Fedha TFF zang'oa kigogo Zanzibar

Tuesday July 7 2020

 

By MOSI ABDALLA, ZANZIBAR

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF),  Adam Natepe ametangaza kujiuzulu kwa madai mbalimbali ikiwemo kutoshirikishwa na viongozi wa juu wa shirikisho hilo katika suala la uombaji wa fedha kutoka Shiriksho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Natepe ambaye alichaguliwa na Rais wa ZFF, Seif Kombo Pandu, mara tu alipongia madarakani Juni 2 mwaka jana, amedai mabosi kuomba msaada huo ni sawa na kujishusha thamani hasa kwa kuwa wao wanalidai Shirikisho hilo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Natepe alisema zipo sababu nyingi zilizopelekea ajiuzulu  lakini kubwa zaidi ni kutoshirikishwa kwenye baadhi ya mambo likiwemo viongozi hao kwenda kuomba pesa TFF wakati wakiwa na madai yao ya msingi ya mgao wa FIFA.

“Nimeamua kujiuzulu kwa sababu najiangalia hali yangu ya kiafya lakini yapo baadhi ya mambo yanafanyika kwenye shirikisho hayajanifurahisha.Kwamba viongozi wenzangu wanatoka kwenda TFF kwenda kuomba msaada bila ya kushirikiana wakati tuna madai ya msingi kwao,” alisema Natepe

Alisema kulikuwa hakuna haja ya kuomba kwani TFF ni wajibu wao kuipa fedha, ZFF na sio kwenda kuomba msaada huo, na  yeye alikuwa mdau mkubwa wa kupigania haki hiyo ya fedha kutoka TFF.

Hata hivyo Natepe amesema katika kipindi alichokaa katika nafasi hiyo ameona mambo mengi yanafanyika kinyume na utaratibu, na hayana afya kwa mpira wa Zanzibar hususani katika vyama vya soka vya wilaya pamoja na kwenye soka la vijana, hivyo ameona akae pembani kwani lengo lake la  kulikuza soka la Zanzibar halitafanikiwa.

Advertisement

Hata hivyo kwa mujibu wa barua kutoka ZFF iliyosainiwa na kaimu katibu wa shirikisho hilo Ali Ameir, wamethibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa Natepe.

Advertisement