Emery anajiamini kumnasa Carrasco

Muktasari:

Shida nyingine inayowakabili Arsenal ni Dalian, ambao wao wanaona ni vyema tu wakamuuza jumla Carrasco kwa Pauni 26 milioni, wakati Emery anamtaka mchezaji huyo kwa mkopo wa msimu mzima wenye kipengele cha kumsajili jumla mwakani.

LONDON, ENGLAND.KOCHA wa Arsenal, Unai Emery bado anapanga mambo yake ya usajili kimyakimya huku akiwa mwenye uhakika mkubwa wa kumnasa winga wa Kibelgiji, Yannick Carrasco kutoka Dalian Yifang.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 25, Carrasco anataka kurudi Ulaya na kuachana na soka la China, huku jina lake likihusishwa na klabu kibao zinazohitaji saini yake.

Kocha Emery anataka kukiboresha kikosi chake hasa kwenye wingi baada ya kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Lakini, Emery asijisahau sana kwenye mbio za kumnasa mchezaji huyo baada ya Bayern Munich nao kumhitaji baada ya kuona wanawekewa ngumu na Manchester City kwa usajili wa Leroy Sane wakiwaambia walipe Pauni 90 milioni.

Shida nyingine inayowakabili Arsenal ni Dalian, ambao wao wanaona ni vyema tu wakamuuza jumla Carrasco kwa Pauni 26 milioni, wakati Emery anamtaka mchezaji huyo kwa mkopo wa msimu mzima wenye kipengele cha kumsajili jumla mwakani.

Carrasco mwenyewe alisema: “Dunia nzima inafahamu kwamba nataka kurudi Ulaya. Kwa sasa, kila kitu kinasubiri kuona rais na mimi tutalimalizaje hili.”

Alipoulizwa kuhusu Arsenal, alijibu "Siwezi kusema kuhusu timu. Mimi sichagui timu, rais ndiye anayefahamu. Yeye ndiye atakayeamua kuniruhusu niondoke au la, lakini naamini nitarudi Ulaya."

Carrasco aliwashangaza wengi kwa kuhamia China sambamba na mchezaji mwenzake wa Atletico Madrid, Nicolas Gaitan, Februari mwaka jana na usajili huo ulikuwa mwepesi kwa sababu kampuni ya Wanda inaimiliki timu ya Dalian na inamiliki pia sehemu ya Atletico.