao FC wamefaidika, ingawa kulikuwa na changamoto ya hali ya juu kutokana na ligi ilivyokuwa msimu ulioisha," anasema.
Naye Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi aliishukuru kampuni hiyo kwamba; "Kusema ukweli si rahisi kudhamini kwa kipindi hiki, tuwashukuru ndugu zetu kwa moyo walionao kuhakikisha wanatupa nguvu ya pesa kuhakikisha hatukwami kufanya mambo ya msingi," Alipoulizwa kwa nini Mbao FC  walifanya vibaya msimu ulioisha? Alijibu kwamba ligi ilikuwa ngumu lakini kwa msimu ujao wanajipanga kuona wanapambana na kuonyesha ushindani.
"Licha ya kwamba tulifanya vyema michuano ya Sports Pesa ila kwenye Ligi Kuu Bara, tulichemka kidogo lakini msimu ujao utakuwa wa mafanikio kwetu.
"Sababu nyingine ilikuwa ni kuondoka kwa wachezaji na kubadilisha makocha, hilo lilitufanya tuwe na maamuzi magumu kuwaambia wachezaji ambao hawati kuendelea na sisi waondoke kwa moyo mmoja.
"Wameondoka tutasajili upya ambao watakuwa wapo tayari kuisaidia Mbao FC, tumeanza na tunaendelea na zoezi hilo," anasema.