Emery aambiwa ambebe Rabiot

Monday April 15 2019

 

PARIS, UFARANSA.GWIJI wa Arsenal, Mfaransa Robert Pires amedai kwamba kocha Unai Emery ndiye mwenye nafasi kubwa ya kunasa huduma ya kiungo Adrien Rabiot na kumvuta huko Emirates kwa sababu ya ukaribu wake na Paris Saint-Germain kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Rabiot alikuwa kwenye mipango ya klabu nyingi za Ligi Kuu England kwenye dirisha la Januari, lakini dili hizo zilishindwa kukamilika na mchezaji huyo akaamua kubaki PSG.

Staa huyo Mfaransa bila shaka amekuwa na kipaji kikubwa sana, lakini huko kwenye kikosi cha PSG hajachezeshwa tangu Desemba mwaka jana wakati alipopewa dakika chache sana kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Crvena Zvezda. Kutokana na Rabiot kuondolewa kwenye mipango ya kocha Thomas Tuchel hakuna ubishi itabidi afungue tu mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu hasa ikizingatiwa kwamba mkataba wake utakuwa umefika mwisho.

Wakati klabu nyingi zikipambana kupata saini yake, Pires anaamini Arsenal ndio wenye nafasi kubwa kutokana na kocha Emery kuwa na ukaribu na mchezaji huyo ambaye aliwahi kumnoa huko nyuma.

“Rabiot ni mchezaji mzuri sana na Arsenal wanapaswa kujaribu kumsajili mchezaji huyo kabla ya timu nyingine kumuwahi,” alisema Pires. “Arsenal wana faida moja ya kuwa na Emery ambaye walikuwa pamoja PSG, kitu ambacho kinaweza kumshawishi Rabiot akaenda kujiunga na Arsenal. Kama Emery atapata huduma yake atakuwa ameliziba vyema pengo litakalokuwa limeanza na Aaron Ramsey.”

Emery amekuwa akizungumza kwamba anataka kuongeza kiungo mpya kwenye kikosi chake ili kukifanya kuwa na nguvu ya kushindania ubingwa wa Ligi Kuu England na Rabiot anaweza kuwa na msaada mkubwa kwao huku ikizingatiwa kwamba mchezaji huyo anapatikana bure kabisa.

Advertisement

Advertisement