FKF yafunguka kuhusu kipa mzungu kikosi Kenya

Thursday June 6 2019

 

By Fadhili Athumani

Nairobi.  Hatimaye Shirikisho la soka nchini (FKF), limetolea ufafanuzi uwepo wa Kipa mzungu Joel Drepper katika kikosi cha timu ya taifa, Harambee Stars, kilichojichimbia kambini, huko Paris Ufaransa kwa ajili ya kujiandaa na fainali za AFCON 2019, zitakafanyika huko Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Kwa mujibu wa mkuu wa mawasiliano wa FKF, Barry Otieno, kipa huyo Drepper hatokuwa katika kikosi cha wachezaji 23, kinachoenda Misri.

Licha ya kutokuwa miongoni mwa wachezaji 27, waliotajwa na Kocha wa Stars, Sebastien Migne, Drepper ambaye makazi yake yako Ujerumani, akiwa ni mzaliwa wa Kenya,  alionekana akifanya mazoezi na kikosi hicho, mambo lililozua sintofahamu miongoni mwa wapenda soka nchini.

Barry alisema kipa huyo wa zamani wa TV, Jahn Hiesfeld inashiriki ligi daraja la tano la Ujerumani, alikuwa anatizamwa uwezo wake kuona kama atafaa kwa ajili ya vikosi vya siku za usoni na kwamba tayari ameshaondoka tangu Jumatatu.

"Drepper hayupo katika kikosi cha Harambee Stars. Benchi la ufundi lilikuwa linamtazama kuona kama ataweza kutufaa katika siku za usoni. Tunavyoongea tayari ameshaondoka tangu Jumatatu, hayupo kambini," alisema Otieno.

Kikosi cha Migne, kitacheza mechi mbili za kirafiki ya kwanza, ikipigwa kesho (Juni 7), Jijini Paris dhidi ya Madagascar ya pili ikiwa ni dhidi ya DR Congo, itakayopigwa Juni 15, Jijini Madrid.

Advertisement

Stars, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal, Julai mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, katika uwanja wa June 30.

Kikosi cha Stars:

Makipa: Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo

Mabeki: Abud Omar, Joash Onyango, Joseph Okumu, Musa Mohammed, David Owino, Bernard Ochieng, Brian Mandela, Philemon Otieno, Eric Ouma

Viungo: Victor Wanyama, Anthony Akumu, Ismael Gonzalez, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ovella Ochieng, Dennis Odhiambo, Eric Johanna, Paul Were, Cliffton Miheso, Johanna Omollo

Mastraika: John Avire, Masud Juma, Christopher Mbamba, Michael Olunga

Advertisement