Fenerbahce nayo yanyatia dili la Samatta

Muktasari:

  • Mbali na kocha wa timu hiyo kuwa na mpango wa kumnasa Samatta pia, amehakikishiwa kupewa fungu nono la usajili ili kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ulinzi ambayo na yenyewe inaonekana kuwa na shida.

FENERBAHCE ya Uturuki nayo imejitosa kumfungia kazi nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye ni kinara wa mabao Ligi Kuu Ubelgiji kwa kuingiza jina lake kwenye ajenda zao majira ya kiangazi.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Uturuki vimeripoti kwa uzito mkurugenzi mpya wa michezo wa klabu hiyo, Damien Comolli amekutana na mmoja kati ya mawakala wa Samatta aitwaye, Louis Alonso.

Alonso ametajwa ni miongoni mwa mawakala wa nne wanaomsimamia mchezaji huyo aliyewahi kutesa kwenye soka la Afrika akiwa na TP Mazembe ya DR Congo.

Comolli ambaye pia ana taaluma ya ukocha na ugunduzi wa vipaji yaani skauti ameithibitishia Bodi ya Fenerbahce kuwa atahakikisha anamnasa mshambuliaji huyo wa Kitanzania.

Hii ni mara ya pili kwa habari za Samatta kuvuma kutakiwa Uturuki ambako anatazamwa atakuwa ni chaguo la kwanza la Kocha Ersun Yanal anayetaka kukiboresha kikosi chake.

Hali ni tete kwa Fenerbahce ambayo imepoteza kasi yake ya ushindani kwenye ligi ya Uturuki kutoka na ubutu kwenye safu yake ya ushambuliaji yenye mastaa kama vile André Ayew Pelé mwenye mabao matano kwenye michezo 22 na Roberto Soldado mwenye mabao matatu kwenye michezo 14.

Ubutu huo wa safu ya ushambuliaji umeifanya Fenerbahce kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, chama hilo limeshinda michezo sita, sare 10 na kupoteza tisa.

Mbali na kocha wa timu hiyo kuwa na mpango wa kumnasa Samatta pia, amehakikishiwa kupewa fungu nono la usajili ili kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ulinzi ambayo na yenyewe inaonekana kuwa na shida.

UZOEFU WA COMOLLI

Damien Comolli (aliyezaliwa Desemba 13 1972), ana uzoefu wa kutosha kwenye kusajili wachezaji wenye viwango vya juu, aliwahi kufanya kazi hiyo kwenye klabu kadhaa kubwa barani humo, zikiwemo Monaco, Saint-Étienne, Arsenal, Tottenham Hotspur na Liverpool.