Federer, Djokovic kwenye mtego wa Messi na Ronaldo

UTATU mtakatifu kwenye mchezo wa tenisi ni huu wa wakali, Roger Federer, Rafael Nadal na Novak Djokovic ambao wameendeleza utawala wao wakivutana kama ilivyo upande wa soka ambapo kwa zaidi ya muongo uliopita umetawaliwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Ndio, wakali hawa wa tenisi kuanzia kwa Djokovic, Nadal hadi Federer kwa muda mrefu wamekuwa wakivutana wenyewe zaidi katika kuchukua mataji ya Grand Slam na hawaonekani kama wanaachia nafasi kwa chipukizi wapya waliokuja kuondoa utawala wao wa tenisi.

Ni bahti mbaya sana kama ilivyoshindikana kwa wachezaji wengi wa soka waliocheza katika himaya ya Messi na Ronaldo kama vile Neymar Jr,W esley Sneijder, Xavi Hernandez na hata Andres Iniesta ambao walitajwa kustahili kubeba tuzo binafsi za Ballon d’Or lakini wakashindwa kutokana na nyota hao wawili.

Mwisho wa enzi? Kama inavyowezekana ujio wa Kylian Mbappe na baadhi ya chipukizi wanaokuja juu kufunika utawala wa kina Messi ndivyo ambavyo alivyojitokeza bingwa wa zamani wa tenisi aliyeshinda mataji ya Wimbledon na zaidi medali za dhahabu mara mbili kwenye michezo ya olimpiki, Mjerumani Boris Becker aliyesema sasa ni zamu ya chipukizi kuhakikisha wanawapiga chini mastaa hao watatu.

Becker amewalenga na kuwataja chipukizi watatu wanaokuja juu kwenye tenisi ambao ni Stefanos Tsitsipas, Alexander Zverev na Daniil Medvedev kuhakikisha wanawashinda nyota hao wakati huu wakiwa bado wanacheza na sio kusubiri wastaafu.