Duh! Corona yawalaza ndani Luis, Niyonzima

Saturday March 21 2020

Corona yawalaza ndani Luis, Niyonzima,HARUNA Niyonzima wa Yanga , winga wa Simba,

 

By Thobias Sebastian

HARUNA Niyonzima wa Yanga na winga wa Simba, Luis Jose Miquissone, kila mmoja kwa nafasi yake amejifungia ndani katika nyumba yake akihofia virusi vya Corona.

Niyonzima alieleza mara baada ya kupata taarifa za ugonjwa huo kuingia nchini alianza kuwa na tahadhari kubwa ambapo hata majirani zake anakoishi Mikocheni hataki kusogeleana nao.

“Nimeamua kukaa ndani muda wote ili kukwepa mikusanyiko ya watu ambayo ni chanzo kimojawapo cha ugonjwa huu hatari, hata familia yangu nayo inaendelea kuishi katika mazingira salama,” alisema Niyonzima ambaye alisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili katika dirisha dogo akitokea AS Kigali ya Rwanda.

Lakini Luis wa Simba alisema; “Katika kipindi hiki cha Corona nimekuwa ndani ya nyumba yangu zaidi ya awali kwani tangu nimeingia ndani siku ya mwisho ambayo tulitoka mazoezini Jumatatu mpaka sasa sijatoka nje ya geti na kwenye nyumba naishi mwenyewe kwa kuogopa muingiliano wa watu tofauti.”

“Nafanya hivyo ili kujikinga na maambukizi haya ya Corona lakini kama ikitokea nataka vocha huwa nanunua kupitia simu yangu lakini mahitaji mengine yote ya msingi kama chakula, maji na mambo mengine yote yapo ya kutosha ndani ya nyumba yangu na kazi kubwa ambayo naifanya wakati huu ni kutumia tu.

“Familia yangu Msumbuji inaishi vizuri na wanaendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na hakuna mtu wangu wa karibu ambaye amepata shida au kuhisi dalili yoyote ya Corona ambayo imekuwa shida katika maeneo yote duniani ila kwangu licha ya kujifungia ndani huwa nafanya mazoezi yangu mepesi asubuhi na jioni ili kuweka mwili sawa.

Advertisement

“Nimeomba uongozi ruhusa ya kwenda nyumbani Msumbiji na umenikubalia ila ambacho nasubiri wakati huu ni tiketi ya ndege tu ya kuondoka na muda wowote kuanzia sasa nitakuwa safarini kwenda kuangalia familia walau kwa siku saba,” alisema Luis, ambaye alisajiliwa na Simba katika dirisha dogo kwa mkataba wa miaka minne akitokea UD Songo ya Msumbiji alikokuwa kwa mkopo.

Advertisement