Emery, Rodgers vitani Arsenal

Saturday November 9 2019

 

LEICESTER, ENGLAND . INASEMAKANA lakini, kuwa kuna kundi kubwa la mashabiki wa Arsenal wanamtaka Brendan Rodgers kwenda kumbadili Unai Emery kwenye kiti cha ukocha cha miamba hiyo ya Emirates.

Kitu kizuri ni kwamba jambo hilo limekuja wakati mwafaka, Emery anakutana na Rodgers huko King Power kwenye Ligi Kuu England leo Jumamosi.

Mashabiki wa Arsenal wapatao 30,000 wanatarajia kwenda King Power kuishangilia timu yao itakapokipiga na Leicester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, mechi ambayo watapata majibu ya kwamba, nani bora kati ya Emery na Rodgers msimu huu.

Kwenye Ligi Kuu England, Leicester City ya Rodgers ipo nafasi ya tatu na pointi zake 23, wakati Arsenal ya Emery ipo nafasi ya tano na pointi zake 17, tofauti na pointi sita.

Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanaripotiwa kumtaka Rodgers, aliyewahi kuinoa pia Liverpool. Lakini mchezo huo wa leo Jumamosi, utatoa taswira halisi ya nani anayestahili kuwapo huko Emirates, Emery aliyepo kwa sasa au Rodgers anayepigiwa debe kutua.

Leicster mechi nane zilizopita, imeshinda saba na kupoteza moja tu, ilipopigwa kwa mbinde na Liverpool, ikishinda kwa penalti ya James Milner dakika ya 95.

Advertisement

Zaidi ya hapo imetoa vipigo vizito vikiwamo vya 5-0 dhidi ya Newcastle United na 9-0 dhidi ya Southampton.

Arsenal mechi zake nane zilizopita, imeshinda tatu tu, imepigwa moja na kutoka sare zilizobaki.

Mbaya zaidi, sare inazopata, yenyewe ndio inatangulia kufunga na wapinzani wanakuja kusawazisha kirahisi tu.

Kwenye mchezo uliopita, Arsenal ilipocheza na Vitoria iliyoonyesha udhaifu mkubwa ilipopata sare ya 1-1, huku Wareno hao wakisawazisha kwa bao ambalo mfungaji alifunga mbele ya wachezaji wanane wa Arsenal waliokuwa kwenye goli lao.

Katika mechi hiyo, Arsenal ilipiga pasi sahihi 520 kati ya 579, lakini kitu cha ajabu hakuna hata pasi moja iliyopigwa ndani ya boksi la Vitoria. Jambo hilo limewakwaza mashabiki na kufanya kelele kuwa nyingi za kumtaka aondoke ili timu apewe Rodgers. Arsenal imefunga mabao 16 tu katika mechi 11, ikiwa imeachwa kwa mbali sana na timu za Top Four kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Liverpool, Manchester City, Leicester na Chelsea.

Kitendo cha kumshindwa kumtumia vyema fundi wa asisti Mesut Ozil, kimekuwa ni kitu kingine ambacho kitamponza Emery asipojiangalia.

Matokeo yoyote ya kupigwa au sare huko King Power kwenye mechi ya leo bila ya shaka itakuwa imemsogea Emery karibu zaidi na mlango wa kutokea huko England.

Mechi nyingine za Ligi Kuu England zitakazopigwa leo Jumamosi, Chelsea itakuwa Stamford Bridge kuikaribisha Crystal Palace, Burnley itacheza na West Ham United na Newcastle itakuwa mwenyeji wa Bournemouth. Southampton itakwaruzana na Everton na Sheffield United itatoka kuifuata Tottenham Hotspur, kabla ya kesho Jumapili kuwashuhudia Manchester United wakiwa nyumbani Old Trafford kucheza na Brighton, Wolves wakipepetana na Aston Villa kabla ya kipute kile matata kabisa cha huko Anfield, wakati wapinzani wawili kwenye mbio za ubingwa, Liverpool watakapokipiga na Man City.

Advertisement