Eti Mo Salah akiuzwa sio ishu

Muktasari:

Mabao hayo yanamwingiza kwenye orodha ya wanaofukuzia Kiatu cha Dhahabu kwa msimu huu na kama atashinda basi itakuwa mara yake ya tatu mfululizo baada ya kushinda kwenye misimu miwili iliyopita.

LIVERPOOL, ENGLAND . GWIJI wa Liverpool, Jamie Carragher amesema mashabiki wa timu hiyo watakuwa tayari kusapoti mauzo ya straika Mohamed Salah kama kutawekwa mezani mkwanja wa maana bila ya kujali ni mchezaji wa kiwango cha dunia.

Kwa mujibu wa beki huyo wa zamani wa Anfield, mashabiki wa Liverpool hawamkubali sana Mo Salah kwa kulinganisha na mastaa wengine kwenye kikosi hicho.

Mo Salah alifunga bao lake la 15 kwenye Ligi Kuu England juzi Jumatatu wakati alipoisaidia Liverpool kutokea nyuma kwa mabao 2-1 na kushinda 3-2 dhidi ya West Ham United ushindi unaowasogeza kabisa kwenye kubeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England.

Mabao hayo yanamwingiza kwenye orodha ya wanaofukuzia Kiatu cha Dhahabu kwa msimu huu na kama atashinda basi itakuwa mara yake ya tatu mfululizo baada ya kushinda kwenye misimu miwili iliyopita.

Alishinda kwenye msimu wake wa kwanza alipofunga mabao 32 msimu wa 2017/18 kisha msimu uliofuatia aligawana tuzo hiyo na wakali wengine, Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal na mchezaji mwenzake wa Liverpool, Sadio Mane baada ya kila mmoja kufunga mabao 22.

Lakini, Carragher anaamini Mo Salah ndiye mchezaji ambaye mashabiki wa Liverpool watachagua kumuuza ikiletwa ofa ya maana.

“Ukitazama alichokifanya kwenye msimu wa kwanza na hivi sasa, ameonekana kushuka. Huoni kama ataweza kufunga tena mabao 47 kwa msimu mmoja,” alisema Carragher.

“Ukizungumza na mashabiki wa Liverpool kwenye mitandao ya kijamii, watakwambia wana wachezaji sita wa kiwango cha dunia, kipa Alisson, Trent Alexander-Arnold, Virgil van Dijk, Sadio Mane, Roberto Firmino na Salah. Lakini, ukiwaambia wachague mchezaji wa kuuzwa, hawawezi kumuuza Alisson au Van Dijk.

“Lakini, kama watapewa ofa ya Pauni 130 milioni kwa ajili ya Salah, watafanya biashara. Ndio maana nasema hawamkubali sana.”

Carragher anawashangaa mashabiki wa Liverpool kwa kutomkubali sana mchezaji aliyewafungia mabao 90 katika mechi 140.