Fifa yafuta mpango wa kuongeza timu 48 Kombe la Dunia 2022

Thursday May 23 2019

 

Geneva, Uswisi. Shirikisho la Soka Duniani Fifa limesitisha mpango wa kuongeza nchi zitakazoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2022 hadi timu 48.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino mwaka jana alisema mpango wa kuongeza timu hizo kutoka 32 ambao ungelianza kutekelezwa mwaka 2026 urudishwe nyuma hadi mwaka 2022.

Mabadiliko hayo yalimaanisha Qatar ambayo ndio mwandalizi wa mashindano hayo kushirikiana na mataifa mengine katika kanda hiyo.

Shirikisho hilo lilisema "baada ya mashauriano ya kina" tumeonelea mabadiliko hayo "hayawezi kutekelezwa kama ilivyopangwa awali".

Fifa imesema ilitathmini uwezekano wa Qatar kuandaa peke yake mashindano hayo ikiwa na timu 48, lakini ikaamua kusitisha mpango huo kutokana na changamoto ya ukosefu wa muda wa kutosha wa "kufanya ukaguzi wa kubaini athari ya hatua hiyo, matokeo yake na jinsi ya kushughulikia masuala ibuka."

Taarifa ya waandalizi wa Kombe la Dunia nchini Qatar ilisema: "Qatar ilikuwa tayari kutekeleza mpango huo katika mashindano ya mwaka 2022 na hatua iliyokua imefikia kufanikisha mpango huo ilikuwa umeafikiwa na na wadau wote.

Advertisement

Infantino, 46, ambaye alimrithi Sepp Blatter katia urais wa Fifa Februari 2016 alifanya kampeni akiahidi kupanua michuano hiyo.

Awali alipendekeza michuano ya timu 40, wazo lililowasilishwa na rais wa wakati huo wa Uefa, Michel Platini 2013, kabla ya kubadilisha msimamo na kuunga mkono michuano ya timu 48.

"Huku zikiwa zimesalia miaka mitatu na nusu kuelekea mashindano hayo, Qatar imejitolea kuhakikisha inaandaa Kombe la Dunia la mwaka 2022 ambalo litaifanya eneo zima la Uarabuni kujivunia."

Novemba, rais wa Uefa, Aleksander Ceferin alisema kuongeza timu 16 katika mashindano hayo ya Qatar 2022 huenda "ingelileta matatizo" na kuongeza kuwa mpango huo"hauwezekani".

Wale waliyo karibu na waandalizi wa mashindano hayo ya Qatar 2022 wanasema uamuzi wa pamoja ulikua umefikiwa kati yao na Fifa, lakini sasa wameamua kuangazia timu 32 zitakazoshiriki.

Uamuzi huo wa Fifa hata hivyo umewapunguzia waandalizi hao tumbo joto la kushirikiana na mataifa mengine kuandaa mashindano hayo maarufu duniani ikizingatia uhasama uliyopo kati ya taifa hilo na majirani zake.

Baadhi ya mashirikisho mengine ya soka ya kitaifa pamoja na Infantino huenda wakasikitishwa na uamuzi huo lakini wengine wengi wanaunga mkono hatua hiyo.

Historia ya Mabadiliko Kombe la Dunia

Kombe la Dunia   Timu

1930 Uruguay      13

1934 Italia     16

1950 Brazil    13

1954 Uswizi  16

1958 Sweden        16

1974 Ujerumani Magharibi       16

1982 Hispania      24

1986 Mexico 24

1998 Ufaransa     32

Advertisement