Dk 60 za Morrison vs Yanga TFF moto

ILE filamu ya winga Bernard Morrison na klabu yake ya Yanga imefikia patamu baada ya nyota huyo na mabosi wake, Yanga, kufikishana mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji jana katika makao makuu ya Shirikisho la Soka (TFF), huku Mghana huyo akitumia takriban dakika 60 kuhojiwa.

Yanga imempeleka Morrison katika shirikisho hilo kwa tuhuma za kutangaza hana mkataba Jangwani, huku ikielezwa anajazwa upepo na ushawishi wa fedha kutoka kwa watani wao wa Simba, ilhali naye akiukana mkataba wa miaka miwili baada ya ule awali wa miezi sita unaomalizika mwezi huu.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi katika ofisi za TFF kuanzia asubuhi kabla ya kesi ya pande hizo mbili na ile ya klabu ya Simba dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela juu ya kauli yake kwamba Yanga ilizungumza na Clatous Chama ili kumsajili, licha ya kuomba radhi akidai alitania.

VIGOGO WAWASILI

Mwanaspoti pia lilimshuhudia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa akifika ofisi za TFF saa 7:28 mchana akiwa na gari yake aina ya Benz na alitulia akiwasubiri wenzake garini.

Wakati Senzo akiwasubiri wenzake wafike, saa 8:08 mchana aliingia Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Mwakalebela na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick kisha walisalimiana na Senzo na kupiga stori mbili tatu huku wakitabasamu.

Viongozi hao walipofika bado kikao kilishindwa kuanza na badala yake waliendelea kusubiri nje mpaka wajumbe wengine walipofika na kikao kuanza.

Saa 8:17 mchana Mjumbe wa kamati hiyo, Zakaria Hans Pope alifika na kusalimiana na viongozi hao kisha moja kwa moja aliingia ndani, ambapo ilipofika 8:21 mchana aliwasili Bernard Morrisson akiwa na mkataba wake mkononi huku akiwa hana wasiwasi wowote.

Mchezaji huyo alikaa pembeni peke yake na muda wote alionekana kuwa ‘bize’ na simu huku akiwa hana habari na mtu yeyote.

KESI YA CHAMA

Saa 10:00 jioni Senzo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Patrick na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Mwakalebela waliingia ndani kwa ajili ya kesi ya Chama lakini walikaa kwa takriban dakika 25 na kutoka.

MORRISON DAKIKA 60

Ilipofika saa 10:25 jioni Morrison aliingia ndani kwa ajili ya kesi yake na kupishana mlangoni na Senzo na Mwakalebela waliotoka huku kila mmoja akiwa na lwake.

Baada ya kuingia kwa Morrison, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Patrick naye aliingia ndani.

Ukimya ulitawala eneo hilo hadi ilipofika saa 11:35 jioni Morrison alipotoka akiwa na mkataba wake mkononi kisha akaondoka na gari yake aina ya Harrier.

Mwanaspoti lilimfuata na kuzungumza naye, ambapo alisema kwa kifupi kuwa pande zote zimesikilizwa na kila kitu kitakuwa wazi.

“Kama nina mkataba basi itajulikana, kama sina mkataba basi pia itajulikana, lakini kwa sasa mimi ni mchezaji wa Yanga mpaka pale wenyewe watakaposema hawanitaki,” alisema mchezaji huyo.

ISHU YA SIMBA

Akizungumzia ishu yake anayodaiwa kusaini mkataba na Simba, alisema anawezaje kusaini huku akiwa ni mchezaji halali wa Yanga.

“Siwezi kusaini mkataba Simba halafu nikacheza Yanga, narudia tena kuhusu hilo la miaka miwili au miezi sita wote tutajua baada ya ligi kumalizika,” alisema.

Winga huyo aliongeza kuwa amekuja Tanzania kucheza soka na siyo kufanya jambo lingine lolote na kwamba, hata wakati kesi yake ikiwa inaendelea anatarajia kurejea kambini kwa safari ya kwenda kucheza mchezo dhidi ya Biashara Utd utakaochezwa Julai 5.

“Hapa kwenye kikao kilipokuwa kinachelewa kuanza nilikuwa nawauliza ili nijue napangiliaje ratiba yangu ya mazoezi kwani lazima nifanye mazoezi,” alisema.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Patrick alisema: “Tumesikiliza lakini bado mambo hayajakamilika, hivyo tunaendelea na kesi, kuna mambo ya kipolisi ambayo hayawezi kuzungumziwa.”

SENZO AFICHUA SIRI

Baada ya kutoka katika kikao hicho, Senzo alisema hawajafikia uamuzi wowote wa kesi yao na Mwakalebela kutokana na vitu vingi kutokukamilika.

Akizungumzia ishu ya Simba kumpa mkataba Morrison, alisema jambo hilo halipo kwa kuwa wanazijua kanuni na sheria zinazosimamia masuala ya mikataba ya wachezaji.

“Sisi tunajitambua kama Simba, hatuwezi kumpa mkataba mchezaji ambaye ana mkataba na timu yake hilo kwetu haliwezi kutokea hata kidogo,” alisema Senzo.

“Pia kuhusu mtu wa Simba kuzungumza naye halipo kwani mimi ndiye ninayesaini mikataba na hata mazungumzo ya mkataba (huwa) nafahamu.”

MWANJALA HUYU HAPA

Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala alisema uamuzi wa kesi hiyo unategemea uwasilishwaji wa ushahidi na kusikilizwa pande zote mbili, huku akifichua kuwa Morrison ndiye aliyefungua shauri akipinga kusaini mkataba wa miaka miwili.

“Kazi yetu ni kusikiliza na kupitia ushahidi ambao pande zote mbili zimewasilisha kwetu. Kama hautoshi, basi tutawapa muda zaidi, lakini kama tumeridhiswa tutatoa uamuzi, lakini sio leo (jana) kwani kuna malalamiko mengi ukiachana na hayo,” alisema Mwanjala.

Alisema kuwa mbali ya kesi hiyo, kamati yake pia inasililiza malalamiko yaliyowasilishwa na klabu ya Yanga dhidi ya Simba ikiwatuhumu kufanya mazungumzo na Morrison kinyume na utaratibu.

Mwanjala alisema Yanga inadai Morrison amekuwa akishawishiwa na Simba ajiunge nayo na kumchanganya kiasi cha kushindwa kutimiza majukumu yake katika klabu hiyo.

Alisema Yanga imewasilisha ushahidi wao kuhusiana na suala hilo ambapo Simba imefikisha utetezi wake.

“Kwa kifupi masuala yote haya tutayatolea uamuzi kesho (leo) kwani kuna mengi sana. Kuna suala la wachezaji kudai mishahara yao, masuala ya mikataba na kesi mbalimbali.”

IMEANDIKWA NA THOMAS NG’ITU, KHATIMU NAHEKA NA MAJUTO OMARY