Eti Ozil kukaa benchi anajitakia

LONDON, ENGLAND. KIUNGO, Mesut Ozil ameambiwa kwamba ni yeye mwenyewe wa kujilaumu kutokana na kuweka benchi huko Arsenal.

Kwa mujibu wa staa wa zamani wa Arsenal, aliyekuwa kwenye kikosi cha miamba hiyo kilichocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England, Lauren -Etame Mayer, alisema wachezaji wengi wa kiwango cha dunia wamekuwa wakijiangusha wenyewe na kwamba Ozil si staa wa kwanza kuondoshwa kikosini na kocha wake.

Ozil ni mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Arsenal na ni mmoja wa mastaa wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi hicho cha Emirates, akilipwa Pauni 350,000 kwa wiki.Staa huyo amepigwa chini kwenye vikosi vyote vya Arsenal vitakavyocheza kwenye Europa League na Ligi Kuu England msimu huu. Ozil hivi karibuni alifichua jinsi alivyoumizwa na kitendo hicho cha kuwekwa kandi akiishutumu Arsenal kushindwa kuwa waungwana.

Lakini, Lauren hataki kuwalaumu Arsenal kwenye jambo hilo na badala yake amemwonyeshea kidole Ozil. “Ozil ni mchezaji wa daraja la juu, inasikitika kuona mchezaji wa daraja kama lake hashirikishwi kwenye timu kama Arsenal,” alisema Lauren.

“Sisi sote tunaowafuatilia Arsenal tunapenda kuwaona wachezaji bora.”