GEORGE MASATU : Simba tulikesha tukiwaroga Stella Abidjan-3

Wednesday May 15 2019

 

By Mwanahiba Richard

KATIKA sehemu mbili zilizopita za makala haya na beki wa kati wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Simba na Taifa Stars, George Magere Masatu, alisimulia masahibu yaliyomfika hadi sasa kuwa dereva wa gari la mizigo wakati alishacheza pia soka la kulipwa kwa miaka saba Indonesia akilipwa mkwanja mrefu. Tuungane katika sehemu hii ya tatu.

GULAMALI AGONGA MWAMBA

Kutokana na kiwango bora cha Masatu wakati ule, mfadhili wa Yanga wakati huo, Abbas Gulamali, alivutika na kuanza harakati za kutaka kumsajli beki huyo ambaye alianza kuingia kwenye mstari wa kutua Jangwani.

Hata hivyo, anakumbuka ghafla dili likaharibiwa na watani wao Simba baada ya aliyekuwa mfadhili wao, Azim Dewji, kutoa kibunda cha Sh3 milioni.

“Kwenye soka kuna mambo mengi sana, wakati nataka kusajiliwa Yanga, Dewji alisikia huo mpango, alinitumia tiketi za ndege fasta nikaja Dar es Salaam wakati huo nilikuwa timu ya Taifa, Dewji aliniahidi kunipa Sh3 milioni, nilikubali na tulirudisha fedha za Gulamali kwani tulikuwa hatujaitumia.

“Niliomba ruhusa kwa kocha wa timu ya taifa wakati huo alikuwa Zacharia Kinanda, nikaja Dar nikamaliza kila kitu nikarudi kambini na huo ukawa mwanzo wa mimi kuchezea Simba.”

Advertisement

HUJUMA SIMBA, STARS

Mbali na kumbukumbu zinazomuumiza kwenye maisha yake ya kawaida, Masatu anasema hata katika soka anaumizwa za historia mbaya ya kutuhumiwa kuzihujumu Taifa Stars na Simba, tuhuma zilizomhusu yeye na rafiki yake, Hussein Masha. “Nilituhumiwa nikiwa Taifa Stars nilijifanya nimeumia ili nisicheze mechi ili nije kucheza mechi ya Simba na Yanga huku wakisema Dewji ndiye aliyenishawishi nijifanye nimeumia.

“Ukweli, niliumia wakati naokoa bao Stars ikicheza dhidi ya Ivory Coast, kipa Steven Nemes, alitoka golini, hivyo ilikuwa ni lazima nikimbie na kwenda kuokoa bao na kujikuta mguu wangu ukijigonga kwenye mwamba wa goli na kuumia mguu wa kulia.

“Nilisikia maumivu kwa ndani, jambo ambalo lilisabisha mguu kuvimba taratibu na mtu mwingine haikuwa rahisi kugundua kama nimeumia,” anasema na kuongeza.

“Nililazimishwa kucheza na viongozi wa FAT wakati huo (sasa TFF), lakini nilishindwa kabisa na kuwaambia ukweli siwezi kucheza nina maumivu makali, hapo ilibaki siku chache mechi ya Simba na Yanga ichezwe, kweli sikuchezea Stars na walikasirika sana na kunituhumu moja kwa moja bila kificho.

“Usiku maumivu yalikuwa makali mno, nilimwita daktari wa timu, Dk Seleman ambaye aliniambia tatizo langu ni kubwa hivyo nipelekwa Hospitali ya Agakhan ambako pia walisema kesi yangu ni kubwa niende Muhimbili, cha ajabu nilibaki Mwanza bila kupata huduma yoyote kutoka FAT kwa wakati huo.

“Hiyo ni kwa sababu waliamini nilikuwa na mpango wa kuihujumu timu ya Taifa Stars kwa kushirikiana na Dewji ili nicheze mechi ya Simba na Yanga. Matokeo katika mechi hiyo Taifa Stars dhidi ya Ghana ilikuwa ni sare ya mabao 2-2,” anasema.

HUJUMA STELLA ABIDJAN

Mashabiki wa soka nchini wanaikumbuka sana mechi ya fainali ya Kombe la CAF Afrika kati ya Simba na Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Simba iliyokuwa katika kiwango cha juu na baada ya kulazimisha sare ya 0-0 ugenini Ivory Coast, wengi waliwapa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo katika mechi ya marudiano Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0 yaliyofungwa na Kouame Desire (dk.17) na Jean Boli Zozo (dk. 77) na kuzua tuhuma nyingi ikiwamo mada Masatu, kipa Mohamed Mwameja na kiungo Hussein Masha, waliihujumu timu kwa kushirikiana na Azim Dewji ili kumwepushia mfadhili huyo ‘balaa’ la kutimiza ahadi ya kutoa gari kubwa la mizigo aina ya KIA kwa mchezaji kama timu ingetwaa ubingwa huo wa Afrika.

“Tulituhumiwa lakini hakikuwa kitu cha kweli, mambo kama hayo huwa yanatokea sana katika soka hasa timu zinapofanya vibaya.”

USHIRIKINA SIMBA

Masatu anasema wakati wanajiandaa na mechi dhidi ya Stella Abidjan, walipiga kambi yao Zanzibar na wakiwa huko yalifanyika mambo mengi tu yakiwamo mambo ya ushirikina ili washinde mechi hiyo.

“Tulirudi Dar siku ya mechi, masharti tuliyopewa na mganga wakati wa kisomo yalikuwa kiboko, mganga alituambia tukishuka Uwanja wa Ndege tusipite barabara ambayo ina makutano wala tusipite barabara yenye lami.

“Tulishuka uwanja wa ndege saa 4 asubuhi, ilibidi tupitie njia ya Segerea ambayo ilikuwa ya vumbi na haina makutano kwa maana njia panda nne, tulizunguka barabarani saa mbili nzima mpaka kufika Tabata baadaye uwanja wa Uhuru tukiwa tumechoka sana maana hata kisomo chenyewe hakikuwa na mapumziko, wiki nzima tunasomewa tu.

“Hiyo mechi ya marudiano dhidi ya Stella Abidjan tuliingia tumechoka, tukapigwa 2-0. Haya mambo ya ushirikina ni imani tu lakini hayasaidii timu kupata matokeo.”

Usikose kusoma Mwanaspoti kesho upate sehemu ya mwisho ya Makala haya ambaPo Masatu anafunguka kuhusu BIFU NA wachezaji wenzake.

Advertisement