Erasto Nyoni awavimbia AS Vita

Muktasari:

Bao walilotanguliwa Simba mwanzoni mwa kipindi hicho cha kwanza lilitokana na uzembe wa kushindwa kuondoa mpira uliokuwa ukizagaa kwenye eneo lao la hatari.

BAO la kusawazisha la beki wa kushoto, Mohammed Hussein 'Tshabalala' dakika ya 36 liliirejesha Simba mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Beki Erasto Nyoni ameendelea kuonyesha ukomavu. Nyoni ameibeba Simba kwenye idara yao ya ulinzi kwa kuokoa hatari kadhaa zilizokuwa zikitokea upande wa Tshabalala ambaye alikuwa akikatika.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Simba na As Vita ya DR Congo kwenda sare ya bao 1-1, na hadi dakika tisini Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Simba waliuanza mchezo huo vizuri ndani ya dakika 10 za mwanzo kwa kuwa na umiliki mkubwa wa mpira hadi pale ambapo walipotanguliwa dakika ya 13 kwa bao la Kasendu Kazadi.

Bao walilotanguliwa Simba mwanzoni mwa kipindi hicho cha kwanza lilitokana na uzembe wa kushindwa kuondoa mpira uliokuwa ukizagaa kwenye eneo lao la hatari.

Baada ya kutanguliwa utulivu kwenye kikosi cha Simba ulipotea kiasi cha kuanza kuonekana tatizo kwenye eneo lao la kiungo mkabaji ambalo alikuwa akicheza James Kotei na Mzamiru Yassin.

Kupwaya kwa eneo hilo kuliwapa nguvu AS Vita ambao walikuwa wakiishambulia Simba kwa mshambulizi mfululizo kupitia kwa wadhambuliaji wao, Tuisila Kisinda, Jean Makusu na Kazadi. Simba walizinduka dakika ya 36 baada ya kusawazisha bao kupitia kwa Tshabalala ambaye alimalizia mpira ambao mabeki wa AS Vital walijaribu kuukoa lakini jitihada zao hazikusaidia.

Mara baada ya kusawazisha bao hilo, Simba walizinduka na AS Vita wakaanza kucheza kwa kujilinda zaidi ndani ya dakika 10 za mwishoni mwa kipindi hicho cha kwanza.